Apr 13, 2017 03:20 UTC
  • Alkhamisi, 13 Aprili, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 15 Rajab 1438 Hijria, sawa na Aprili 13, 2017.

Miaka 1436 iliyopita katika siku kama ya leo, mnamo tarehe 15 Rajab mwaka wa Pili Hijria, kibla cha Waislamu kilibadilishwa kutoka Baitul Muqaddas na kuelekea Makka kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Mayahudi daima walikuwa wakiwakebehi Waislamu kwa vile walikuwa nao wakielekea kwenye kibla hicho hicho cha Baitul Muqaddas. Hali hiyo iliwatia unyonge Waislamu na hasa Mtume Mtukufu SAW, na kwa minajili hiyo, katika siku kama ya leo Mwenyezi Mungu aliteremsha wahyi kwa Mtume SAW kupitia Malaika Jibrail AS akimtaka aelekee Makka wakati wa ibada ya Swala, badala ya Baitul Muqaddas. 

Masjidul Qiblatain

Siku kama ya leo miaka 1376 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Bibi Zaynab (AS) mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW baada ya kuvumilia mateso na machungu mengi. Bibi Zaynab AS alizaliwa mwaka wa 6 Hijiria na alipata malezi bora kutoka kwa baba yake Imam Ali AS na mama yake Bibi Fatimat Zahra AS. Mwaka 61 Hijria, Bibi Zaynab AS alishiriki katika tukio la Karbala pamoja na kaka yake Imam Hussein AS na watu wengine wa familia ya Mtume SAW. Baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) na wafuasi wake, Bibi Zaynab alikuwa mfikisha ujumbe wa hamasa ya kudumu ya Imam Hussein na wafuasi wake.

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, kulijiri tukio la umwagaji damu mkubwa katika Bustani ya Jallianwala Bagh nchini India. Mwaka 1919 na kwa lengo la kuzuia uasi na mapambano ya wananchi, serikali ya kikoloni ya Uingereza ilipasisha sheria iliyowapa polisi haki ya kuwatia mbaroni wanaharakati wa India bila sababu yoyote na kuwashikilia kwa muda usiojulikana. Sheria hiyo iliwakasirisha mno wananchi wa India na katika siku kama ya leo zaidi ya Wahindi elfu tano waliokuwa wamekusanyika kwa amani katika Bustani ya Jallianwala katika mji wa Amritsar walimiminiwa risasi kwa amri ya kamanda mmoja wa Uingereza. Watu 1200 waliuawa na wengine 4000 kujeruhiwa katika tukio hilo. Baada ya mauaji hayo, harakati ya ukombozi wa India ikiongozwa na shujaa Mahatma Ghandhi ilipamba moto.

Mahatma Ghandhi

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu, Ayatullah Mujtaba Hatami Lankarani. Ayatullah Lankarani alizaliwa katika mji wa Isfahan hapa nchini Iran na katika kipindi cha ujanani alielekea katika mji wa Najaf huko Iraq kwa ajili ya kupata masomo. Akiwa huko Najaf, Ayatullah Mujtaba Hatami Lankarani aliweza kusoma chini ya maulama wakubwa wa zama zake kama vile Dhiyaudin Iraqi, Ayatullah Mirzai Naayini na Sayyid Abul-Hassan Isfahani. Baada ya kumaliza masomo yake na kufikia daraja ya juu ya elimu alirudi katika mji alikozaliwa wa Isfahan na kutumia umri wake wote katika kutoa mafunzo ya dini tukufu ya Kiislamu. Ayatullah Lankarani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 75.

Ayatullah Mujtaba Hatami Lankarani

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, shambulio la wanamgambo wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa kundi la Mafalanja dhidi ya basi moja lililokuwa na Wapalestina na kuua watu 30 kati yao, lilipelekea kuibuka vita vya ndani nchini Lebanon. kufuatia mauaji hayo, Waislamu na wazalendo wa Lebanon walianzisha mapambano ya kukabiliana na Mafalanja hao. Muda mfupi baadaye harakati za wapiganaji wa Kipalestina pia ziliingia katika vita hivyo vya ndani vya Lebanon. Vita hivyo ambayo vilikuwa vikichochewa na utawala haramu wa Kizayuni, viliiletea hasara kubwa ya mali na roho serikali ya Beirut.

Wanamgambo wa Kikristo, Lebanon

 

Tags