Aug 13, 2017 02:19 UTC
  • Jumapili, 13 Agosti,, 2017

Leo ni Jumapili tarehe 20 Dhul-Qaadah mwaka 1438 Hijria, sawa na tarehe 13 Agosti, 2017.

Siku kama ya leo miaka 982 iliyopita, alifariki dunia malenga, mwanafasihi na mhakiki wa Morocco, Abu Ali Qirwani. Alizaliwa nchini Morocco mwaka 390 Hijria na kuanza kujifunza mashairi, fasihi na elimu nyengine za wakati huo. Baada ya hapo Ali Qirwani alifunga safari na kuelekea mji wa Kirwan unaopatikana Tunisia kwa minajili ya kushiriki majlisi za kielimu za wasomi wakubwa wa zama hizo. Katika kipindi hicho mji wa Kirwan ulikuwa kitovu cha utamaduni wa Kiislamu katika nchi za kaskazini mwa Afrika na Andulusia na wasomi wengi wa Kiislamu, maulamaa na wataalamu wa fasihi walitoka katika mji huo.

Abu Ali Qirwani.

Siku kama ya leo miaka 199 iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilianza shughuli zake chini ya usimamizi wa Mirza Abul-Hassan Shirazi. Kabla ya hapo kulikuwepo taasisi iliyokuwa inaitwa ‘Taasisi ya Masuala ya Kigeni’ ambayo ndio iliyokuwa ikishughulikia mahusiano ya kigeni. Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilikuwa wizara ya kwanza nchini Iran na baadaya kulianzishwa wizara nyengine chini ya usimamizi wa Waziri Mkuu. Mwaka 1299 Hijria kuliandikwa kanuni zinazohusiana na masuala ya kigeni yaliyotakiwa kufuatiliwa na wizara hiyo. Hii leo Wizara ya Mambo ya Nje ni miongoni mwa wizara zenye utendeji mkubwa na muhimu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mirza Abul-Hassan Shirazi, waziri mkuu wa kwanza wa Iran

Siku kama ya leo miaka 154 iliyopita aliaga dunia Frederick Eugene Delacroix, mchoraji maarufu wa Ufaransa. Eugene Delacroix alirithi kipaji cha sanaa ya uchoraji kutoka kwa mama yake. Baada ya kupoteza wazazi wake wawili akiwa kijana mdogo na kujikuta akiishi maisha magumu sana ya umasikini, aliamua kufanya juhudi kubwa katika kujiendeleza na fani yake uchoraji. Baadaye alianza kufanya maonyesho ya sanaa hiyo katika ukumbi wa jiji la Paris. Katika kipindi hicho baadhi ya watu walikuwa wakimfanyia maskhara na kumkebehi, hata hivyo hakuvunjika moyo na hatimaye kazi zake zilikuwa na taathira. Alipata umashuhuri katika kipindi kifupi na kazi zake zikapokewa sana katika jamii.

Frederick Eugene Delacroix

Siku kama ya leo miaka 118, yaani tarehe 13 Agosti miaka 115 iliyopita, alizaliwa Alfred Hitchcock mtengeneza filamu mashuhuri wa Kiingereza. Alionesha kazi yake ya kwanza mwaka 1920 na baadaye akaanza kujihusisha na uongozaji filamu. Filamu zake za kuogopesha na za kusisimua zilikuwa mashuhuri mno katika zama hizo. Filamu hizo zilimfanya awe mashuhuri kwa jina la the Master of Suspense. Miongoni mwa filamu zake ni The Man Who Knew Too Much na Young and Innocent. Alfred Hitchcock aliaga dunia tarehe 28 Aprili 1980.

Alfred Hitchcock

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, aliaga dunia Florence Nightingale, mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa huko nchini Italia, akiwa na umri wa miaka 90. Nightingale alizaliwa tarehe 12 Mei 1820 nchini Italia. Aliishi kipindi kirefu cha ujana wake nchini Uingereza. Akiwa kijana alifanya juhudi kubwa katika kuwasaidia watu, suala ambalo alilipa umuhimu mkubwa kuliko kitu kingine chochote na hatimaye alisabilia maisha yake kwa amjili ya kuuguza wagonjwa. Bi, Florence Nightingale alikuwa muuguzi na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Alipewa lakabu ya ''Mwanamke Mwenye Taa Mkononi' kutokana na uvumilivu wake mkubwa na kujinyima usingizi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa nyakati za usiku. Alifanya juhudi kubwa pia kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali nyingi nchini Uingereza. Kazi hiyo aliyoifanya kwa miaka mingi bila kuchoka ilimdhoofisha sana kimwili kwa kadiri kwamba alikuwa kipofu mwishoni mwa umri wake na hatimaye aliaga dunia tarehe 13 Agosti 1910.

Florence Nightingale

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilijikomboa na kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Ilikuwa katikati ya karne ya 19 wakati nchi hiyo iliyokuwa ikijulikana hapo kabla kwa jina la Ubangi-Shari, ilipounganishwa na makoloni ya Ufaransa barani Afrika. Hata hivyo mwaka 1958, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilijipatia mamlaka ya ndani na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1960, ikajikomboa na kupata uhuru kamili.

Ramani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati

 

Tags