Feb 14, 2017 12:14 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (147)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi cha juma hili cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kinakujieni moja kwa moja kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka hapa mjini Tehran.

Kipindi cha juma hili, bado kinaendelea kujadili, kwa mujibu wa maandiko matakatifu ya Qur’ani Tukufu na Hadithi za Kiislamu, suala ambalo tumekuwa tukilijadili katika vipindi vitatu vilivyopita ambalo linahusiana na majukumu ya Umma wa Kiislamu kwa kizazi kitoharifu cha Mtume (saw). Katika vipindi vilivyopita tulinufaika na mwongozo wa Qur’ani na Sunna katika kufahamu majukumu hayo ambayo ni utiifu mutlaki kwao, utiifu ambao unajumuisha kufuata sira na njia yao ya maisha katika shughuli zetu za kila siku maishani. Wajibu wa pili ni kuwarejea ili watuhukumu panapotokea hitilafu na mivutano miongoni mwetu ili wapate kutuhukumu na kuondoa hitilafu hizo kwa msingi wa mafundisho ya Qur’ani Tukufu na hukumu ya Mwenyezi Mungu.

Na wajibu wa tatu ni kuwapenda kwa dhati na kwa nyoyo zetu zote, mapenzi ambayo yanatulazimu kuwanusuru na kuwafuata kivitendo katika nyenendo zao zote. Hivyo, wajibu wa nne ni upi?

Endeleeni kuwa nasi wapenzi wasikilizaji hadi mwisho wa kipindi ili tupate kunufaika na jibu la swali hili muhimu kuhusiana na wajibu wa nne tunaoapasa kuutekeleza kuhusiana na Maimamu wetu watukufu (as). Tutaanza kwa kuzingatia maandiko matakatifu yafuatayo, karibuni.

 

Ndugu wasikilizaji, pamde zote mbili za Shia na Suni zimenukuu hadithi za kuaminika kutoka kwa Bwana Mtume (saw) zinazosisitiza wazi kwamba swala ambayo Waislamu wameamrishwa kumswalia Mtume katika Qur’ani Tukufu haikamiliki ila kwa kujumuishwa Aali zake kwenye swala hiyo. Swala isiyojumuisha Aali hao bila shaka huhesabiwa kuwa ni swala iliyokatika na kutokamilika na hivyo haimridhishi Mwenyezi Mungu wala Mtume wake (saw). Kwa maelezo hayo tunafahamu wazi kwamba wajibu wa nne tulionao kwa Maimamu watoharifu wa Mtume ni kuwaswalia pamoja na bwana wao (saw). Hilo hutimia kupitia hadithi nyingi zilizonukuliwa na kutafitiwa na maulama kwamba Aali za Mtume Muhammad ni kizazi chake kilichotakaswa katika maasumeen ambao wote ni Ahlul Kisaa na tisa katika kizazi cha Imam Hussein (as). Na hadithi sahihi kutoka pande zote mbili kwamba aya inayomrisha wajibu wa kumswalia Mtume Mtukufu (saw) ilipoteremka, Mtume aliulizwa namna ya kuswaliwa naye akatoa jibu kamili namna Waislamu wanavyopaswa kumswali ambapo aliwajumuisha Aali zake watoharifu kwenye swala hiyo. Tutatosheka hapa kwa kutaja hadithi iliyonukuliwa na Bukhari katika juzu ya sita ya Sahihi yake ambapo amemnukuu Ka’b bin Ajra akisema: ‘Palisemwa: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ama kuhusu kukuswalia tumeelewa, lakini swala hii ni vipi? Akajibu: Semeni Allahumma, Mswalie Muhammad na Aali za Muhammad kama ulivyomswalia Ibrahim na Aali za Ibrahim, hakika Wewe ni Muhimidiwa, Mtukufu.’

Madhumuni hii ya hadithi imepokelewa kutoka kwa Abu Said al-Khudari kama alivyonukuu katika Musnadi wake Ahmad bin Hambal kauli ya Mtume (saw) katika hadithi ya Ahlu Kisaa inayosema: ‘Allahumma hakika wao ni katika mimi na mimi ni katika wao, hivyo basi jaalia swala, rehema, maghfira na ridhaa yako iwe juu yake na juu yao.’ Katika hadithi hii kuna sisitizo jingine linalobana maana ya neno ‘Aal’ kwa watu maalumu ambao wametakaswa na ambao wanakusudiwa na aya ya Tat’hir na sio kizazi kizima cha Mtume Mtukufu (saw).

 

Na sisitizo hili linapata nguvu zaidi tunapozingatia hadithi nyingi tukufu ambazo zimenukuliwa na maulama wengi wa Kisuni zinazokemea na kukataza kumswalia Mtume (saw) swala iliyokatika. Ibn Hajar amenukuu baadhi ya hadithi hizi katika kitabu chake cha Swawaiq al-Muhriqa ikiwa ni pamoja na hii inayosema: ‘Msiniswalie swala iliyokatika. Wakasema: Je, swala iliyokatika ni ipi? Akasema: Mnaposema, Allahumma! Mswalie Muhammad na kisha mkanyamaza, bali semeni: Allahumma! Mswalie Muhammad na Aali za Muhammad.’

Ibn Hajar vilevile amesema: ‘Ad-Dar Qutni na al-Beihaqi wamenukuu hadithi inayosema: Mtu anayeswali swala na kutoniswalia wala kuwaswalia Watu wa Nyumba yangu kwenye swala hiyo, swala yake haikubaliki.’ Kisha Ibn Hajar akasema: ‘Na hadithi hii ndiyo aliyoitegemea as-Shafii (MA) katika kauli yake kwamba kuwaswalia Aali wa Mtume ni katika wajibu wa swala kama ilivyo katika kumswali Mtume mwenyewe (saw). Na Imamu wa wafasiri wa Kisuni, Fakhr ar-Razi anasema katika juzuu ya 27 ya tafsiri yake al-Kabir: ‘Hakika dua kwa Aal ni cheo adhimu na ndio maana dua hiyo ikajaaliwa kuwa mwishoni mwa Tashahhud kwenye swala na katika kauli yake (saw): Allahumma! Mswalie Muhammad na Aali za Muhammad, na mrehemu Muhammad na Aali za Muhammad. Na hii ni taadhima ambayo haipatikani kwa wasiokuwa Aal. Hivyo basi haya yote yana maana kwamba kuwapenda Aali wa Muhammad ni wajibu.’ Na al-Fakhr ar-Razi amenukuwali na baadhi ya maulamaa wa Ahlu Suna akisema kama ilivyonukuliwa katika vitabu vya Nur al-Abswar na katika juzuu za 18 na 33 za kitabu cha Sharh Ihqaaq al-Haq: ‘Ahlu Beit wake, yaani wa Mtume (saw), ni wale waliokuwa sawa naye katika vitu vitano: Katika kumswalia yeye na wao kwenye Tashahhud, katika kuwatumia swala, utakaso, katika kuharamishiwa sadaka na katika kuwapenda.’

 

Jambo tunalojifunza kutokana na maandiko matakatifu ni kuwa amri ya kuwaswalia Aali wa Mtume kila mara linapotajwa jina la Bwana wao huyo (saw) ni ya moja kwa moja na isiyoshurutishwa na jambo jingine lolote. Hili linatokana na katazo la Mtume huyo kuswaliwa swala iliyokatika na isiyokamilika na kuwajibishwa swala hiyo kwenye Tashahhud ya swala za kila siku. Na hadithi za pande zote mbili za Suni na Shia zimetaja na kufafanua baraka nyingi zinazopatikana katika kumswalia Mtume na Ahlu Beit wake (as). Hii ni kwa sababu swala hiyo ndio ufunguo wa kujibiwa dua, njia ya kusamehewa dhambi na ngazi ya kumkurubia Mwenyezi Mungu na hivyo kufanikiwa kunufaika na upendo wake Subhanahu Wataala na baraka nyingine nyingi.

Na swala za kuvutia zaidi ni zile ambazo zimetajwa kwenye vitabu vyetu vya kuaminika kama vile Mis’bah al-Mutahajjid cha Sheikh Tusi na Jamal al-Usbuu’ cha Ibn Tawus akimnukuu Imam Mtukufu al-Hassan al-Askari (as), swala ambazo alimfundisha Abu Muhammad Abdullah bin Muhammad al-Abid (MA). Kitabu hiki kimegawanywa katika faslu kumi na tatu ambapo kila faslu imetengewa kila maasumu wa Nyumba ya Mtume (saw) isipokuwa Imam Hassan na Hussein (as) ambao wamejumuishwa kwenye faslu moja.

Swala hizi za kuvutia zimenukuliwa na Sheikh Abbas ak-Qumi mwishoni mwa kitabu chake mashuhuri cha Mafatih al-Jinan chini ya anwani, as-Swalawaat ala al-Hujaj at-Twahirin.

************

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi cha wiki hii cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain  ambacho kama kawaida kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kuwa mmenufaika vya kutosha na yale mliyoyasikia kwenye kipindi hiki. Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.