Apr 30, 2017 13:07 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya tatu ya makala yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar.

Katika kipindi kilichopita sambamba na kuzungumzia jinai za Mabudha dhidi ya Waislamu wa Rohingya, tuliashiria pia namna ambavyo viongozi wa serikali ya Burma wanavyokana kuhusiaka na jinai hizo. Kati ya viongozi hao, ni Aung San Suu Kyi, mshindi wa zawadi ya Nobel wa nchini Myanmar ambaye sambamba na kuuona mgogoro huo kama mdogo, alikadhibisha kabisa kuwepo mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu wa Rohingya. Katika fremu hiyo mwanamke huyo eti mpigania demokrasia hakuna mahala popote alipowahi kulaani jinai hizo wala kuwatetea Waislamu wa Rohingya wanaouawa kwa namna ya kutisha nchini Myanmar. Kwa mfano tu akijibu swali la mwandishi wa habari, Suu Kyi alisema: "Sijui ikiwa Waislamu wa Rohingya ni raia wa Myanmar au la." Mwisho wa kunukuu.

Makazi ya Waislamu yaliyobomolewa na Mabudha kwa kushirikiana na askari wa serikali

Matamshi hayo yanakinzana kabisa na hotuba aliyoitoa katika bunge la Myanmar pale aliposema: "Katika fremu ya mabadiliko kuelekea demokrasia ya kweli na roho ya umoja, kuheshimiwa sheria za usawa na kuheshimiana, ni jambo muhimu sana kwa wabunge wote kufanya juhudi katika kupitisha sheria ambazo zitaheshimu usawa wa jamii ya wachache nchini." Mwisho wa kunukuu. Hata hivyo suala la kusikitisha ni kwamba Waislamu wa Rohingya hawana nafasi yoyote katika pendekezo hilo la Aung San Suu Kyi na maneno hayo yalikuwa ni hadaa tupu. Hii ni kwa kuwa hadi sasa mwanamke huyo muitifaki wa madola ya Magharibi, bado hajawatambua Waislamu wa Rohingya kuwa ni raia wa Myanmar.

Kwa hakika matamshi ya wanasiasa wa Myanmar hayatofautiani na misimamo hasi ya asasi za kimataifa kuhusiana na jinai za Mabudha kuwalenga Waislamu wa Burma. Hii ni kusema kuwa, tangu awali Umoja wa Mataifa umekuwa kimya kwa muda mrefu sana kuhusiana na kadhia hiyo.

Watoto wa Waislamu wa Myanmar na hali ngumu ya kimaisha

Kama tulivyosema awali, misimamo isiyokuwa ya kuwajibika na isiyokuwa na taathira yoyote ya Umoja wa Mataifa na wanachama wa umoja huo juu ya mauaji na jinai dhidi ya Waislamu wa Rohingya, inakumbusha kimya kirefu kuhusiana na mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Bosnia na Herzegovina barani Ulaya. Kwa kuangalia historia ya Umoja wa Mataifa inatubainikia kuwa, wakati wowote kunapojiri mauaji dhidi ya Waislamu, umoja huo ima huwa unahusika katika jinai hizo kwa kushindwa kwake kuchukua hatua za maana za kuzuia mauaji hayo na wakati mwingine hutoa maazimio yasiyo na taathira yoyote katika uwanja huo. Hata hivyo swali la msingi ni hili kwamba, je, lau kama mauaji kama hayo yanayowakumba Waislamu wa Myanmar, yangekuwa yanawakabili watu wa dini nyingine tofauti na Waislamu, ni upi ungekuwa msimamo wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala hilo? Hivi lau kama wahanga wa jinai za Mabudha wangekuwa ni watu wenye imani tofauti na ya Uislamu, tungeendelea kushuhudia kimya na msimamo wa kutojali unaoonyeshwa leo na madola ya Magharibi kuhusu Waislamu? Suala la kushangaza zaidi ni kwamba, si tu kuwa asasi za kimataifa na wanaharakati wa utetezi wa haki za binaadamu wamesalia kimya kunako jinai wanazofanyiwa Waislamu wa Myanmar, bali hali hiyo imefikia hatua ya kuwatunuku zawadi mbalimbali viongozi wa nchi hiyo.

Walimwengu duniani wakipaza sauti kulaani mauaji dhidi ya Waislamu wa Rohingya

Kiasi kwamba, katika kikao cha pamoja cha Wizara za Mambo ya Nje za nchi wanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya hapo tarehe 22 April mwaka 2013, kulitangazwa kuwa: "Kutokana na serikali kutekeleza marekebisho ya kisiasa nchini Burma, hivyo vikwazo vya kibiashara na kiuchumi iliyowekewa nchi hiyo na viongozi wake vinaondolewa kikamilifu." Mwisho wa kunukuu. Ikumbukwe kuwa uamuzi huo ulikuja ikiwa imepita miezi michache baada ya serikali hiyo kuwaua zaidi ya Waislamu elfu 20. Hii ni katika hali ambayo azimio lililotolewa mwezi Disemba mwaka 1946 linasema: "Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, mauaji ya umati yanahesabiwa kuwa ni jinai, sawa sawa mauaji hayo yawe yametokea katika kipindi cha vita au kipindi cha amani. Watiaji saini wote wa hati ya Umoja wa Mataifa watatakiwa kuungana pamoja kwa lengo la kuwaokoa wahanga kutokana na balaa hilo la kibinaadamu na lenye kuchukiza." Mwisho wa kunukuu.

**************************************

Ndugu wasikilizaji Waislamu wa Rohingya kama tulivyosema, ndio jamii ya watu waliodhulumiwa zaidi duniani. Hadi sasa serikali ya Burma imekataa kikamilifu kuwapatia vitambulisho vya uraia Waislamu hao ambao uepo wao hauwezi kupuuzwa.

Vilio vya Waislamu duniani wakitaka kukomeshwa jinai dhidi ya wenzao huko Burma

Na ni kwa ajili hiyo ndio maana wakawa wanakabiliwa na kila aina ya jinai na mauaji kutoka kwa Mabudha. Licha ya kwamba awali ilitarajiwa kwamba, kuingia madarakani chama cha Aung San Suu Kyi, kungesaidia kuboresha hali ya Waislamu wa nchi hiyo, hata hivyo mwanamke huyo amepuuza kabisa kilio cha Waislamu hao wa Rohingya na hivyo akawa amepigilia msumari wa mateso dhidi yao. Katika miaka ya hivi karibuni Waislamu wengi wa Rohingya wameuawa au kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi ya kutisha ya Mabudha makatili hususan katika jimbo la Rakhine nchini humo. Waislamu hao hulazimika kukimbia mauaji kwa kutumia mitumbwi midogo ambayo kutokana na udogo wake, huwafanya akthari yao kupoteza maisha kwa kuzama majini. Katika hali hiyo Waislamu hao huwa wana machaguo mawili tu, ima wauawe na Mabudha kwa namna ya kutisha au wakimbie kupitia njia hatari zinazoambatana na kifo. Jinai za Mabudha wa Burma huwa hazitofautishi Waislamu wanaume na wanawake, watoto na vijana, wazee au watoto wachanga, kama tulivyoona katika kipindi kilichopita kuhusiana na mtoto wa miezi 16 kwa jina la Muhammad ambaye alikufa maji na mwili wake kuokotwa kando ya mto Naf. 

Sehemu nyingine ya malalamiko ya walimwengu, juu ya jinai hizo

Tukio ambalo lilikumbushia kifo cha Alan Kurdi, mtoto mchanga wa Syria aliyekufa maji akiwa na familia yake na mwili wake kuokotwa baadaye katika pwani ya Uturuki na kuibua hisia za walimwengu wote.Mtoto Muhammad asiye na hatia na ambaye hata alikuwa hajafikisha umri wa miaka miwili, alikuwa mhanga wa jinai na taasubi za kibinaadamu za Mabudha wa Burma. Swali la kujiuliza ni hili kwamba, je, nini lilikuwa kosa la mtoto huyo hadi kufikia kukatishiwa maisha yake?

*********************************************

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako kipindi kilichoko hewani ni Makala ya tatu yanayozungumzia jinai za Mabudha makatili wanaowalenga Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar. Ndugu wasikilizaji mtafahamu kwamba,  licha ya taasisi za kimataifa kuituhumu serikali ya Naypyidaw katika kuhusiaka kwake na ukiukaji wa wazi wa haki za Waislamu wa Rohingya, lakini serikali hiyo imekuwa ikikadhibisha tuhuma hizo.

 Aung San Suu Kyi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Myanmar na kiongozi wa harakati ya kidemokrasia Burma

Hata hivyo pamoja na hayo serikali ya nchi hiyo haijaweza kuficha ukweli wa jinai zake ambapo hatimaye imelazimika kukubali kufanyika uchungunzi kuhusiana na suala hilo. Kufuatia mashinikizo hayo hatimaye Aung San Suu Kyi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Myanmar na kiongozi wa harakati ya kidemokrasia nchini humo alimwalika Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni kiongozi wa kamisheni ya uchunguzi wa ukandamizaji wa haki za binaadamu ili kutembelea jimbo la Rakhine nchini Myanmar. Hata hivyo pamoja na Annan kuzuru Myanmar na kufanya uchunguzi wake, hakuna mabadiliko yoyote yaliyopatikana kuhusiana na ukatili na jinai za Mabudha dhidi ya Waislamu hao wa Rohingya. Baba wa mtoto Muhammad aliyefariki dunia kwa kuzama maji (yaani Zafar Alam) anasimulia kwa kusema: "Kabla ya timu ya kamisheni hiyo kutembelea maeneo kulipojiri mauaji, jeshi lilikuwa likiwaondoa wakazi wa eneo hilo. Wakati kulipofanyika uchaguzi nchini Myanmar, nilifikiria kwamba ushindi wa Aung San Suu Kyi ungesaidia kupunguza machungu ya Waislamu. Hata hivyo hali ya mambo ilikuwa tofauti na matarajio hayo. Tangu mwanamke huyo alipoingia madarakani hakuna kitu kilichobadilika kwani ukaatili na udhia bado unatuandama." Mwisho wa kunukuu.

Waislamu wakionyesha hisia zao kutokana na ukubwa wa jinai dhidi yao

Ukweli ni kwamba, Aung San Suu Kyi na jeshi la Myanmar kwa pamoja wanataka kuwaondoa Waislamu wa Rohingya kutoka mji wao asili wa Rakhine, na ndio maana mwanamke huyo anakadhabisha habari ya kuwepo jinai zinazofanywa na jeshi la Myanmar.

Katika fremu hiyo Aung San Suu Kyi ambaye kwa sasa ni mshauri wa serikali ya Myanmar aliitisha kikao na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Nchi za Kusini mwa Asia kwa ajili ya kuchunguza hali ya jimbo la Rakhine. Katika kikao hicho mwanamama huyo alisema: "Serikali ya Myanmar inafungamana na ahadi zake kwa ajili ya utatuzi wa mgogoro wa eneo la Rakhine. Hata hivyo utatuzi huo unahitajia muda Zaidi." Mwisho wa kunukuu. Kuhusiana na kauli hiyo, Zafar Alam, baba wa mtoto Muhammad anasema: "Nataka dunia yote ifahamu kwamba, serikali ya Myanmar haifai kupewa muda wowote wa ziada. Ikiwa dunia itazembea hata kidogo katika hilo, basi serikali hiyo itawaua Waislamu wote wa kabila la Rohingya." Mwisho wa kunukuu.

Maandamano ya kulaani ukatili dhidi ya Waislamu wa ohingya yanasikika kila mahala

Kitendo cha kutosikika vilio, machozi, taabu na mateso ya muda mrefu ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar kwa asasi zinazojinadi kuwa watetezi wa haki za binaadamu, kumeifanya serikali ya Burma kupata jeuri zaidi katika mwenendo wake wa ukatili. Katika mwenendo huo, maelfu ya Waislamu wasio na hatia wameuawa kikatili na Mabudha na askari wa serikali wasio na mioyo ya ubinaadamu.

***************************

Ofisi ya Shirika la Kushughulikia Masuala ya Haki za Binadamu sambamba na kutoa ripoti yake mwezi Novemba 2016 kuhusiana na ukandamizaji wa haki za binaadamu dhidi ya Waislamu wa Rohingya, ilikiri juu ya Waislamu  hao kufanyiwa jinai hizo kukiwemo kuuawa , kufanyiwa ukandamizaji wa kuwahamisha kwa nguvu kutoka katika maeneo yao asili, kuwatisha kiroho na kiusalama, kuwanyima haki ya matibabu na elimu, kuwafanyisha kazi  ngumu kwa lazima na kuwafanyia ukatili wa kijinsia kukiwemo kuwabaka wanawake na mabinti wa Kiislamu. Kwa hakika hata jeshi la Myanmar nalo haliwaonei huruma watu wa jamii hiyo. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa hapo tarehe 19 Disemba mwaka jana, askari na polisi wa serikali ya Myanmar wanawamiminia risasi ovyo raia wa kawaida na wasio na hatia yoyote na kuwaua.

Mabudha wakatili

Aidha askari hao huwabaka wanawake na mabinti wa Kiislamu, kuzichoma moto nyumba zao, kuwatia mbaroni wanaume na kuwazuilia mahala kuzikojulikana bila ya kufunguliwa mashtaka. Katika hujuma za mwaka 2012 wakati Mabudha walipoanzisha mauaji makali dhidi ya Waislamu hao, walichoma moto kikamilifu vijiji kadhaa vya Waislamu na kuwalazimu Waislamu hao kwenda kuishi katika kambi za muda za wakimbizi. Baada ya hapo, mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu hao huko kaskazini mwa taifa hilo yaliibuka tena mwezi Oktoba mwaka jana baada ya askari tisa wa kulinda mpaka wa Myanmar kuuawa na watu wasiojulikana. Hata hivyo na bila ya kufanya uchunguzi wala kuwepo ushahidi wowote, serikali ya Burma iliwatuhumu Waislamu wa Rohingya kuwa ndio waliohusika na shambulizi hilo.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya tatu ya makala haya yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar inakomea hapa. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

 

 

Tags