Aug 13, 2017 12:53 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 12 na ya mwisho ya makala yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia namna ambavyo serikali ya Myanmar kwa muda sasa imekuwa ikitekeleza mpango wa kutwaa ardhi za Waislamu wa jamii ya Rohingya na kuzikabidhi kwa wawekezaji na viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya nchi hiyo. Kadhalika tuliashiria njama za serikali ya nchi hiyo za kuanzisha vijiji vipya katika maeneo ya Waislamu kwa lengo la kupotosha fikra za walio wengi duniani ili kuionyesha dunia kwamba Waislamu hawakuwa na nafasi katika eneo la Rakhine. Katika kipindi hiki cha mwisho tutazungumzia njama za serikali za kujaribu kuficha ukweli wa jinai zake kwa kuanzisha mazungumo bandia na makabila tofauti ya nchi hiyo, hivyo endeleeni kuwa nami hadi mwisho wa kipindi.

Makazi ya Waislamu yakiwa yameharibiwa na askari wa serikali

Ndugu wasikilizaji baada ya jinai na ukatili wa kutisha wa serikali na Mabudha wa Myanmar dhidi ya Waislamu kufichuliwa na kutangazwa duniani, hivi sasa viongozi wa nchi hiyo wamekuwa wakifanya njama mbalimbali kwa lengo la kujaribu kupotosha fikra za walimwengu juu ya kile kinachojiri nchini humo. Katika uwanja huo, viongozi hao wameanzisha kile walichokipa jina la 'mazungumzo ya amani nchini Myanmar' yanayohudhuriwa na wawakilishi wa makundi ya jamii za wachache wa nchi hiyo. Mazungumzo hayo yalianza kupitia tangazo la Aung San Suu Kyi, mshauri wa ngazi ya juu wa serikali na Waziri wa Mambo ya Nje wa Myanmar ambaye anadai kuwa, dhumuni la mazungumzo tajwa ni kuhitimisha mapigano katika maeneo tofauti ya nchi hiyo. Duru ya mwisho ya mazungumzo hayo ilihudhuriwa na wawakilishi kutoka karibu makundi 20 ambayo yamekuwa na mzozo na serikali ya Burma, ikiwa ni katika mwendelezo wa mazungumzo ambayo karibu mwaka mmoja uliopita yalifanyika chini ya usimamizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

**********************************

Licha ya mazungumzo hayo, hata hivyo mapigano baina ya jeshi la Myanmar na makundi ya jamii za wachache nchini humo hayajaweza kumalizika. Kwa mtazamo wa wawakilishi wa makundi ya kikaumu yaliyoshiriki mazungumzo ya amani na serikali ya Myanmar, ratiba ya Aung San Suu Kyi katika uwanja huo haiwezi kuhitimisha mgogoro huo.

Akari wa Myanmar wakielekea kufanya mashambulizi dhidi ya Waislamu 

Kwa mujibu wa wawakilishi hao, Suu Kyi ambaye anawakilisha serikali ya Myanmar katika mazungumzo, bado hajaupa umuhimu wowote wasi wasi yaliyonayo makundi hayo ya walio wachache kama ambavyo pia hajachukua hatua yoyote kwa ajili ya kukomesha mashambulizi ya jeshi la serikali dhidi ya Waislamu wa Rohingya. Hata hivyo suala linalofaa kuashiria hapa ni kwamba, mazungumzo hayo hayahusu namna ya kumaliza jinai na ukatili wa askari na Mabudha dhidi ya Waislamu, bali lengo la mazungumzo hayo ni kujadili tu njia za utatuzi wa makundi ya waasi ambayo yamekuwa yakipigana na serikali kutetea maslahi yao. Hii ni kwa kuwa, hadi sasa serikali ya Naypyidaw imekataa kuwatambua watu wa jamii ya Rohingya kuwa raia wa taifa hilo, na kwa msingi huo hakuna haja ya kufanya mazungumzo na asiyekuwa raia. Hii ni katika hali ambayo hata baadhi ya wawakilishi wa makundi ya upinzani wa serikali wanawataka viongozi wa nchi hiyo kuyajumuisha makundi yote ya kikabila nchini bila kufanya ubaguzi. Kuhusiana na suala hilo Sai Kyaq Nyunt, mwakilishi kutoka chama cha Shan National League for Democracy amenukuliwa akisema kuwa, ni suala gumu sana kufikiwa makubaliano, bila kuyashirikisha makundi yote ya nchi hiyo.

Waislamu hao wakiwa tayari wamezingirwa na askari hao watatili wakisubiria kuuawa kwa ukatili

Ni kutokana na hatua hizo za undumakuwili za serikali ndio maana weledi wa mambo wakaamini kuwa, serikali ya Myanmar inatumia mazungumzo hayo kama kiini macho cha kuzipotosha fikra za walio wengi kuhusiana na jinai inazozifanya dhidi ya jamii ya Waislamu, na wala haina nia yoyote ya kufanya mazungumzo yenye lengo la kuhitimisha jinai na ukatili wake huo.

***********************************

Katika kubainisha undumakuwili wa serikali ya Naypyidaw ni kwamba, wakati inadai kuitisha mazungumzo na wawakilishi wa makabila ya wachache nchini humo, bado hadi sasa haijatangaza kuwatambua watu wa jamii ya Rohingya ambao wamekuwepo kwa karne kadhaa jimbo la Rakhine kuliko makabila mengine, kuwa ni raia wa taifa hilo. Mbali na hayo, hadi sasa serikali ya Myanmar mbali na kukataa katakata suala la wakimbizi wa Rohingya walioko ughaibuni kurejea maeneo yao ya asili nchini Myanmar, imekataa pia kurejesha ardhi na mali za Waislamu hao zilizotwaliwa kwa nguvu na serikali. Mtakumbuka katika vipindi vilivyopita tulisema kuwa, katika kuendeleza ukatili na ukandamizaji dhidi ya Waislamu, serikali ya Burma sambamba na kutangaza kutowatambua watu wa jamii hiyo kuwa ni raia wa Myanmar, ilifunga akaunti za fedha za watu wa jamii hiyo, huku nyumba, fedha na vitu vingine vya thamani vikifilisiwa.

Aung San Suu Kyi, Mshauri wa serikali ya nchi hiyo aliyetangaza kutowatambua Waislamu

Aidha wakati Aung San Suu Kyi akiitisha mazungumzo hayo, hadi sasa mamia ya watoto wadogo wa jamii ya Rohingya bado wanazuiliwa na vyombo vya usalama chini ya mazingira magumu katika jimbo la Rakhine. Ni kutokana na suala hilo ndipo Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF hivi karibuni ukaitaka serikali ya Myanmar kuwaachilia huru watoto hao bila ya masharti yoyote. Justin Forsyth, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF alitoa pendekezo hilo mara baada ya kuitembelea nchi hiyo na kubainisha kuwa, mamia ya watoto wadogo wa kabila la Rohingya wanazuiliwa katika gereza la Buthidaung jimboni Rakhine. Forsyth alisisitiza kuwa, iwapo hatua za kuipatia ufumbuzi kadhia ya Waislamu wa Myanmar hazitachukuliwa haraka, basi zimwi la jinai kuwalenga Waislamu walio wachache katika jimbo la Rakhine litaendelea kushuhudiwa siku hadi siku. Katika hali kama hiyo, ni kivipi serikali itangaze kuwa na nia ya kufanya mazungumzo katika hali ambayo bado inaendelea kukiuka wazi wazi haki za jamii ya Waislamu walio wachache nchini humo? Aidha miongoni mwa jinai ambazo zimeendelea kufanywa na serikali ya Myanmar licha ya kutangaza kutaka kufanya mazungumzo na jamii za wachache, ni ubomoaji wa maeneo ya ibada ya Waislamu nchini humo. Kuhusiana na suala hilo, jeshi la Myanmar limekuwa likibomoa na kuharibu kikamilifu misikiti ya kihistoria ya Waislamu wa Rakhine.

Msikiti ukiwa umebomolewa na askari hao wakatili

Mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, vyombo vya habari viliripoti habari ya kubomolewa msikiti wa karne kadhaa katika kijiji cha Lawei Dek, katika mji wa Buthidaung katika jimbo hilo lenye Waislamu wengi la Rakhine magharibi mwa Myanmar. Huo haukuwa msikiti wa kwanza kubomolewa na askari wa serikali. Baadhi ya duru za habari zinaeleza kuwa, askari na Mabudha wamekuwa wakihujumu misikiti tofauti nchini humo huku mingine ikifungwa na kuwazuia Waislamu kuweza kutekeleza ibada zao ndani yake. Kiujumla tunaweza kusema kuwa, jamii ya Waislamu nchini Myanmar haina haki yoyote ya msingi.

Katika kumalizia kipindi hiki, tunaashiria wajibu na majukumu ya Waislamu kwa ajili ya kuwasaidia Waislamu wenzao wa Myanmar. Ndugu wasikilizaji, katika hali ambayo watawala wa nchi nyingi za Kiiaslamu hususan za Kiarabu wamejikita tu katika kulinda na kuwania madaraka kiasi hata cha kuwakandamiza raia wao wenyewe, hawawezi kukumbuka na kulipa umuhimu suala la Waislamu wanaodhulumiwa wa Myanmar au nchi nyingine kama vile Palestina na kadhalika. Hakuna shaka kwamba udhaifu huo wa Waarabu ndio umewapa kiburi viongozi wa Myanmar kuendeleza jinai zao kuwalenga Waislamu, na hii ni kusema kuwa, wakati watawala hao wanaishia tu kutoa matamshi yasiyokuwa na maana ya kulaani jinai hizo, wakati huo huo wanafanya mahusiano na urafiki mkubwa na viongozi wa Marekani ambao wanajulikana kwa kuwapa ulinzi na kuwaunga mkono viongozi wa serikali ya Burma.

Msikiti ukiwa unateketezwa kwa moto 

Katika hali hiyo hakuwezi kushuhudiwa uafadhali wowote wa kukomeshwa jinai na dhulma zinazowakabili Waislamu wa nchi hiyo. Hata hivyo kama ilivyo katika kuwatetea watu wote wanaodhulumiwa duniani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku zote imekuwa mstari wa mbele katika kufuatilia na kuwasaidia Waislamu wa nchini Myanmar. Tangu awali nchi ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kuakisi jinai za serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu,  ni Iran ambapo vyombo vyake vya habari vimelipa umuhimu mkubwa suala la Waislamu wa Rohingya na dhulma wanazofanyiwa. Katika uwanja huo, mara baada ya kuteuliwa Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres,  Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifanya mazungumzo na kiongozi huyo wa UN na kumfikishia kilio cha taifa la Iran na Waislamu wa dunia juu ya hali mbaya waliyonayo Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar. Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika pembezoni nwa Mkutano wa Usalama wa mjini Munich nchini Ujerumani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliutaka umoja huo uchukue hatua za haraka katika kutatua migogoro inayowakabili Waislamu Warohingya pamoja na Waislamu wa Yemen, Syria na Iraq.

Ukatili na ukandamizaji wa kuchupa mipaka ukiendelea dhidi ya Waislamu

Kadhalika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitoa mwito kwa nchi zote za Kiislamu kushirikiana na kuishinikiza serikali ya Burma kuheshimu haki za Waislamu wa nchi hiyo sambamba na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wahusika wa jinai dhidi ya Waislamu.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 12 na ya mwisho ya makala haya yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

 

Tags