Mar 07, 2016 12:19 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (34)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji ni wasaa mwingine wa kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

 Katika vipindi kadhaa vilivyopita vya mfululizo huu sanjari na kubainisha hadithi zinazohusiana na kutatua shida za watu na kutoa misdaqi na baadhi ya mifano katika hilo, tulifahamu kwamba, kama watu watasaidiana na kila mmoja kuguswa na shida na mushkili wa mwenzake na watu katika jamii wakaitambua ghamu na huzuni ya wengine kwamba, ni yao, basi utulivu na udugu vitatawala katika jamii. Na kinyume chake, endapo watu katika jamii watahisi kwamba, kila mtu anapaswa kujihusisha na mambo yake tu na hakuna haja ya kusaidiana, basi kivuli cha kukata tamaa kitatawala katika jamii hiyo. Wapenzi wasikilizaji katika sehemu hii ya 34 ya Hadithi ya Uongofu juma hili tutazungumzia baadhi ya sababu zinazopelekea kutowasaidia watu wengine. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nami hadi mwishowa kipindi hiki. Karibuni. 

******

Moja ya sababu za ndani ambazo ni chimbuko na kikwazo cha mtu kumsaidia mwenzake mwenye shida ni ubahili. Ubahili au unyimivu ni sifa ambayo humzuia mtu kutumia mali na utajiri katika njia sahihi na hivyo kumnyima fursa ya kuwa mkarimu. Mtu ambaye ni bahili sio tu kwamba, huwa hayuko tayari kutoa na kuwasaidia watu, bali huwakataza watu wengine pia kufanya hivyo. Ubahili kinyume chake ni ukarimu, wema, hisani na moyo wa kusaidia. Endapo mtu atatoa na kutumia mali na utajiri alionao katika njia inayofaa na stahiki, basi mtu huyo hutambulika kuwa ni mkarimu na mwenye moyo wa kutoa. Lakini kama mtu atajizuia kutoa mali na fedha zake, akafanya unyimivu na kutozitumia katika njia inayostahiki huwa bahili, mchoyo na mnyimivu.

Imam Swadiq (a.s) anasema kuhusiana na mabahili kwamba:

“Bahili hafanyi ubahili na unyimivu kwa kile alichonacho tu, bali hata kwa kile ambacho kiko mikononi mwa watu wengine; ubahili huo huendelea hadi kufikia hatua ya bahili kutamani kupata kila ambacho kiko mikononi mwa watu wengine, iwe ni kwa njia ya halali au ya haramu, na katu hakinaiki na kile ambacho Mwenyezi Mungu amemruzuku.”

Kwa hakika ni jambo la kawaida kwamba, kutawala sifa ya ubahili miongoni mwa watu hupelekea masikini na wahitaji kusahauliwa na wakati huo huo, huba, hurumana mapenzi ambayo huwafikia wenye shida na wahitaji kupitia kwa wengine hukatika na kutoweka. Hali hii huongezeka siku baada ya siku na kupelekea kushadidi pengo na tofauti kati ya masikini na tajiri. Katika mazingira kama haya jamii hukumbwa na mgogoro na matatizo mengi. Katika vitabu vya Kiislamu kuna hadithi nyingi zinazozungumzia ubahili. Baadhi ya hadithi hizo zinabainisha kwamba, ubahili ni wenzo ambao humfanya kila mwenye sifa hii kuelekea katika kila baya. Moja ya hadithi hizo ni ile inaeleza kwamba: “Kufanya ubahili na unyimivu kwa kile ulichonacho ni kuwa na dhana mbaya kwa Mwenyezi Mungu.”

Hii ni kutokana na kuwa, shetani ndiye ambaye huwatisha watu na ufakiri na umasikini, lakini Mwenyezi Mungu huwaahidi waja wake fadhila na maghufira. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 39 ya Sura ya 34 kwamba:

“Sema: Kwa hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki na humdhikisha amtakaye katika waja wake. Na chochote mtakachokitoa Yeye atakilipa. Naye ni Mbora wa wanaoruzuku.”

*******

Uvivu ni kikwazo kingine cha kutatua shida za watu na kuwakidhia hawaiji wahitaji. Jambo hili lina madhara makubwa. Uvivu unahesabiwa kuwa, hupelekea kuporomoka dini na dunia ya mtu. Uvivu hupelekea kupatikana uzembe katika kutekeleza mambo ya wajibu, hupoteza haki za wengine na kumfanya mtu mwenye sifa hii mbaya kutofanya hima kwa ajili ya kuwasaidia wenye shida na kutatua hawaiji zao. Imekuja katika hadithi kwamba, Imam Ja’afar Swadiq (a.s) alikuwa akimuusia mwanawe kwa kumwambia: “Jiepushe na uvivu na kutokuwa na raghba ya kufanya mambo; kwani mambo haya mawili humzuia mtu kunufaika na dunia na akhera.

Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) anasema kuwa: “Jitengeni na uvivu kwani kila mwenye kufanya uvivu hawezi kutekeleza haki ya Mwenyezi Mungu.”

Katika upande mwingine ni kuwa, thamani ya kila mwanadamu ni kulingana na hima na jitihada zake. Mtu mwenye hima kubwa daima huwa na malengo ya kufanya mambo makubwa zaidi.

Mtu kama huyu huwa hafurahi kutokana na kupata mambo na manufaa ya kidunia, bali daima hufikiria kupata radhi za Mwenyezi Mungu na rehma Zake kupitia njia ya kuwasaidia watu wengine. Labda ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) akasema kuwa: “Utoaji na ukarimu wa mtu ni ishara ya hima ya juu aliyonayo mtu huyo.”

Moja ya ujazi na neema za Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu ni kuona haya na soni; na hali ya kuona haya ni kizuizi muhimu cha ndani ya nafsi kinachomzuia mtu kufanya mambo mabaya na machafu. Je daima haya na soni ni jambo zuri na lenye kupendeza?

Katika mafundisho ya kiakhlaqi na maadili ya maktaba ya Ahlul Bayt (a.s) neema ya soni na haya imegawanywa katika sehemu mbili yaani soni na haya nzuri na mbaya. Haya au soni nzuri ni ishara ya akili na elimu, ilhali haya mbaya na isiyokubaliwa ni ishara ya ujinga na ujahili. Kuona soni au aibu kusema neno la haki katika sehemu na mazingira ambayo haki inapaswa kusemwa na kubainishwa na kuona aibu na soni kutoa sadaka kidogo kutokana na kukabiliwa na ukata ni mifano miwili ya haya na soni mbaya.

Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) anasema kuwa: “Fanyeni jambo la kheri na msikihesabu mnachokifanya kwamba, ni kidogo…kisha anasema: Msione haya hata kidogo kutoa na kufanya ukarimu kwani kunyimwa hilo ndiko kusiko na thamani zaidi.

Kwa msingi huo basi, kuona haya kusema haki katika nafasi ya kutoa nasaha na ushauri, kuona aibu kuwasaidia watu wengine mbele za watu, kuona soni kuwa mpatanishi katika mambo ya watu na kuona haya katika kuamrisha jema na kukataza ovu, ni mambo yasiyopendeza na yasiyokubalika.

Hii ni kutokana na kuwa, hatua hiyo huzuia kutekeleza jukumu la kidini la mtu na kufunga njia ya kufikia athari na baraka za dunia na akhera.

*******

Kusahau kifo na kwamba, kuna Siku ya Kiyama ni kikwazo kingine katika njia ya kusaidia watu na kutatua shida na hawaiji zao. Kuamini kwamba, kuna Siku ya Kiyama na kwamba, siku hiyo kila mtu atahesabiwa amali zake ni jambo muhimu lilalomzuia mtu kutenda dhambi na kufanya matendo mabaya na machafu. Aidha imani hiyo huwa ni msukumo muhimu kwa ajili ya kufanya mambo mema na matendo mazuri na wakati huo huo kufanya mambo ya kheri na kutatua shida za watu.

Imam Ja’afar Swadiq (a.s) anasema: Kukumbuka kifo huuwa matakwa ya nafsi, hung’oa mizizi ya mghafala, huupa nguvu moyo kwa ahadi za Mwenyezi Mungu, huporomosha bendera za hawaa na matamanio, huzima moto wa tamaa na huiona dunia kuwa ni ndogo.”

Kwa msingi huo basi, kukumbuka kifo na mauti huondoa mghafala katika nyoyo na pindi nyoyo zinapolainika, uja kwa Mwenyezi Mungu na kutenda mambo mema huwa jambo jepesi kwa watu.

Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa, jiungeni nami tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.