Mar 07, 2016 12:22 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (35)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji wa kujiunga nami tena katika kipindi kingine cha Hadithi ya Uongofu. Juma lililopita kipindi chetu kilizungumzia baadhi ya sababu zinawafanya watu licha ya kuwa na uwezo huamua kujizuia na kutowasaidia wenzao wenye kuhitaji msaada iwe wa kimaada au kimaanawi.

Katika sehemu hii ya 35 ya mfululizo huu tutazungumzia maudhui ya kujighafilisha na kupuuza mapungufu anayoyashuhudia mtu baina ya watu anaoishi nao. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki kwa juma hili. 

********

Mwanadamu akiwa mmoja wa wanachama katika jamii huwa na mdakhala na mawasiliano na watu mbalimbali katika jamii anayoishi. Endapo mwanadamu huyu ataamua kutazama kwa umakini wa hali ya juu kila amali inayofanywa na watu wengine katika jamii hiyo bila shaka ataona na kushuhudia aibu na mapungufu mengi. Kuzingatia aibu na mapungufu ya watu wengine na kuyatilia maanani kupita kiasi hupelekea kuingia dosari mahusiano baina ya wanajamii. Hii ni katika hali ambayo kufumbia macho, kutotilia maanani na kujighafilisha na mapungufu anayoyaona mtu kwa watu wengine huyafanya machungu kuwa matamu na huondoa hali ya msongo wa mawazo na wasiwasi. Uislamu umelizingatia na kulipa umuhimu maalumu suala la kujighafilisha na kupuuza baadhi ya mapungufu ya watu katika jamii na umelitaja suala hilo kuwa moja ya sifa za nzuri za waumini. Kujighafilisha maana yake ni mtu kushuhudia kosa la mtu katika jamii na licha ya kujua na kufahamu hilo, lakini kutokana na maslahi hupuuza hilo na kujighafilisha nalo na kuonesha kana kwamba, hajui chochote kuhusiana na kosa la ndugu yake huyo, kiasi kwamba, hata mhusika hudhani na kutasawari kwamba, mwenzake huyo hana habari kuhusiana na kosa lake hilo. Thamani ya kitendo na amali hii ya kiakhlaqi ina umuhimu mno kiasi kwamba, kuna hadithi nzuri zimenukuliwa kuhusiana na maudhui hii. Amir al-Muuminina Ali bin Abi Twalib (a.s) amenukuliwa akisema kuhusiana na jambo hili kwamba: “Inua kiwango cha thamani na daraja yako kwa kujighafilisha na kufumbia macho mambo madogo ya watu na yasiyo na maana….na usifanye upekuzi katika mambo yaliyojificha na yaliyofunikwa….na thibitisha hadhi na adhama yako kwa kutozingatia kupita kiasi undani wa mambo.”

Akthari ya watu katika kipindi cha maisha yao hapa duniani hutokea kufanya makosa madogo au makubwa kwa kusahau au kwa makusudi. Si hekima hata kidogo na ni jambo lisilopendeza kutoa hukumu kuhusiana na makosa haya ambayo hayajafikia hatua ya dhambi kubwa. Katika mazingira kama haya, kujighafilisha na kufumbia macho na kujifanya kutokuwa na habari kuhusiana na makosa kama haya, ni jambo ambalo lina thamani zaidi kuliko kusamehe. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 22 ya Surat an-Nur kwamba:

“Na wasamehe, na waachilie mbali. Je! Nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.”

********

Kuna hadithi nyingi zilizopokewa kutoka kwa viongozi wema zinazobainisha umuhimu na thamani ya kujighafilisha na kufumbia macho pamoja na kujifanya kutokuwa na habari kuhusiana na makosa ya watu katika jamii. Imam Ali bin Hussein Zayn al-Abidiin (a.s) amenukuliwa katika hadithi mashuhuri akisema kwamba:

“Maslahi ya kuishi pamoja, mdakhala na maingiliano salama na watu yamo katika chombo ambacho theluthi mbili yake ni welewa na kuwa macho na theluthi moja yake ni kujighafilisha.”

Kwa hakika hadithi hii awali inasisitiza juu ya kuwa macho na kuwa na mwamko na kuacha kughafilika na unaitaja hisa ya jambo hilo kuwa ni theluthi mbili. Maana na mafuhumu ya hilo ni kwamba, mwanadamu hapaswi kujighafilisha na mambo muhimu na yenye kuainisha mustakbali wa kitu, bali anapaswa kulichunga hilo kwa umakini wa hali ya juu hasa katika mambo ambayo yana kheri na maslahi ndani yake. Kwa msingi huo basi, kujighafilisha kunakosifiwa na kupongezwa katika mafundisho ya dini na ambako mawalii wa Mwenyezi Mungu na viongozi wa Uislamu wanawashajiisha wafuasi wao washikamane nako ni kujighafilisha ambako chimbuko lake ni akili na maslahi na ambako kunakwenda sambamba na akhaqi na sifa njema.

Hata hivyo nukta ya kuzingatia hapa ni hii kwamba, kujighafilisha kulikoamrishwa na dini kunahusiana na mambo madogo madogo na yasiyo na thamani au aibu na mapungufu ambayo ni maslahi kutofahamika mambo hayo na jambo hilo lisiwe linakinzana na kuamrishana mema na kukatazana mabaya au kujighafilisha huko kusiwe kunakinzana na ukosojia sahihi, unaofaa na wa mahala pake. Hii ni kutokana na kuwa, kuamrishana mema na kukatazana mabaya kunahusiana na mambo ya wajibu na yaliyoharamishwa ambayo yanakiukwa na kukanyagwa waziwazi.

Kujighafilisha na kufumbia macho makosa madogo madogo ya watu ni moja ya mbinu za kimalezi katika Uislamu. Mbinu ya malezi ya kujighafilisha imesimama juu ya msingi wa izza na heshima. Kwa hakika uimara na udhaifu wa kila mtu una uhusiano na kuhisi izza na heshima.

*********

Bila shaka kumkosoa mtu na wakati mwingine kumuadhibu au hata kumpigisha faini mhusika kutokana na kuzembea katika jambo la kawaida na lisilo na umuhimu, huvunja haiba na heshima ya mkosoaji. Ili kujikinga na madhara kama haya ni lazima kujighafilisha na kujifanya kutokuwa na habari na makosa madogo ya mtu na ambayo hayana umuhimu. Imam Ja’afar Swadiq (a.s) anasema: Ifanye thamani na daraja yako kuwa kubwa kwa kujighafilisha. Yaani kujifanya kutokuwa na habari na mambo na makosa madogo wanayofanya watu wanaokuzunguka katika jamii unayoishi.

Kwa hakika mtu ambaye hatafumbia macho makosa na kuteleza kwa watu wengine, shakhsia na utukufu wake hukumbwa na kuchukiwa na kuvunjiwa heshima. Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) anasema kuhusiana na kujighafilisha ya kwamba: Mtu ambaye hajighafilishi katika mambo mengi, ameteteresha na kuvuruga utulivu wake.

Kwa hakika kujighafilisha na kupuuzilia mbali mapungufu na makosa madogo madogo ya watu ni tawi la subira, uvumilivu na kudhibiti ghadhabu. Mwanadamu anapswa kuwa na subira na uvumilivu mbele ya makosa ya watu wengine. Fadhila ya kiakhlaqi ya subira na ustahamilivu ni ishara ya akili na kutumia akili. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Amir al-Muuminina Ali bin Abi Twalib (a.s) anaitambua subira na uvumilivu kuwa dhihirisho la juu kabisa la kujighafilisha na kutoyazingatia makosa ya watu. Anasema: Hakuna subira kama kupuuzia mambo na hakuna hekima kama kujifanya kutojua jambo na kujifanya kutokuwa na habari."

Inanukuliwa kwamba, siku moja Imam Ali (a.s) alipita sehemu ambayo kulikuwa na maadui zake ambao mara baada ya kumuona wakaanza kutoa matusi na maneno mabaya. Imam Ali (a.s) aliwaapuza na kupita akilinda heshima yake kama inavyosema aya ya 72 ya Surat al-Furqan: "na pindi wapitapo penye upuuzi, hupita kwa hishima yao". Kisha Imamu Ali (a.s) aliwaambia watu aliokuwa amefuatana nao na ambao walikuwa wamechukizwa mno na kitendo hicho kwamba: Watu hawa hawanikusudii mimi."

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa juma hili umefikia tamati. Msisite kuwa nami tena wiki ijayo.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh