May 24, 2017 18:15 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (77)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia na kujadili moja ya tabia mbaya nayo ni ya kufurahia shida, masaibu na matatizo ya watu wengine na tulisema kwamba, kitendo hicho huwa na athari mbaya hapa duniani na kesho akhera.

Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 77 ya mfululizo huu, kitazunghumzia moja ya tabia nyingine mbaya ambayo inahesabiwa kuwa ni miongoni mwa maradhi ya kinafsi nayo ni husuda.  Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

Husuda maana yake ni mtu kutamani neema aliyonayo mtu imtoke hata kama neema hiyo hatoipata yeye. Kwa maana nyingine hasidi ni mtu anayeonea kijicho mafanikio ya wengine. Mtu mwenye husuda ni yule ambaye anachukia na kusononeka kutokana na mtu fulani kuwa na neema, furaha, mafanikio au maendeleo ya watu wengine iwe ni ya kimali, kielimu, kikazi na hata masuala ya kimaanawi. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 120 ya Surat Aal-Imran:

Ikikupateni kheri huwaudhi. Na ikikupateni shari wanafurahia. Na nyinyi mkisubiri na mkajizuilia, hila zao hazitakudhuruni kitu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyazunguka yote wayatendayo.

Aya hii inabainisha kwamba, kama mtu ataonyesha furaha kutokana na kutoweka na kuondoka neema za watu wengine au akakasirika kutokana na mtu fulani kupata neema, mtu wa aina hiyo huwa ni hasidi na mwenye sifa ya husuda. Aidha aya hiyo inataja sifa mbili za hasidi. Mosi, ni mwenye kufurahia mambo mabaya ya watu wengine na pili huchukia na kukasirika kutokana na furaha za watu wengine.

 

Kiuhakika ni kuwa, husuda maana yake ni kutamani kutoweka na kuondoka neema za watu wengine, bila kujali kama neema hiyo imfikie yeye au hata kama hatoipata; kwani wakati mwingine hasidi huyo huwa na neema hiyo hiyo aliyonayo mwenzake lakini pamoja na hayo hutamani kutoweka neema za wengine.  Imam Ali bin Abi Twalib as amenukuliwa akisema: Hasidi huchukia kutokana na neema za anayemhusudu kiasi kwamba, kuondokewa na neema mtu huyo yeye hulihesabu jambo hilo kama ni neema kwake.

Mtu mwenye husuda daima huwa katika taabu, mashaka na mashinikizo, kwani neema za Mwenyezi Mungu kwa waja wake hazina kikomo na katu si zenye kumalizika. Hasidi huhuzunika na kuwa na ghamu kwa kila neema anayoina kwa wengine. Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana Imam Ali bin Abi Twalib as anasema: Matunda ya husuda, ni taabu na mashaka duniani na akhera." Hasidi siku zote ni mwenye kujiona kuwa amenyimwa neema na kwamba, amepata hasara na sababu ya hilo ni mwenzake kuwa na neema na ndio maana daima husikitika na kupata ghamu na huzuni ambayo imechanganyika na hasira na ghadhabu.

Maradhi haya ya kinafsi endapo hayatapatiwa tiba huwa na athari haribifu kwa mwili wa mwanadamu. Kiuhakika ni kuwa, husuda hutokomeza na kuangamiza roho na mwili wa hasidi. Imam Ali as anasema kuwa: Husuda huyeyusha mwili. Na katika hadithi nyingine Kiongozi huyo wa wachamungu amenukuliwa akisema kuwa, mtu ambaye hataweza kuishinda husuda yake basi mwili wake huwa mahala pake pa kuzikiwa.

Husuda ni moja ya maradhi mabaya mno ya kiroho na kisaikolojia. Katika kuelezea ubaya wa maradhi haya, Imam Ali bin Abi Twalib as anasema: Sijamuona dhalimu kama hasidi ambaye anafanana zaidi na madhulumu, ana roho inayohangaika na kutangatanga na moyo wenye huzuni na usio na utulivu.

Kwa hakika hasidi daima ni mtu mwenye huzuni na ghamu. Kikawaida mahasidi hukumbwa na hali ya msongo wa mawazo, kwani kwa mujibu wa Imam Ali (as), husuda huyafanya maisha ya hasidi kuwa machungu.

Hasidi kwa husuda yake hujiweka katika daraja ya uadui na upinzani dhidi ya Mola Muumba. Hii ni kutokana na kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu huwapatia waja wake neema kutokana na hekima na hali ya waja wake. Lakini mtu mwenye husuda hutamani neema aliyonayo mtu imtokea kama vile yeye ni mjuzi zaidi ya Mwenyezi Mungu. Kwa mtazamo wa hasidi ni kuwa, mtu ambaye anamhusudu hastahiki neema aliyopatiwa na Mwenyezi Mungu. Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa: Mwenyezi Mungu SWT alimwambia Nabii Mussa as kwamba: Hasidi ana ghadhabu na neema zangu, na ni mwenye kuasi na kulalamikia neema ambazo nimewapatia waja wangu.

Hadithi ya Uongofu

 

Aidha mbora huyo wa viumbe amenukuliwa akizungumzia kuweko maadui wa neema za Mwenyezi Mungu kwa kusema: Kwa hakika kuna maadui wa neema za Mwenyezi Mungu. Akaulizwa, maadui hawa ni akina nani? Mtume saw akasema:  Watu ambao wanafanya husuda kwa kile ambacho wengine wamepatiwa na Mwenyezi Mungu.

Kwa muktadha huo, hasidi kwa kujua au kwa kutokujua, kitendo chake hicho cha kufanya husuda huwa ni kupambana na Mwenyezi Mungu, na kitendo hicho huwa na madhara kwa imani na dini yake. Ni kwa msingi huo, ndio maana Imam Ali as anasema kuwa, husuda ni balaa ya dini.

Kwa kuzingatia yaliyotangulia tunafahamu kwamba, mahasidi hawana imani, kwani katika mahusiano baina ya viwili hivi kuna nukta hasi ambayo inaashiria kwamba, penye husuda hakuna dini na penye dini hakuna husuda. Kwa maana kwamba, pindi husuda inapoingia katika moyo wa mwanadamu, kidogo kidogo imani nayo hufifia. Kwa hakika uhusiano baina ya husuda na kuondoka imani uko kwa namna ambayo unashabihishwa na moto unaoondoa imani hiyo.

 Imam Ali (a.s.) amesema katika Hotuba ya 86 ya Nahaj al-Balagha alipokuwa akikemea tabia mbaya ya husuda kwamba:  "Msihusudiane, kwani husuda inakula imani, kama moto ulavyo kuni." Aidha amesema kuwa: "Siha ya mwili ni husuda kuwa chache."

Kwa hakika maradhi ya husuda huleta maradhi mengine ambapo kila moja ya maradhi hayo yanatosha kupotosha na kuondoa ubinadamu wa mtu. Kwa msingi huo kama hasidi atataka kuendeleza uhasidi wake na kulifanya hilo kama wenzo wake ni lazima atumie dhambi nyingine kama kusengenya, tuhuma, uzushi uongo na mengineyo.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki kwa leo umemalizika hivyo sina budi kukomea hapa kwa leo, nikiwa na matumaini kwamba, mtajiunga nami wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo wa kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Ninakuageni nikimuomba Mwenyezi Mungu atuepushie husuda katika nyoyo zetu.

Wassalaamu alaykum warahmatullahi wabarakaatuh…..