Jun 03, 2017 14:40 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya nane ya makala yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia matatizo mbalimbali yanayowapata wahajiri wanapokuwa safarini kwenda nchi za jirani na Myanmar ili kuokoa nafsi zao kutokana na ukatili wa jeshi la nchi hiyo. Leo pia tutaendelea kuzungumzia suala hilo na radiamali ya Umoja wa Mataifa kuhusu jinai hizo. Ndugu wasikilizaji kutokana na umasikini wao, anapotokea mtu mwenye uwezo wa kifedha kwa ajili ya kuwanunua wasichana wahajiri kutoka mikononi mwa wafanya magendo ya binaadamu, basi huweza kununua idadi kadhaa ya wasichana hao na kuwatumia anavyotaka na kinyume kabisa na maadili ya kibinaadamu. Ifahamike kuwa vitendo hivyo hufanyika mbele ya kimya cha jamii ya kimataifa na asasi zinazojinadi kuwa watetezi wa haki za binaadamu, suala ambalo linatia wasi wasi mkubwa.

Baada ya wahajiri hao kufikishwa nchini Thailand, wafanya magendo hao huwauza wasichana na wanawake wa Rohingya kwa magenge mengine ya mabaharia na wavuvi wa nchi hiyo kwa thamani ya Dola 900 na kuwafanya watumwa katika shughuli hizo za uvuvi. Hii ikiwa na maana kwamba, wavuvi hao baadaye huwauza wahajiri hao katika biashara zao za samaki, ambapo badala ya kuuza samaki, hujihusisha pia na mauzo ya binaadamu hasa kwa kuwa biashara ya magendo ya binaadamu ni yenye faida kubwa. Uchunguzi unaonyesha kwamba baadhi ya viongozi wa Thailand, wana mahusiano ya moja kwa moja na wamiliki wa kambi za wahajiri. Katika mwenendo huo, viongozi hao hushirikiana na wafanya magendo hao na kuwasaidia katika kuwauza wahajiri hao kwa wavuvi na kujipatia kiasi kikubwa cha fedha.

Radiamali isiyo na taathira ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na hali ya Waislamu wa Rohingya

Aidha mmoja wa mawakala wa wauza watumwa alinukuliwa akilieleza gazeti moja la Uingereza kuwa, mwaka jana binafsi aliuza kwa namna ya utumwa kwa akali wahajiri 100 kwa wavuvi wa Thailand ambapo kila muhajiri mmoja aliuzwa kwa kiasi cha Dola 900. Kwa hakika Waislamu wa Rohingya wanakumbwa na udhalilishaji huo wa kufikia kuuzwa kama bidhaa kutokana na ukatili, ukandamizaji na dhulma ya hali ya juu wanayofanyiwa na Mabudha wanaoshirikiana na askari wa serikali ya Myanmar. Hata hivyo wakati wanapojaribu kuokoa maisha yao wahajiri hao hujikuta wakiangukia mikononi mwa wafanya magendo hao katili. Hakuna shaka kwamba machungu yote haya yanawakuta kutokana na jamii ya Rohingya kunyimwa vitambulisho vya uraia na serikali ya Naypyidaw ambayo inakataa kuwatambua watu wa jamii hiyo kuwa raia wa nchi hiyo.

************************************************************

Waislamu wa Rohingya hujikuta vyambo vya wafanya magendo ya binaadamu kwa kuwa, wafanya magendo hao ambao awali huwa wanakubaliana  kupokea kiasi cha Dola 200-300 ili kuwafikisha Malaysia, huingiwa na tamaa ya pesa ambapo badala ya kutekeleza makubaliano ya awali ya kuwafikisha mahala salama, huwa wanawazuilia katika kambi za siri mithili ya jela katika misitu ya Thailand.

Waislamu wa Myanmar waliokimbia ukatili wa jeshi na Mabudha wa nchi hiyo

Safari hiyo huchukua wiki kadhaa wakiwa katika kambi hizo. Katika kipindi hicho wahajiri hao wa Rohingya hukumbwa na mateso zaidi hasa kwa kuzingatia kuwa, kambi hizo huwa hazina nyenzo muhimu za kimaisha kama vile chakula, maji na wamadawa. Kutokana na mazingira hayo akthari ya wahajiri hao Waislamu hupoteza maisha huku wale ambao wamebakia hai wakivumilia matatizo mengi yanayowakabili. Aidha Waislamu wa Rohingya katika kambi hizo, huishi kama wafungwa. Hii ni kwa kuwa kila siku huwa wanapigwa viboko, kuteswa na kudhalilishwa. Mara nyingi wahajiri hao hukumbwa na mateso hayo ili kuzishinikiza familia zao kulipia kiasi cha Dola 2000 ili waweze kuachiliwa huru na wafanya magendo hao. Kambi hizo za kifo zinaweza kuwa ni maeneo ya kutisha zaidi katika eneo la Asia Mashariki. Mwislamu mmoja mwenye umri wa miaka 23 ambaye aliishi kwa miezi kadhaa katika kambi hizo za kuogofya anaelezea kwa kusema: “Tulikuwa tukipigwa kila siku asubuhi na jioni. Walikuwa wakitufanyia ukatili huo ili kuzilazimisha familia zetu kulipa kikomboleo. Walikuwa wakitupiga hivyo kutudhoofisha kwa lengo la kutufanya tusiweze kutoroka.” Mwisho wa kunukuu.

Polisi wa serikali wakiwazingira watu wa jamii ya Rohingya

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, wahajiri hao huwa wanapakizwa katika boti ambazo huwa zimefurika watu na kupelekwa moja kwa moja kwa wafanya magendo ya binaadamu na wakati mwingine wahajiri hao masikini, hujikuta wakitoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuachiliwa huru. Kwa hakika masaibu na matatizo ya Waislamu wa Myanmar ambao wamekuwa wakimbizi nchini kwao hayana ukomo wa kuelezwa. Watu hao ambao wamefukuzwa kwa namna ya kutisha na serikali ya nchi yao, pia huko ughaibuni hawana mahala pa kukimbilia. Ima huangukia mikononi mwa magenge ya wahalifu wa Thailand na kuuawa kwa namna ya kutisha katika misitu iliyo mpakani mwa nchi hiyo huku viungo vyao vikiporwa au miili yao kutupwa katika maji ya mto au baharini. Wakati mwingine wahajiri hao hutupwa baharini wakiwa hai na kupoteza maisha au kuangukia mikononi mwa wafanya magendo ya binaadamu nchini Malaysia, Indonesia au Singapore. Ukweli ni kwamba wafanya magendo ya binaadamu wanawachukulia wahajiri hao Waislamu wa Rohingya kama neema isiyo na mithili kutokana na kwamba huwaletea pato kubwa la fedha.

****************************************************

Ndugu wasikilizaji kuendelea hali hiyo ya mateso, kumeufanya hata Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine kuonyesha wasi wasi wake mkubwa na hata kuionya serikali ya Myanmar kutokana na hatua yake ya kuwafukuza watu wote wa jamii hiyo ya wachache nchini humo.

Wanawake wa jamii madhlumu ya Rohingya

Kuhusiana na suala hilo Young Hee Lee, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa ambaye anashughulikia hali za Waislamu wa Rohingya waliokimbilia nchini Bangladesh kutoka Myanmar anasema: “Kuna haja ya kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na mateso yanayowakabili watu wa jamii hiyo ya Rohingya.” Mwisho wa kunukuu. Kadhalika Young Hee Lee sambamba na kuashiria juu ya uwezekano wa kufukuzwa Waislamu wote nchini Burma, amesema kuwa, lengo kuu la watawala wa nchi hiyo ni kuiepusha Myanmar na uwepo wa watu wa jamii hiyo. Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa alisikitishwa na habari za kutisha zinazothibitisha kushtadi ukatili dhidi ya watu wa jamii hiyo ya wachache nchini Burma kinyume na alivyokuwa akidhani hapo awali. Kwa mujibu wa Young Hee Lee, wakimbizi hao wa Rohingya walimwambia kuwa, wanawake wa Kiislamu wa jamii hiyo wanabakwa na kunajisiwa kwa namna ya kutisha na askari wa serikali, kuchinjwa wanaume wao na kuchomwa moto wakiwa hai watoto wa jamii hiyo. Kadhalika Lee anasema kuwa, wimbi jipya la ukatili na mauaji lililoibuka mwezi Oktoba mwaka jana katika jimbo la Rakhine lilisababisha maelfu ya Waislamu wa jamii hiyo ya Rohingya kuwa wakimbizi eneo la Cox's Bazar nchini Bangladesh.

Young Hee Lee, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa ambaye anashughulikia hali za Waislamu wa Rohingya

Kabla ya hapo pia Umoja wa Mataifa ulionya juu ya ongezeko la ukatili wa serikali dhidi ya watu wa jamii hiyo ya Rohingya eneo la Rakhine sambamba na kuzitaja jinai hizo kuwa ni jinai dhidi ya binaadamu.

****************************************************

Baada ya wataalamu wa masuala ya haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa kuendesha uchunguzi na muda na kutoa ripoti ambayo iliyataja mashambulizi ya jeshi na polisi ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya kuwa yanayoweza kuwa jinai dhidi ya binaadamu na maangamizi ya kikabila, hatimaye Umoja wa Ulaya nao ulitoa pendekezo la kutumwa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa nchini Burma ili kufuatilia jinai hizo za maafisa usalama wa taifa hilo kuwalenga Waislamu.

Tume ya Bi Young Hee Lee, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa 

Ni kufuatia hatua hiyo ndipo Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa likaafiki kutumwa tume ya kubaini ukweli wa jinai za askari hao wa serikali dhidi ya jamii ya Waislamu wa jimbo la Rakhine. Wasi wasi wa Umoja wa Mataifa ulikuja katika hali ambayo mashambulizi na jinai zilikuwa zimeshika kasi kuwalenga Waislamu hao wa Rohingya. Hata hivyo mwakilishi wa Myanmar katika Umoja wa Mataifa alifanya juhudi kubwa kujaribu kupinga uamuzi huo na kuutaja kuwa usiokubalika. Pamoja na hayo Baraza la Haki za Binaadamu la umoja huo lilipitisha azimio ambalo lilitaka kuchukuliwa hatua kali dhidi ya wahusika wa jinai hizo dhidi ya binaadamu. Tangu serikali ya Naypyidaw ilipoanza kutekeleza siasa za ukandamizaji na ukatili kwa kutumia askari wake hapo mwezi Oktoba mwaka jana, karibu watu elfu 75 wakazi wa jimbo hilo wamekuwa wakimbizi nchini Bangladesh.

Jamii madhlumu ya Waislamu wa Myanmar wakiwa katika boti zinazokatisha maisha yao

Kadhalika ofisi ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch imeelezea uwezekano wa kujiri mauaji ya mamia ya Waislamu katika mashambulizi hayo yaliyofanywa katika kipindi cha miezi michache ya hivi karibuni. Pamoja na hayo viongozi wa serikali ya Burma na kwa ujeuri wa hali ya juu wametetea jinai na ukatili wao huo.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya nane ya makala haya yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, Was-Salaamu Alaykum Warahmatullahi wa Barakaatu…………./

 

Tags