Apr 23, 2017 04:24 UTC
  • Jumapili Aprili 23

Leo ni Jumapili tarehe 25 Rajab 1438 Hijiria, mwafaka na tarehe 23 April, 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 2495 iliyopita, yaani tarehe 23 April mwaka 478 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (as), kuliundwa umoja wa Delos League baina ya nchi zaidi ya 150 katika mji na kisiwa cha Ugiriki chini ya usimamizi wa Athens kwa lengo la kukabiliana na vitisho vya mfalme wa wakati huo wa Iran. Muungano huo ulikuwa muungano mkubwa wenye nguvu duniani. Aidha muungano wa Delos ulikuwa muungano wa kwanza wa kimataifa katika kukabiliana na serikali kubwa ya wakati huo ya Iran. Jina la muungano huo lilitokana na jina la kisiwa cha Delos, kwa kuwa nchi wanachama zilikusanya dhahabu na shaba na kuwekeza katika mji huo.

Siku kama ya leo miaka 471 iliyopita, yaani mwaka 953 Hijiria, alizaliwa Ayatollah, Muhammad Bin Hussein Aamili, maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, alimu mkubwa, mtaalamu wa sheria za Kiislamu na mwanatheolojia mashuhuri katika kipindi cha utawala wa Safavid. Sheikh Bahai aliyezaliwa mjini Baalbek, Lebanon. Alikuwa mmoja wa wanafunzi wa Shahidu at Thani na alikuwa fakhari ya ulimwengu wa Kiislamu. Katika kujiendeleza kimasomo alifanya safari katika maeneo mbalimbali ya dunia na kutabahari katika elimu nyingi za wakati huo, huku akiacha athari nyingi katika fani karibu 100, kama vile uhandisi, hisabati, fasihi, elimu ya hadithi, tafsiri ya Qur’ani, usulu fiqhi na kadhalika. Aidha alishughulika na uleaji wa wanafunzi wengi ambapo kila mwanafunzi alitokea kuwa alimu mkubwa. Mmoja wa wanafunzi wa Sheikh Bahai ni pamoja na Mulla Sadra Shirazi, Mulla Muhsin Feidh Kashan, Fayadh Lahiji, Muhaqiqi Sabzawari, Sayyid Hassan Karki, Sayyid Majid Bahrani na Mulla Muhammad Taqi Majlisi. Ayatollah, Muhammad Bin Hussein Aamili alifariki dunia mwaka 1031 Hijiria.

Siku kama ya leo miaka 608 iliyopita, alifariki dunia mjini Kerman, moja ya miji ya Iran Shah Nimatullah Wali, mmoja wa mawalii wakubwa wa Kishia. Nurud-Din Shah Nimatullah Bin Sayyid Abdullah Kermani, alikuwa miongoni mwa wataalamu wa elimu ya irfani (ya kumjua Mwenyezi Mungu) wa karne ya tisa Hijiria huku akiwa alizaliwa yapata mwaka 730 mjini Kermani. Shah Nimatullah Wali alikuwa miongoni mwa wafuasi wa Hafez Shirazi. Tariqa ya mwanazuoni huyo ilijitenga mbali na ifrat na tafrit na kadhalika itikadi potofu, kama ambavyo pia alikuwa mfuasi wa fikra na athari za Ibn Arabi. ‘Amaanat’ ‘Sharh Golshan Razi’ na ‘Nasihatul-Muluuk' ni miongoni mwa vitabu alivyoandika.

Siku kama ya leo miaka 401 iliyopita, alizaliwa William Shakespeare, mshairi na mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Uingereza. Shakespeare alianza kazi zake za usanii sambamba na kushiriki katika michezo ya kuigiza. Alipata umashuhuri mkubwa katika fani hiyo. Kazi zake za kisanii zilikuwa mchanganyiko wa sanaa iliyoakisi majonzi na vichekesho. 

Siku kama ya leo miaka 199 alizaliwa  James Anthony Froude, mwandishi na mwanahistoria wa Uingereza. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi Anthony Froude alijiunga na Chuo Kikuu cha Oxford. Awali alikusudia kujiunga na kanisa. Hata hivyo wasi wasi aliokuwa nao juu ya masuala ya kidini na kadhalika miamala ya kanisa, ilimfanya Froude kuachana na azma yake hiyo. Kitabu chake cha ‘Ilhamu ya Kisasi kutokana na Imani’ kiliibua hasira ya kanisa. Hata hivyo kitabu muhimu cha msomi huyo ni kile alichokipa jina la ‘Historia ya Uingereza’ ambacho alikiandika kwa kipindi cha miaka 20. Kadhalika aliandika historia ya shakhsia mbalimbali kama vile ‘Thomas Carlyle’ ‘Martin Luther’ na ‘Julius Caesar.’

Siku kama ya leo miaka 159 iliyopita, alizaliwa mwanafizikia Max Planck wa Ujerumani ambaye pia alikuwa mtaalamu wa hesabati aliyebuni nadharia ya kwanta, katika elimu ya fizikia au Quantum Theory. Mwaka 1918 Max Planck alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel kwa kugundua nadharia hiyo. Planck ambaye alikuwa mpinzani mkubwa wa dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolph Hitler, alifanya utafiti mkubwa katika nyanja za mwendojoto au Themodynamic, fizikia nadharia, joto, mnururisho na nuru na kuandika vitabu kadhaa katika uwanja huo.

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Aprili 1992, alifariki dunia Satyajit Ray mwandishi na mtengeneza filamu mashuhuri wa India. Satyajit Ray alizaliwa mwaka 1921, na filamu zake za kijamii ziligusa zaidi hisia za jamii ya wananchi wa nchi hiyo. Jambo hilo lilimfanya apendwe sana na wananchi wa India. Filamu ya kwanza ya Satyajit Ray ilikuwa Pather Panchali (Song of The Little Road) ambayo wachambuzi wa filamu wanasema, iliifikisha sanaa ya filamu ya India kwenye kilele chake.

Na siku kama ya leo miaka 33 iliyopita sawa na tarehe 3 Ordibehest, utawala wa Kibaath wa Iraq ulianzisha vita na mashambulizi dhidi ya meli za kubeba mafuta za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika maji ya Ghuba ya Uajemi. Baada ya kupita karibu miaka minne tangu Saddam Hussein aivamie ardhi ya Iran, Iraq ikisaidiwa na madola makubwa, ilichukua hatua ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran kwa kutumia wenzo wa kuzuia uuzaji nje mafuta yake na badala yake wazidishe uzalisha wa mafuta katika nchi za Kiarabu ili kufidia nakisi ya mafuta ya Iran katika masoko ya kimataifa. Kwa misingi huo walianza kushambulia meli za kubeba mafuta za Iran na bandari za kupakia bidhaa hiyo hapa nchini. Siku hiyo Iraq ikisaidiwa na Marekani na nchi nyingine za Magharibi, ilitumia ndege za kivita za Super Standard za Ufaransa kushambulia kisiwa cha Khark na meli zilizokuwa zimebeba mafuta za Iran.