Mar 06, 2017 05:58 UTC
  • Jumatatu, 6 Machi, 2017

Leo ni Jumatatu, tarehe 7 Jamadithani 1438 Hijria sawa na 6 Machi, 2017

Miaka 913 iliyopita katika siku kama ya leo, arifu mkubwa wa Kiislamu Ainul Qudhaat Hamedani mwenye lakabu ya Abul Fadhl, aliuawa shahidi kwa kunyongwa huko Hamedan. Alikuwa fakihi, mwanafasihi, msomi na malenga mahiri. Ainul Qudhaat alizaliwa mwaka 492 Hijria. Msomi huyo katu hakuwa akiogopa kubainisha itikadi yake. Ni kutokana na misimamo yake hiyo thabiti ambapo mwaka 525 Hijria alitiwa mbaroni na kufungwa huko Baghdad. Baada ya muda alihamishiwa Hamedan nchini Iran na kunyongwa kando na shule yake. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni al Tamhiidat na Haqaiqul Qur’an.

Ayatullah Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin Aamili

Siku kama ya leo miaka 542 iliyopita, alizaliwa mjini Caprese Michelangelo, mchoraji na mhunzi wa masanamu wa Italia. Licha ya upinzani mkubwa wa baba yake dhidi ya sanaa hiyo ya uhunzi na uchoraji, Michelangelo alijiendeleza katika taaluma hiyo na kupata umahiri mkubwa. Uhodari wake ulionekana miaka michache baadaye ambapo alifanikiwa kuchonga masanamu mengi ya kuvutia. Michelangelo, alitokea kuwa mhunzi hodari wa karne ya 16 Miladia. Mwaka 1505, wakazi wa mji wa Roma walimwalika Michelangelo, ili aende kuwachongea sanamu la papa kwenye kaburi lake. Baadaye papa wa wakati huo, alimtaka mtaalamu huyo kupamba paa la kanisa la Sistine, kazi iliyoanza hapo mwaka 1508 na kumalizika mwaka 1512. Mbali na hayo, Michelangelo alichonga sanamu kubwa la Nabii Issa (as), ambalo lipo mjini Roma hadi leo.

Michelangelo

Siku kama ya leo maka 117 iliyopita alifariki dunia mvumbuzi wa pikipiki raia wa Ujerumani Gottlieb Daimler akiwa na umri wa miaka 64. Daimler alizaliwa mwaka 1834 na kazi yake ya mwanzo ilikuwa utengenezaji bunduki. Tangu akiwa kijana mvumbuzi huyo alivutiwa sana na kazi za viwandani na alifanya utafiti mkubwa katika uwanja huo hadi alipofanikiwa kutengeneza pikipiki. Gottlieb Daimler pia alikuwa miongoni mwa watu walioweka misingi ya utengenezaji wa magari madogo na hata mabasi.

Gottlieb Daimler

Siku kama ya leo, miaka 80 iliyopita, alizaliwa, Valentina Tereshkova, mwanamke wa kwanza mwanaanga wa dunia. Akiwa kijana na baada ya kushiriki katika mashindano ya kuruka kwa mwavuli, Tereshkova aliibuka mshindi na hivyo kufikia daraja la ukapteni katika kikosi cha anga cha jeshi la Urusi ya zamani. Ni baada ya hapo ndipo akajifunza urubani wa ndege. Hatimaye tarehe 16 mwezi Juni, mwaka 1963 na akiwa na umri wa miaka 22, aliweka rekodi ya dunia kwa kuwa mwanamke wa kwanza mwanaanga, baada ya kuanza safari ya mwezini na chombo cha Vostok 6.

Valentina Tereshkova

Tarehe 7 Jamadithani 78 iliyopita yaani tarehe 19 Jamadut-Thani mwaka 1360 Hijria, aliaga dunia Ayatullah Abu Abdullah Zanjani mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Alimu huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 51 na kuzikwa mahala alipozaliwa yaani Zanjan kaskazini magharibi mwa Iran. Alijifunza elimu za fasihi, falsafa na itikadi akiwa kijana mdogo. Baadaye Ayatullah Zanjani alielekea Najaf Iraq kwa shabaha ya kujiendeleza zaidi kielimu. Historia ya Qur'ani, Historia ya Maisha ya Mtume Muhammad SAW na Adhama ya Hussein bin Ali ni baadhi tu ya vitabu vya Ayatullah Zanjani vyenye thamani kubwa.

Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, aliuawa Ali Razmara, Waziri Mkuu wa Iran aliyekuwa kibaraka wa Uingereza. Razmara aliyekuwa jenerali wa jeshi katika utawala wa kifalme aliuawa na mwanamapinduzi wa Kiislamu aliyejulikana kwa jina la Khalil Tahmasbi. Usaliti na uovu wa wazi wa Ali Razmara katika siasa za kuiongoza nchi, ulizusha upinzani mkubwa wa wananchi dhidi ya Waziri Mkuu huyo na kutayarisha mazingira ya kuangamizwa kwake.

Ali Razmara

Tarehe 6 Machi miaka 60 iliyopita, nchi ya Ghana ilifanikiwa kupata uhuru chini ya uongozi wa Dakta Kwame Nkurumah. Ghana ilitumbukia katika makucha ya mkoloni wa Kireno kuanzia karne ya 15. Baada ya Wareno, Waingereza waliidhibiti na kuikoloni nchi hiyo iliyokuwa mashuhuri kwa jina la "Pwani ya Dhahabu" kutokana na utajiri wake mkubwa wa madini hayo.