Mar 03, 2017 00:50 UTC
  • Ijumaa, 3 Machi 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 4 Jamadithani 1438 Hijria sawa na Machi 3, 2017.

Miaka 15 iliyopita katika siku kama ya leo Wahindu wenye misimamo mikali walifanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu wa katika jimbo la Gujarat nchini India. Serikali ya India ilitangaza kuwa Waislamu 790 waliuawa kwa umati katika mauaji mauaji hayo lakini vyombo vingine vya kujitegemea vilisema kuwa, idadi ya Waislamu waliouawa ni zaidi ya 2000. Kisingizio kilichotumiwa na Wahindu kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waislamu wa Gujarat hususan katika mji wa Ahmadabad ni moto uliotokea katika gari moshi iliyokuwa imebeba Wahindu lakini baadaye ilibainika kuwa, Waislamu hawakuhusika kwa njia yoyote na tukio hilo. Katika mauaji hayo polisi na maafisa wa jimbo la Gujarat walishirikiana na Wahindu katika mauaji dhidi ya Waislamu.

Waislamu wa India

Miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo ilifanyika kura ya maoni kwa ajili ya uhuru na kujitawala Jamhuri ya Bosnia Herzegovina. Kura hiyo ya maoni iliungwa mkono na karibu asilimia 100 ya wananchi walioshiriki katika zoezi hilo na kupelekea nchi hiyo kujitenga na Yugoslavia, baada ya Slovenia na Croatia kufanya hivyo. Jamhuri ya Bosnia Herzegovina ina ukubwa na kilomita mraba karibu 51,129 na inapakana na Croatia kwa upande wa kaskazini na magharibi, Serbia upande wa mashariki na Jamhuri ya Montenegro upande wa kusini mashariki. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka 1991, asilimia 44 ya jamii ya nchi hiyo ilikuwa ni Waislamu, jamii ambayo inaunda kundi kubwa zaidi la kidini katika jamhuri hiyo ya eneo la Balkan. 

Bendera ya Jamhuri ya Bosnia

Tarehe 4 Jumadi Thani miaka 63 iliyopita Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi akiwa pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini. Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.

Navvab Safavi

Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita, utawala wa Othmaniya na Russia zilisaini mkataba katika eneo lilopewa jina la mkataba huo yaani San Stefano. Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya utawala wa Othmaniya kushindwa na Urusi katika vita. Urusi iliuvamia utawala huo kutokana na uchu wake wa kutaka kuzidhibiti ardhi zilizokuwa chini ya himaya ya Othmaniya katika eneo la Balkan.

Na miaka 314 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Robert Hooke, mwanasayansi wa Uingereza. Hooke alizaliwa mwaka 1635 huko kusini mwa nchi hiyo. Alifanya utafiti mbalimbali katika sayansi ya fizikia, na kutoa mchango mkubwa katika mapinduzi ya sayansi kupitia kazi zake za majaribio na nadharia. Hooke kwa mara ya kwanza aliweza kutumia darubini yake na kutazama chembe ndogo kabisa ya kiumbe hai na kuipa jina la seli.  Mwanasayansi huyo wa Uingereza pia alivumbua vifaa kadhaa katika taaluma ya hali ya hewa.

Robert Hooke