Apr 10, 2017 12:53 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (157)

Ndugu wasikilizaji ni nini kinachotofautisha kati a elimu ya Watu wa Nyumba ya Mtume (as) na elimu ya watu wengine ambao wamenakili elimu ya Mtume huyo Mtukufu (saw)? Hili ni swali ambalo limeulizwa na msikilizaji wetu Said Ahmad wa Tanga Tanzaia ambapo tunakuombeni muwe pamoja nasi ili tupate kulitafutia jibu kutoka kwenye maandiko matakatifu, karibuni.

Tunaanza kujibu swali hili kwa hadithi mashuhuri na ya kuaminika ambayo imepokelewa na madhehebu zote mbili za Suni na Shia kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) ambayo inasema kuhusiana na Maimamu (as): ‘’Msiwafundishe kwa sababu wao ni wajuzi zaidi kukulikoni nyinyi,’’ kama ilivyokuja katika hadithi iliyonukuliwa na at-Tabarani ambaye ni mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Ahlu Suna na wasomi wengine.

Na amefafanua maneno haya ya Mtukufu Mtume (saw) al-Hafidh bin Hajar katika kitabu chake kinachoitwa as-Swaiq al-Muhriqa kwa kusema: ‘’Mtume wa Mwenyezi Mungu aliita Quráni pamoja na kizazi chake at-Thiqlain (Vizito Viwili) kwa sababu uzito ni kila kilicho na thamani, umuhimu mkubwa na kilichohifadhiwa. Na viwili hivi ni hivyo hivyo kwa sababu kila kimoja ni madini ya elimu ya Mwenyezi Mungu, siri, hekima ya hali ya juu na hukumu za kisheria. Ni kutokana na hilo ndipo Mtume (saw) akahimiza kufuatwa na kushikamana na watukufu hawa pamoja na kujifunza kutoka kwao na kusema: ‘’Hamdu zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye alijaalia miongoni mwetu hekima ya Ahlul Beit.’’

Na al-Hafidh bin Hajar ambaye ni mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Ahlu Suna anaendelea kufafanua suala hili na kubainisha ubora wa elimu ya Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) ikilinganishwa na ya watu wengine kwa kusema: ‘’Kisha wale waliosifiwa miongoni mwao ndio wanaofahamu vyema Kitabu cha Mwemyezi Mungu na Suna ya Mtume wake (saw) kwa sababu wao ndio wale ambao hawatatengana na Kitabu hicho hadi watakapofika mbele ya Hodhi na suala hili linathibitishwa na maneno yaliyotangulia, yaani kauli ya Mtume (saw) inayosema: ‘’Msiwafundishe kwa sababu wao ni wajuzi zaidi kukulikoni nyinyi.’’ Na walifadhilishwa kwa hilo kuliko maulamaa wengine kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwaondolea uchafu na kuwatoharisha kabisa na kuwatukuza kwa karama takatifu na sifa nyingi njema.’’

 

Ndugu wasikilizaji, kuna hadithi nyingine nyingi za kuaminika pia ambazo zimepokelewa kwa njia zote mbili za Shia na Suni ambazo zinathibitisha wazi kwamba Mtume Mtukufu (saw) aliwarithisha Maimamu Watukufu wa Nyumba yake (as) elimu yote ya Quráni. Na hili ni jambo ambalo pia tunapata kulifahamu kutokana na hadithi ya Thaqalain yenyewe kwa sababu maana ya mfungamano madhubuti uliopo kati ya Quráni na Ahlul Beit (as) hautakuwa na maana ila iwapo Maimamu watakuwa wanafahamu vyema makusudio na mambo yote yaliyomo kwenye kitabu hicho kitakatifu, la sivyo, kutojua kwao kwa kina mambo yaliyomo humo kutazua pengo baina yao na kitabu hicho cha mbinguni. Mtume (saw) ameliashiria suala hili katika baadhi ya madhumuni ya hadithi ya Thaqalain ambayo alikuwa akiikariri sana mbele ya Waislamu ili wapate kuihifadhi na kutambua kwamba njia pekee ya wao kuepuka upotovu ni kushikamana kikamilifui na kwa wakati mmoja na Kitabu hiki pamoja na Watu wa Nyumba yake (as). Mtume (saw) alisisitiza waziwazi kwamba Maimamu wa Nyumba yake (as) kamwe hawawezi kumuingiza mtu kwenye mlango wa upotovu wala kumuondoa kwenye mlango wa wongofu. Na hii ina maana kwamba wanaelewa vyema milango yote ya upotovu na wongofu na wala hawawezi kukusudia kuwapotosha watu kwa sababu wamekingwa na hilo, hivyo uwezekano wa pekee unaosalia ni kuwa upotovu unatokana na kutokuwa na elimu, jambo ambalo liko mbali nao pia. Mtume Mtukufu (saw) amesema kama ilivyonukuliwa katika kitabu cha al-Kafi na vitabu vingine vya madhehebu zote mbili: ‘’Mtu anayetaka kuishi maisha kama yangu na kufa kifo kama changu na kuingia kwenye Pepo ambayo Mola wangu ameniahidi……..basi na amfuate Ali bin Abi Talib na Mawasii wake baada yangu. Hii ni kwa sababu hawatakuingizeni kwenye mlango wa upotovu wala kukuondoeni kwenye mlango wa wongofu. Hivyo msiwafundishe kwa sababu wao ni wajuzi zaidi kukulikoni nyinyi, na mimi nilimwomba Mola wangu asiwatenganishe na Kitabu (Quráni) hadi watakaponijia kwenye Hodhi wakiwa hivyo.’’

 

Ndugu wasikilizaji, katika vipindi vilivyopita tulikunukulieni hadithi nyingi ambazo zinathibitisha kwamba Ahlu Beit wa Mtume (as) wana elimu ya Kitabu kizima cha Quráni na kwamba Mwenyezi Mungu aliwapa uwezo huo wao tu na sio watu wengine kwenye viumbe wake. Kwa msingi huo wao dio warithi halisi wa mji mzima wa elimu ya Mtume Mtukufu (saw). Kama inavyoshuhudia hilo Quiráni yenyewe kwa kusema kuwa ni wao tu ndio waliotoharishwa ambao wana uwezo wa kudiriki hakika ya kina iliyohifadhiwa kwenye kitabu hicho na wala sio mambo ya dhahiri tu. Tulikunukulieni dalili za kiakili na za kunukuliwa kwenye maandiko matakatifu kuhusiana na suala hilo katika vipindi vilivyopita. Hii ina maana kwamba watukufu hao wanatofautiana sana na wapokezi wengine wa suna za Mtume Mtukufu (saw) kwa sababu mambo wanayoyajua wao ni elimu yote ya Quráni na sio baadhi ya elimu ya kitabu hicho kama ilivyo kwa baadhi ya watu ambao walisikia sehemu ndogo tu ya hadithi za Mtume na sio hadithi zote. Suala la pili ni kuwa mambo wanayoyajua hayawezi kuguswa na makosa, mughafiliko wala kusahau kwa sababu wao wametakaswa na wanajua kila hakika ya Quráni na mambo yote yaliyomo kwenye kitabu hicho. Wao hawatengani kwamwe na kitabu hicho kitakatifu cha mbinguni kwa sababu wanaofanya makosa na kusahau huwa wametengana na kujiweka mbali na kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Hii ni katika hali ambayo wasiokuwa watukufu hao kadiri watakavyojaribu kufanya na kufikia daraja ya juu kielimu lakini bado wanakabiliwa na uwezekano wa kufanya makosa kughafilika na kusahau kama inavyoshuhudiwa katika hali halisi ya mambo. Jambo la tatu ni kuwa elimu ya Maimamu Watoharifu (as) hujibu na kwenda sambamba na mahitaji ya maisha ya mwanadamu kwa sababu wao hufunguliwa milango mingi katika kila mlango mmoja wa elimu, milango ambayo hufungamana kikamilifu na elimu ya yakini. Na hili ni jambo ambalo limeashiriwa na maandiko mengine matakatifu ambayo panapo majaliwa tutayazungumzia katika kipindi kijacho cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain Inshallah. Basi hadi wakati huo, kutoka Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hatuna la ziada isipokuwa kukuageni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kusema kwaherini.

Tags