Ulimwengu wa Michezo, Februari 13
Mkusanyiko wa matukio kemkem ya spoti ndani ya siku saba zilizopita......................
Debi la Tehran, Esteghlal yang'ara
Klabu ya Esteghlal imetwaa ushindi katika Debi la Tehran ambalo pia linafahamika kama Debi la Sarkhobi, baada ya kuikung'uta Persepolis mabao 3-2 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Soka ya Iran, hii ikiwa ni mara ya 84 kwa watani hawana wa jadi kuchuana. Katika kipute hicho kilichopigwa mbele ya mashabiki 70 elfu katika Uwanja wa Taifa wa Azadi hapa Tehran siku ya Jumapili, vijana wa mkufunzi Alireza Mansourian walidhihirisha kuwa wao ni moto wa kuotea mbali licha ya kibaridi kikali kilichokuwa kikishuhudiwa wakati wa mchuano huo wa Sarkhobi (Mechi ya Wekundu na The Blues). Kiungo wa The Reds Soroush Rafiei alikuwa wa kwanza kutikisa nyavu kupitia bao lake la mapema, dakika 5 baada ya kupulizwa kipenga cha kuanza mechi.
Na kwa kuwa kutangulia sio kufika, Esteghlal walipata mpenyo na kusawazisha mambo kunako dakika ya 17 kupitia Farshid Esmaeili. Dakika 3 baadaye The Blues waliongeza la pili baada ya Ali Ghorbani kufunga kwa kichwa. Katika dakika za lala salama kipindi cha kwanza, Kaveh Rezaei wa Persepolis alicheka na nyavu baada ya kupokea pasi ya juu kwa juu kutoka kwa mchezaji wa safu ya kati, Omid Noorafkan, na hadi wanaenda mapumzikoni, ilikua ngoma draw. Kipindi cha pili kilishuhudia mchezo wa kasi na kivumbi kutifuka uwanjani. Nahodha wa Esteghlal Seyyed Jalal Hosseini, alipiga msumari mwa mwisho kwenye jeneza la Esteghlal kunako dakika ya 93, kabla ya kipa wa The Blues kupigwa kadi ya pili ya njano, na kulazimika kuondoka uwanjani. Licha ya kichapo hicho, Persepolis wanasalia kileleni mwa Ligi Kuu ya Soka nchini, wakiwa ana alama 47, pointi 6 mbele ya Teractor Sazi, huku tatu bora ikifungwa na Esteghlal wenye alama 37.
Klabu Bingwa Afrika; Yanga yaidhalilisha Comoro
Michuano ya soka mzunguko wa kwanza kuwania taji la Klabu Bingwa barani Afrika mwaka 2017 ilianza kurindima siku ya Ijumaa. Baada ya kuishia hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika msimu uliopita, Mabingwa wa Tanzania bara Dar es Salaam Young Africans Yanga, walicheza mchezo wao wa kwanza wa duru ya kwanza ugenini dhidi ya klabu ya N’gaya ya Comoro siku ya Jumapili. Yanga waliingia kucheza dhidi ya N’gaya wakiwa na tahadhari kubwa kwa mujibu wa kocha wao msaidzi Juma Mwambusi. Kikosi cha N’gaya licha ya kujumuika na wachezaji 5 wa kimataifa, watatu wakitoka Kodivaa na wawili wakitokea Madagascar, walikubali kipigo cha mbwa cha mabao 5-1 kutoka Yanga. Magoli ya wawakilishi hao wa Tanzania yalifungwa na Justine Zulu, Simon Msuva, Obrey Chirwa, Amissi Tambwe na Thabani Kamusoko. Goli la kufutia machozi la N’gaya lilifungwa na Said Anifane. N’gaya watarudiana na Yanga baada ya wiki moja uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Klabu ambazo zimefuzu katika mzunguko wa kwanza ni pamoja na USM Alger ya Algeria, Etoile du Sahel na Esperance de Tunis za Tunisia. Timu nyingine ni pamoja na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Wydad Casablanca ya Morocco, Zamalek na Al-Ahly ya Misri, TP Mazembe ya DRC na Al-Hilal ya Sudan. Ifahamike kuwa mabingwa watetezi wa taji hili ni Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Riadha: Wakenya watamba Uhispania
Wanariadha wa Kenya Florence Kiplagat na Leonard Langat wametwaa ubingwa wa mbio za Barcelona Half Marathon mwaka huu 2017 nchini Uhispania, siku ya Jumapili. Hata hivyo, juhudi za Kiplagat kutaka kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 ya saa 1:05:06 ziligonga mwamba. Kiplagat alishinda taji, lakini zaidi ya dakika tatu nje ya rekodi ya dunia, ambayo Mkenya Peres Jepchirchir aliweka Februari 10 alipotwaa taji la Ras Khaimah Half Marathon huko Imarati. Kiplagat, ambaye ni mshindi wa Chicago Marathon mwaka 2016, alitumia saa 1:08:15 kunyakua taji lake la tatu la Barcelona Half Marathon. Kiplagat, 29, alitamalaki rekodi ya dunia ya Half Marathon mara mbili kabla ya Jepchirchir kuivunja. Alivunja rekodi ya dunia ya Mkenya Mary Keitany ya 1:05:50 mwaka 2014 aliposhinda Barcelona Half Marathon kwa saa 1:05:12 na kufuta rekodi yake mjini Barcelona mwaka 2015 aliposhinda taji lake la pili kwa 1:05:09. Naye Langat, ambaye ni bingwa wa Cologne Half Marathon mwaka 2010, alishinda Barcelona Half Marathon kwa saa 1:00:52. Aliongoza Wakenya wenzake Meshak Koech, Joel Kimurer na bingwa wa Chicago Marathon mwaka 2016, Abel Kirui, kufagia nafasi nne za kwanza.
Maafa uwanjani nchini Angola
Kwa akali mashabiki 17 wa soka walipoteza maisha kutokana na mkanyagano na msongamano katika uwanja wa soka nchini Angola Ijumaa hii. Duru za polisi na hospitali nchini humo zimethibitisha kutokea mkanyangano huo katika uwanja wa Januari 4 kaskazini mwa nchi, ambapo mashabiki zaidi ya 50 walijeruhiwa.
Orlando Bernardo, msemaji wa polisi nchini humo amethibitisha habari hizo na kuongeza kuwa, mkanyangano huo ulisababishwa na baadhi ya mashabiki wa soka kujaribu kutumia kifua kuingia bila tiketi katika uwanja huo kushuhudia mchuano wa ligi ya ndani, kati ya timu ya Santa Rita de Cassia na Recreativo de Libolo. Serikali imeagiza kuanzishwa uchunguzi juu ya mkasa huo huo idara ya polisi ikishutumiwa kwa uzembe na utepetevu. Itakumbukwa kuwa, watu 127 waliuawa katika mkanyagano mwingine katika uwanja wa michezo wa Accra nchini Ghana mwaka 2001; na miaka miwili kabla ya hapo, wengine 19 walifariki dunia kwenye mkanyangano mwingine mjini Abidjan, katika mchuano wa kusaka tiketi ya kushikiri Kombe la Dunia 2010, kati ya Malawi na Kodivaa. Ajali mbaya ya mkanyagano iliwahi kushudiwa katika Uwanja wa Taifa wa Lima, katika mechi kati ya Peru-Argentina Mei mwaka 1964, ambapo watu 324 waliaga dunia, huku wengine zaidi ya 1000 wakijeruhiwa.
Ligi ya EPL
Bingwa mtetezi wa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, Leicester City wameendelea kuwa na msimu mbaya kwa kupoteza mchezo wa tano mfululizo. Siku ya Jumapili Leicester ilikubali kichapo cha mabao 2-0 ikiwa ugenini kuvaana na Swansea City. Mabao ya Swansea yalifungwa na Alfie Mawson na Martin Olsson.
Kipigo hiki kimemshusha bingwa huyo mtetezi wa ligi katika nafasi ya 17 kumweka katika hatari ya kushushwa daraja. Kwengineko Chelsea ilipoteza fursa ya kuongoza jedwali la ligi kwa pointi 12 baada ya kukazimishwa sare ya bao 1-1 na Burnley. The Blues wa Uingereza waliitawala mechi na ndio walikuwa wa kwanza kuona lango la Burnley dakika ya 7 baada ya kuanza mgaragazano. Huku hayo yakijiri, kiungo mahiri Alexis Sanchez alitikisa nyavua mara mbili na kuisaidia Arsenal kuibwaga Hull City mabao 2-0. Hata hivyo bao la kwanza la Sanchez lilizusha utata huku refa akilaumiwa, kwa kuwa mpira ulionekana umemgonga mkono kabla ya kuingia katika dakika ya 34. Sanchez aliongeza bao la pili kupitia mkwaju wa penalti uliotolewa katika dakika za ziada baada ya Sam Clucas kutolewa nje kwa kushika kichwa cha Lucas Perez kilichokaribia kuingia katika goli.
Kichapo kama hiki kwa Hull City cha 2-0 kilipokewa na Watford iliposhuka dimbani kuvaana na Manchester United. Mabao ya Man U yalifungwa na Juan Mata katika dakika ya 31, huku Anthony Martial akipiga msumari wa mwisho kunako dakika ya 60, na kuupa maana msemo usemao mcheza kwao hutuzwa.
Licha ya ushindi huo, Man U wapo katika nafasi ya 6 kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na alama 48. The Blues wanasalia kileleni mwa jedwali la ligi wakiwa na alama 60, mwanya wa alama 10 kati yao na Tottenham na Arsenal ambao wanabanana katika nafasi ya pili na ya tatu. Liverpool licha ya kuinyoosha Tottenham mabao 2-0, inalazimika kuridhika na nafasi ya nne kwa sasa ikiwa na pointi 49, alama sawa na Man City waliyeko katika nafasi ya 5, wakisubiri kuvaana na Bournmouth.
....................................................TAMATI.......................................