Feb 27, 2017 07:23 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Februari 27

Tutakupasha kuhusu fainali ya Kombe la Roll Ball; Kisa cha Simba kummeza Yanga; Na Man U yatwaa Kombe la EPL na kuwa klabu yenye ufanisi zaidi Uingereza, mahala pale Liverpool.......

Roll Ball: Iran yaibuka ya 2 Kombe la Dunia

Timu za taifa za mchezo wa Rolasketi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa upande wa wanaume na wanawake zimeibuka katika nafasi ya pili kwenye mashindano ya Kombe la Dunia ya Roll Ball mwaka huu 2017 huko Bangladesh. Hii ni bada ya timu mbili hizo kushindwa kutamba mbele ya timu za taifa za India katika michezo ya fainali mjini Dhaka siku ya Jumatano. Timu ya wanaume ya India iliishinda Iran kwa magoli 8-7, huu ukiwa ni ushindi wa nne mfululizo kwa timu hiyo katika mashindano hayo ya kimataifa. Kwa upande wa akina dada, timu ya taifa ya India ya Rolasketi iliibamiza Iran mabao 6-4, hili likiwa ni taji la pili kutwaliwa na timu hiyo. Timu ya Roll Ball ya Iran ya wanaume ilianza vyema mashindano hayo ya Kombe la Dunia ya Rollball mwaka huu 2017, baada ya kuizamisha Tanzania pointi 7-2 katika mchuano wa pili wiki jana. Kabla ya hapo, vijana wa Kiirani waliwasagasaga Mafarao wa Misri alama 11-0. Mashindano ya kuwania Kombe la Rolasketi/Roll Ball hufanyika baada ya miaka miwili, tangu mwaka 2011. Katika duru zote, India imeibuka kidedea huku Iran ikishika nafasi ya pili. Hata hivyo Kenya ilitwaa taji hilo katika duru ya mwaka 2015, kwa upande wa wanawake. Timu hiyo ya Kenya ilikuwa na wingi wa matumaini ya kunyakua japo taji moja katika mashindano ya mwaka huu, kama walivyosema wachezaji na kocha wao muda mfupi kabla ya kuondoka nchini. Hata hivyo waliambulia nafasi ya nne katika mashindano hayo yaliyopigwa katika mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka.

Simba yaitafuna Yanga

Mchuano wa watani wa jadi wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara uliokua ukisubiriwa kwa hamu na shauku kuu ulipigwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam, ambapo Simba alifanikiwa kumtafuna na kummeza mzima mzima hasimu wake Yanga. Katika kipute hicho kilichoshuhudiwa na mamia ya maelfu ya mashabiki, klabu ya Simba iliititiga Young Africans Yanga mabao 2-1, huu ukiwa ni mchuano wa marudiano. Mechi hii imekata mzizi wa fitina na uhasama ulioanza Oktoba Mosi mwaka jana 2016 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara kati ya Yanga na Simba; ambao uliishia kwa sare ya 1-1. Katika mchezo wa Jumamosi, Yanga ndio walikuwa wa kwanza kupata goli kunako dakika ya 4 lililojazwa wavuni na kiungo Simon Msuva kwa mkwaju wa penati. Hii ni baada ya Obrey Chirwa kuchezewa visivyo katika sanduku la hatari.

Kiungo wa Simba akivaana na wa Yanga

Na kwa kuwa kutangulia sio kufika, na pia usimuone simba kanyeshewa ukadhani ni paka, vijana wa klabu ya Simba walijipapatua na kunguruma uwanjani. Kiungo Laudit Mavugo aliipa Simba bao la kwanza la kusawazisha mambo katika dakika ya 66 huku mtoka benchi Shiza Kichuya akipiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Yanga kwa bao la pili na la ushindi.

Yanga wanasalia na point zao 49 wakiwa wamecheza mechi 22 ingawaje wana mchuano mmoja wa kiporo. Simba ambao wanaongoza ligi kwa sasa wamecheza jumla ya michezo 23 ya Ligi Kuu ya Tanzania inayodhaminiwa na Vodacom, na wamesalia na mechi saba tu kabla ya ligi kuisha. Miongoni mwa wanasasiasa, viongozi na shakhsia walioshuhudia mechi hiyo ya Jumamosi ni pamoja na Waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa, Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete, Kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam Simon Sirro na Mbunge na mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, kila mmoja akishabikia timu yake.

Man U yatwaa Kombe la EFL

Mashetani Wekundu wa Old Trafford wametwaa Kombe la EFL baada ya kuichachawiza Southampton mabao 3-2 katika mchuano wa aina yake siku ya Jumapili. Katika mchezo huo wa kukata na shoka uwanjani Wimbley, kiungo mahiri wa Manchester United Zlatan Ibrahimovic alionekana kuwa nyota wa mechi kwa kufanikiwa kucheka na nyavu mara mbili, bao la kwanza na la ushindi. Bao la pili la Mau U lilitiwa kimyani na Jesse Lingard kunako dakika ya 39.

Pogba

 

Ibrahimovic alifunga bao la kwanza katika dakika ya 19 na la mwisho na la ushindi katika dakika za lala salama. Mabao mawili ya kiungo wa Southampton Manolo Gabbiadini hayakutosha kuifanya klabu hiyo itambe mbele ya Mashetani Wekundu. Mchezaji huyo aliyafunga magoli hayo dakika chache kabla ya mapumziko, na dakika chache baada ya kupulizwa kipenga cha kuanza mchezo baada ya kutoka mapumzikoni. Wanasema wenye kusema mgala muue na haki yake mpe, ukweli wa mambo ni kuwa, Southampton waliutawala mchezo huo kwa asilimia 52 na Man U 48, ingawaje utamu wa mchezo ni wingi wa mabao. Hili ni taji kuu la 42 kutwaliwa na Man U katika historia ya soka nchini Uingereza. 

Dondoo; Leicester yamtimua mkufunzi, Rooney habanduki Man U

Hisia mbali mbali zinaendelea kutolewa baada ya bingwa mtetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza, Leicester City kumtimua mkufunzi wake raia wa Italia Claudio Ranieri, ikiwa ni miezi tisa baada ya kuiwezesha kupata ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Uingereza almaarufu EPL. Leicester iko katika nafasi ya 17 kwa sasa na ikipoteza alama moja tu itakuwa kwenye hatari ya kushushwa daraja. Msimu uliopita, klabu hiyo ilitwaa ubingwa kwa zaidi ya alama 10 mbele, lakini msimu huu, mpaka sasa wamecheza michezo 25 ya ligi na kushinda mitano pekee, na imesalia michezo 13 ligi kuisha. Baadhi ya wadau katika ulimwengu wa soka akiwemo kocha wa Man U wameikashifu hatua ya kutimuliwa Ranieri, baadhi wakipongeza wakisema kuwa klabu hiyo inahitaji busara mpya. Binafsi kocha huyo anasema shoka hilo limesambaratisha ndoto zake za kuendelea kuinoa klabu aliyoienzi ya Leicerster. Huku hayo yakirifiwa, nahodha wa Uingereza Wayne Rooney anasema kuwa atasalia katika klabu ya Manchester United baada ya kuhusishwa na uhamisho wa China. Rooney mwenye umri wa miaka 31 amesema anatumai kwamba atashirikishwa kamili katika mechi zilizosalia za klabu hiyo msimu huu. Mkufunzi wa Man U, Jose Mourinho amekataa amekataa kuzungumzia tetesi kuwa Rooney huenda akaondoka klabu hiyo mwezi huu. Ifahamike kuwa, dirisha la uhamisho nchini China linafungwa Februari 28. Ajenti wa Rooney, Paul Stretford, hivi karibuni alisafiri China kuona iwapo atafanikiwa kupata makubaliano, ingwaje haijulikani alizungumza na klabu gani.

……………………………..TAMATI………..………………

 

 

Tags