Jumatatu 07 Agosti, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 14 Dhulqaada 1438 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Agosti 2017.
Siku kama ya leo miaka 9 iliyopita vikosi vya jeshi la Georgia vikisaidiwa na serikali ya Marekani vililishambulia eneo linalopigania kujitenga la Ossetia ya Kusini huko kaskazini mwa nchi hiyo. Mamia ya raia wasio na hatia wala ulinzi waliuawa na kujeruhiwa kwenye mashambulio hayo. Siku moja baadaye, wanajeshi wa Russia waliingilia kati na kuamua kuwaunga mkono wapiganaji wanaopigania kujitenga wa Ossetia ya Kusini na kulilazimisha jeshi la Georgia kurudi nyuma. Vikosi vya jeshi la Russia vilifanikiwa kuiteka bandari muhimu ya Patumi na kusonga mbele karibu na Tiblis mji mkuu wa nchi hiyo. Jeshi la Russia liliondoka huko Georgia Agosti 12 kwa upatanishi wa Rais wa Ufaransa, na Moscow ikayatambua rasmi kuwa huru maeneo mawili yaliyokuwa yakipigania kujitenga yaani Ossetia ya Kusini na Abkhazia.
Miaka 35 iliyopita mwafaka na tarehe 7 Agosti 1982, Marekani, Lebanon na Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) zilisaini makubaliano ya kuwaondoa wapiganaji wa harakati hiyo huko Beirut mji mkuu wa Lebanon. Makubaliano hayo yalisainiwa kufuatia mashambulio makubwa yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Lebanon tangu mwezi Juni 1982. Lengo la mashambulizi hayo lilikuwa kuwaangamiza au kuwafukuza wanamapambano wa Palestina waliokuweko huko Lebanon. Jeshi la kibaguzi la utawala wa Israel lilitumia silaha nyingi na za kisasa katika mashambulio hayo. Hatimaye Yasir Arafat kiongozi wa zamani wa harakati ya PLO alilazimika kuwaondoa huko Lebanon wanamapambano elfu 12 wa Kipalestina na kuwatuma katika nchi nyingine nane za Kiarabu.
Na siku kama hii ya leo miaka 57 iliyopita Ivory Coast ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wareno waliivamia Ivory Coast katika karne ya 16, na Ufaransa ikaifanya nchi hiyo kuwa koloni lake mwaka 1891. Hatimaye mwaka 1960, Ivory Coast na nchi nyingine kadhaa makoloni ya Ufaransa barani Afrika zikapata uhuru na kuasisi mfumo wa Jamhuri.