Aug 28, 2017 02:17 UTC
  • Jumatatu, 28 Agosti, mwaka 2017

Leo ni Jumatatu tarehe sita Mfunguo Tatu Dhul-Hijja mwaka 1438 Hijria, mwafaka na tarehe 28 Agosti, mwaka 2017.

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, mamia ya mahujaji wa Iran na wengine kutoka nchi tofauti waliokuwa wameenda kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu mjini Makka na wakiwa katika hali ya kutekeleza ibada ya faradhi ya kujitenga na mushrikina, waliuawa shahidi na vibaraka wa utawala wa Saudi Arabia. Ni vyema kukumbusha kuwa, mahujaji wa Iran kwa miaka yote huwa wanatekeleza ibada hiyo kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo mbali na kuwasisitizia Waislamu kuungana, hutangaza kujitenga na maadui wa Uislamu hususan Marekani na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Kwa hakika ibada hiyo ambayo hufanyika kwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, huwa na taathira kubwa katika msimu wa hija. Ni kwa ajili hiyo, ndio maana Imam Khomein Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akasisitizia sana umuhimu wa ibada ya kujitenga na mushrikina na maadui wa dini ya Kiislamu.

mamia ya mahujaji waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi ya Saudia

Miaka 24 iliyopita katika siku kama ya leo, Yasir Arafat kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na Yitzhak Rabin Waziri Mkuu wa wakati huo wa utawala haramu wa Israel walisaini mkataba wa mapatano kwa jina la "Makubaliano ya Ghaza-Jericho" huko Washington, Marekani. Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na utawala wa Kizayuni zilitambuana rasmi katika makubaliano hayo yaliyosainiwa miaka miwili baada ya kuanza mazungumzo eti ya amani kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni.

Arafat, Clinton na Yitzhak Rabin

Siku kama hii ya leo miaka 54 iliyopita yaani Agosti 28, 1963, Martin Luther King mwanaharakati mkubwa wa kutetea haki za Wamarekani weusi nchini Marekani, alihutubia umati mkubwa wa watu waliofanya mgomo wa kutaka wapewe haki ya kijamii nchini humo. Luther King ambaye ni Mmarekani mweusi alihutubia umati huo kwenye uwanja wa kumbukumbu wa Lincoln mjini Washington. Kwenye mkutano huo, Martin Luther King alieleza ndoto yake ya kuwa huru Wamarekani weusi.

Tarehe 28 Agosti 1749 alizaliwa Johann Wolfgang Von Goethe malenga na mwandishi mkubwa wa Kijerumani. Von Goethe alisoma na kujifunza mambo mbalimbali kama uchoraji na kadhalika katika mji aliozaliwa wa Frankfurt nchini Ujerumani, huku akiendelea na masomo yake ya taaluma ya sheria. Von Goethe ambaye anahesabiwa kuwa mmoja kati ya waenezaji wa fasihi ya lugha ya Kifarsi, alivutiwa mno na fasihi ya Kifarsi na hasa mashairi ya Hafidh, malenga na mshairi mashuhuri wa Kiirani. Mwandishi huyo wa Kijerumani alikipenda sana Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani pamoja na dini ya Kiislamu. Johann Wolfgang Von Goethe alifariki dunia mwaka 1832.

Johann Wolfgang Von Goethe

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita kombora la kwanza la kuvuka mabara lilirushwa hewani na wasomi wa Urusi ya zamani. Siku nne baadaye yaani tarehe 4 Oktoba wasomi wa Urusi walirusha angani satalaiti ya kwanza dunia iliyopewa jina la Sputnik 1 kwa kutumia kombora hilo. Hatua hiyo ilipongezwa kote dunia na wasomi hao walitangaza kuwa watatuma mwanadamu angani katika kipindi cha chini ya miaka mitatu na kwamba watatuma chombo cha anga katika mwezi miaka mitano baadaye. Wasomi hao wa Urusi walitimiza hadi zao. 

Kombora la Russia

Na siku kama ya leo miaka 1180 iliyopita, yaani sawa na tarehe 6 Dhul-Hijjah mwaka 258 Hijiria, alizaliwa Abu Ali Muhammad ibn Hammam, mmoja wa maulama mashuhuri wa Iran. Ibn Hammam alikuwa akiishi mjini Baghdad, Iraq ambapo alifanikiwa kusoma elimu ya hadithi kutoka kwa maulama wakubwa wa enzi zake. Msomi huyo pia alikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao walijifunza kwake elimu ya hadithi na elimu nyingine za Kiislamu. Msomi huyo ameacha vitabu kadhaa katika uga wa hadithi.

 

Tags