Aug 13, 2017 12:34 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 11 ya makala yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar.

Ukweli ni kwamba tangu muongo wa 1990 Miladia, serikali ya Myanmar ilijikita tu katika kutwaa kwa nguvu ardhi za wanavijiji hususan Waislamu wa kabila la Rohinya. Hata hivyo kama tulivyosema, hali hiyo ilishika kasi zaidi mwaka 2012 hasa baada ya kubadilishwa sheria ya umiliki wa ardhi ambayo ilizingatia maslahi ya serikali na wawekezaji wa kigeni. Ilikuwa ni tarehe 30 Machi mwaka 2012 ambapo wawakilishi wa mabunge yote  ya nchi hiyo walianza kuchunguza sheria za ardhi ambapo katika hilo walipasisha sheria hiyo ambayo ilipigilia msumari wa machungu kwa jamii ya Waislamu wa Rohingya. Ni baada ya hapo ndipo kukapasishwa sheria ya wawekezaji wa kigeni wanaowekeza ndani ya taifa hilo, sheria ambayo inatoa ruhusa kwa asilimia 100 kwa wawekezaji kumiliki ardhi hizo kwa kipindi cha miaka 70.

Mwaka huo huo wa 2012 kukatenguliwa sheria iliyopasishwa mwaka 1963 ambayo ilikuwa inawapa umiliki wa ardhi wanavijiji. Ni baada ya hapo ndipo kukashuhudiwa uhamishaji wa lazima wa mamilioni ya wakulima na wamiliki wa ardhi wa Myanmar ambapo awali iliwajumuisha pia Mabudha wa vijijini. Katika hilo hata baadhi ya Mabudha wa tabaka la chini walijikuta wakihamishwa kwa nguvu kutokana na kuanza kutekelezwa sheria mpya na serikali ya Burma. Mabadiliko ya sheria hizo hayakuihusu Myanmar pekee, bali mwenendo huo ulishuhudiwa pia katika nchi nyingine, hasa baada ya kuingia katika nchi hizo mashirika makubwa ya kilimo. Pamoja na hayo kunaibuka swali hili kwamba, je, ni vipi serikali iliweza kupasisha sheria ambayo inawapuuza raia wazalendo na kuwapa nafasi kubwa wawekezaji wa kigeni?

Aidha ni kwa nini Waislamu wa kabila la Rohingya waonekane kuwa wahanga wakuu wa sheria hizo mbapo hadi sasa uchunguzi unaonyesha kwamba asilimia kubwa ya ardhi zilizotwaliwa kwa nguvu ni za Waislamu hao wa Rohingya?

***********************************************

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni nchini Myanmar umeshika kasi zaidi katika sekta za uchimbaji madini, usambazaji wa maji na umeme. Kinyume chake uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta za uzalishaji ambao ulitarajiwa kuboresha hali ya wafanyakazi, haukuweza kufikia malengo hayo. Kwa mfano mradi wa ujenzi wa bomba la Yadana ambao unagharimu kiasi cha Dola bilioni moja za uwekezaji, utajengwa na wafanyakazi 800 tu. Aidha makamanda wa jeshi wa kieneo na makundi ya wabeba silaha ndio wanaonufaika na mauzo au ununuzi wa ardhi nyingi za kilimo eneo la kaskazini mwa Myanmar.

Uharibifu wa askari wa serikali ya Myanmar katika maeneo ya Waislamu

Ni katika mazingira hayo ndipo kukashuhudiwa matukio ya uvunjwaji wa haki za binaadamu na kadhalika ongezeko la wawekezaji wa kigeni nchini humo na kuanza kudhibitiwa ardhi za kilimo, kulikoenda sambamba na kuwanyang'anywa ardhi hizo wamiliki wake halali. Kwa mwenendo huo wakulima waneendelea kuwa masikini siku hadi siku, huku wengine wakilazimika kukabidhi mashamba yao kwa magenge vamizi, huku soko la ununuzi na uuzaji wa ardhi zisizo halali likaendelea kunawiri. Ni kwa msingi huo ndio maana wimbi la ukatili wa jinai dhidi ya jamii ya wachache wa Rohingya likawa la pande mbili. Upande wa kwanza unalenga kuwapokonya ardhi zao ili zitumike kwa ajili ya malengo ya kuwanufaisha mabwenyenye na viongozi wa ngazi ya juu wa serikali na upande mwingine ni kwamba jinai hizo zinasukumwa na chuki za kidini. Ukweli ni kwamba kuwaondoa kwa nguvu na kuwakandamiza Waislamu katika maeneo yao ya asili, kunatekelezwa kwa lengo la kuzitwaa ardhi zao. Uchomaji moto wa makazi yao, kwa shabaha ya kuwafanya Mwislamu hao wasiweze kurejea tena katika maeneo hayo.

*****************************

Katika hali kama hiyo serikali ya Myanmar haiko tayari kabisa kuheshimu misingi ya ubinaadamu na kukomesha jinai dhidi ya jamii ya watu hao.

Aung San Suu Kyi, ambaye chama chake ndio kinaongoza kwa sasa nchini humo

Aidha katika hatua nyingine ya kuwapora ardhi Waislamu wa Rohingya, baadhi ya viongozi wa serikali wakiwemo wabunge, walibuni njia ya kuanzisha vijiji vipya vya kikabila ambavyo vinaasisiwa katika maeneo yaliyotwaliwa kutoka mikononi mwa Waislamu. Katika hali hiyo, hivi karibuni wawakilishi wa bunge la Myanmar walitaka kujengwa vijiji zaidi vya kikabila kwa lengo la kuwakandamiza Waislamu wa jamii hiyo ya Rohingya ikiwa ni katika kuendelea kuangamizwa kizazi cha Waislamu hao huko Myanmar khususan katika mkoa wa Rakhine. Kama tulivyosema, aghalabu ya Waislamu wa Rohingya wanaishi katika mkoa huo unaopatikana magharibi mwa Myanmar na sambamba na kuwepo mkakati wa kuwafukuza kabisa Waslamu hao katika mkoa wa Rakhine, wabunge wa Myanmar walikiri kuwa tangu maelfu ya miaka nyuma, eneo hilo limekuwa makazi asilia ya Waislamu wa Rohingya tangu enzi za mababu huku likijulikana kwa jina la Aragan ambalo lilikuwa na utawala wa kifalme  kwa muda wa miaka mia tatu. Mashinikizo na ukatili huo rasmi dhidi ya Waislamu hao ulianza katika muongo wa sitini Miladia baada ya kuingia madarakani wanajeshi nchini humo na kisha mashinikizo hayo kuendelezwa kufutia vitisho na uchochezi wa watawala wa Kibudha wenye misimamo mikali kama Ashin Wirathu.

Kwa kadiri kwamba kuanzia mwaka 2012 Waislamu wa Rohingya zaidi ya elfu moja waliuawa na wengine zaidi ya laki moja kulazimishwa kuwa wakimbizi katika nchi jirani kutokana na ukandamizaji na mauaji ya umwagaji damu mkubwa yaliyofanywa na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada. Inaonekana kuwa, sasa utekelezaji wa mauaji au maangamizi ya kizazi ya Waislamu wa kabila la Rohingya umeshika mkondo mpya ambapo, viongozi wa serikali na wale wa kieneo wameazimia kuasisi vijiji vya kikabila ili kuwanyang'anya ardhi jamii hiyo. Kwa kuzingatia radiamali inayotolewa na jamii ya kimataifa kwa mauaji ya kizazi huko Myanmar na pia kuwahusu viongozi wa nchi hiyo khususan Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala cha National League for Democracy (NLD) ambaye pia ni mshauri wa ngazi ya juu wa serikali ya nchi hiyo, serikali ya Myanmar inadhani kwamba, kwa kuanzisha vijiji hivyo itaweza kuzihadaa fikra za walio wengi ambapo itawaalika waangalizi wa kimataifa na kuwafanya waamini kuwa, hakukuwahi kujiri ukandamizaji wala mauaji dhidi ya Waislamu katika maeneo hayo.

Siasa hizo zinafuatliliwa kwa jadi na kupewa kipaumbele cha awali na wabunge wa Myanmar ambao wengi ni kutoka chama cha National League for Democracy chini ya uongozi wa Bi Suu Kyi. Jenerali Than Htut Naibu Waziri Anayehusika na Masuala ya Mipaka wa Myanmar amesema kuwa vijiji 36 vya kikabila vimejengwa katika maeneo tofauti mkoani Rakhine na kwamba serikali ina mpango wa kuyahamisha makabila mbalimbali kutoka katika eneo la Yangon na kuyapeleka katika maeneo hayo lengo likiwa ni kuvuruga muundo wa kijamii wa mkoa wa Rakhine na hivyo kuwadhihirisha Waislamu wa Rohingya kuwa ni jamii ya waliowachache zaidi au kuwafanya kuwa wakimbizi.

Ardhi za Waislamu zikiwa zinatwaliwa kimabavu

Kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2016 hadi Februari mwaka huu maeneo ya Buthidaung na Mandau katika mkoa huo yamekumbwa na mashambulizi ya umwagaji damu ya Mabudha wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu wa Rohingya. 

*************************************

Kwa kuzingatia nafasi nzuri ya kijiografia ya mkoa wa Rakhine kwa upande wa hali ya hewa na ardhi ya kilimo na vile vile shughuli za kibishara, ni karibu miongo sita sasa ambapo Mabudha wenye misimamo mikali wameanzisha jitihada kubwa kwa kutumia mbinu mbalimbali za kiuongozi na kijeshi ili kupora na kumiliki ardhi, vituo vya kibiashara na kuwadhibiti Waislamu wa Rohingya, ambapo  lengo lao kuu ni kuwafukuza katika makazi na nyumba zao kwa kutekeleza mauaji ya kizazi dhidi ya jamii hiyo.

Waislamu wakilia kwa machungu kutokana na jinai wanazofanyiwa na serikali ya Burma

Pamoja na hayo yote, kusimama kidete na kuendesha muqawama Waislamu wa kabila la Rohingya mkabala na mashinikizo na ukandamizaji wa Mabudha wenye misimamo ya kuchupa mipaka huko Myanmar kumechelewesha utekelezaji siasa za kuangamiza kizazi dhidi ya jamii hiyo iliyodhulumika na hilo ndilo limewafanya watawala wa nchi hiyo wakimbilie kuasisi vijiji vya kikabila ambavyo hakuna matarajio kwamba vitaweza kufanikisha mkakati wao huo wa kuwafukuza Waislamu wa Rohingya katika ardhi zao asilia. 

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 11 ya makala haya yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, Was-Salaamu Alaykum Warahmatullahi wa Barakaatu…………./ 

 

 

 

 

Tags