Jumapili, Machi 26, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 27 Jamadu th-Thani mwaka 1438 Hijria sawa na tarehe 26 Machi 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1322 iliyopita na kwa mujibu wa baadhi ya riwaya yaani sawa na tarehe 27 Jamadu th-Thani mwaka 116 Qamaria, alifariki dunia Ali Ibn Muhammad, mtoto wa Imamu Muhammad Baqir (as), imamu wa tano wa madhehebu ya Ahlu Bayti wa Mtume (as.) Mwaka 113 Hijiria Ali Ibn Muhammad alifanya safari nchini Iran kwa ajili ya kufanya tablighi ya dini ya Kiislamu na kujibu maswali yanayohusiana na dini hii. Baada ya kuwasili Iran alifikia katika mji wa Kashan ambapo aliishi huko kwa miaka mitatu na kujishughulisha na kazi ya kuwaongoza Waislamu. Kabla ya kufariki dunia baba yake Imamu Muhammad Baqir (as), Ali Ibn Muhammad, alikuwa akimtumia baba yake huyo aliyekuwa mjini Madina, habari za njama chafu za mtawala Hisham Bin Abdul-Malik dhidi yake na Waislamu wa Shia. Katika kipindi chote cha uhai wake nchini Iran alipata kuwa mashuhuri kwa uchaji-Mungu na ibada. Mwaka 116 Ali Ibn Muhammad, aliuawa shahidi na maadui wa Ahlu Baiti wa Mtume (saw) baada ya kujiri vita vikali vilivyopelekea wafuasi wake wanaokaribia 100 kuuawa. Alizikwa eneo ambalo linafahamikwa kwa jina la Mashhad-e Ardahal, mjini Kashan eneo ambalo ni karibu na mahala alipouawa shahidi. Eneo hilo hadi leo hutembelewa sana na Waislamu wafuasi wa Ahlu Baiti wa Mtume (as.)
Siku kama ya leo miaka 1047 iliyopita alifariki dunia Hussein Bin Ahmad Bin Hajjaj, malenga maarufu wa Kishia. Bin Hajjaj alikuwa mtaalamu wa fasihi aliyeishi katika karne ya nne Hijiria pamoja na Sayyid Murtadha na Sayydi Ridha, wasomi mashuhuri wa karne hiyo. Alifahamika sana kwa kusoma mashairi ya kuwasifu Ahlu Baiti wa Mtume (as) na kuwalaani maadui wao. Miongoni mwa athari za Hussein Bin Ahmad Bin Hajjaj ni kitabu chake chenye juzuu 10 ambacho hii leo kipo katika majumba tofauti ya makumbusho duniani. Alifariki dunia katika eneo lililo kati ya mji wa Kufa na Baghdad huku akizikwa karibu na kaburi la Imam Musa al-Kadhim, mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw), mjini Kadhimiya.
Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 57, Ludwig van Beethoven, mtunzi na muimbaji mashuhuri wa muziki wa nchini Ujerumani. Beethoven alizaliwa mjini Bonn mwaka 1770 Miladia. Akiwa kijana mdogo alikumbwa na matatizo mbalimbali lakini pamoja na hayo alienda kujifunza kwa wataalamu wakubwa wa fani hiyo wa zama zake kama vile Mozart na Joseph Haydn. Baadaye alikumbwa na tatizo la kutosikia huku akiwa kiziwi kabisa alipofikisha umri wa miaka 49. Ludwig van Beethoven anafahamika kwa kubuni Symphony namba tisa ambayo hii leo inatumika miongoni mwa Symphony zingine za muziki.
Siku kama hii ya leo miaka 106 iliyopita alizaliwa mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Marekani, Tennessee Williams. Alivutiwa sana na fasihi na mvuto huo ulikolea na kuimarika zaidi wakati alipokuwa masomoni katika chuo kikuu na hatimaye akafanikiwa kuwa mwandishi mkubwa. Tennessee Williams alitumia uhodari wake kueleza fikra zake kwa lugha ya michezo ya kuigiza. Kazi zake nyingi zilieleza hali ya watu wa tabaka la chini na wanaosumbuliwa na ukata katika jamii ya Marekani. Miongoni mwa kazi za mwandishi huyo mashuhuri ni pamoja na Cat on a Hot Tin Roof, Sweet Bird of Youth na The Glass Menagerie.
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, yalianza mapambano ya Mau-Mau yakiongozwa na Mzee Jomo Kenyatta, mwasisi wa nchi huru ya Kenya, dhidi ya wakoloni wa Kiingereza. Katika kipindi cha vita viwili vikubwa vya dunia, Kenya ilikumbwa na machafuko na vurugu nyingi. Hata hivyo baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wananchi wa nchi hiyo waliamua kupambana kufa na kupona ili kuikomboa nchi yao kutoka mikononi mwa wakoloni wa Ulaya. Wakoloni wa Kiingereza waliweka sheria kali katika maeneo tofauti ya Kenya hasa katika maeneo ya Wakikuyu lakini hilo halikuzuia kuasisiwa harakati ya Mau-Mau. Kaulimbiu kuu ya wapiganaji wa Mau-Mau ilikuwa ni kuweko usawa na uadilifu katika masuala ya kijamii na kisiasa baina ya wenyeji wa Kenya na Wazungu. Hatimaye harakati hiyo ya Mau-Mau kwa uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta ilifanikiwa kuikomboa Kenya kutoka mikononi mwa wakoloni wa Kiingereza mwanzoni mwa muongo wa 60.
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, yaani sawa na tarehe 26 Machi 1971, Pakistan Mashariki ambayo hivi sasa inajulikana kwa jina la Bangladeh iliamua kujitenga na taifa la Pakistan baada ya kuzuka mivutano mikubwa ya kisiasa na uasi nchini humo. Pakistan Mashariki na ile ya Magharibi ilikuwa nchi moja, ambapo pande hizo mbili ziliamua kujitenga mwaka 1947 kutoka taifa la India. Wabangladeshi waliokuwa wakiishi Pakistan Mashariki na kuunda jumla ya asilimia 98 ya watu wa eneo hilo, hawakuridhishwa na vitendo vya kibaguzi vilivyokuwa vikifanywa na serikali kuu huko Pakistan Magharibi.
Na siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, alifariki dunia dunia Ahmad Sekou Toure kiongozi wa nchi ya Kiafrika ya Guinea. Sekou Toure alizaliwa Januari 9 mwaka 1922 katika moja ya miji ya katikati mwa Guinea. Aliingia katika harakati za kisiasa akiwa katika rika la ujana na alikuwa akitaka uhuru wa nchi yake kutoka kwa wakoloni wa Kifaransa. Hatimaye mwaka 1958 nchi hiyo ilipata uhuru na mwaka mmoja baadaye Touré akateuliwa kuwa rais na kusalia madarakani hadi mwaka 1984 alipofariki dunia.