Dec 12, 2017 02:34 UTC
  • Jumanne tarehe 12 Disemba, 2017

Leo ni Jumanne tarehe 23 Rabiul Awwal 1439 Hijria sawa na tarehe 12 Disemba, 2017.

Miaka 116 iliyopita katika siku kama ya leo, kulianza ukurasa mpya katika historia ya mawasiliano ya mwanadamu baada ya kuzinduliwa mawasiliano ya njia ya mawimbi ya redio bila ya kutumiwa nyaya. Tukio hilo lilifanyika kwa kuwasiliana kwa maneno kutoka eneo moja la Italia kwenda jingine. Mtu aliyetumia mawasiliano ya aina hiyo kwa mara ya kwanza alikuwa mwanafizikia wa Italia Marconi ambaye baadaye alivumbua pia redio. Hii leo vyombo vya mawasiliano vinavyotumia mawimbi ya redio vinatumiwa katika masuala mengi duniani.

Marconi

Tarehe 12 Disemba 1963, yaani miaka 54 iliyopita, Kenya ilifanikiwa kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kenya ilianza kuvamiwa na Waingereza mwanzoni mwa karne ya 20 na mwaka 1920 ikakoloniwa rasmi na mkoloni huyo. Sambamba na kukoloniwa rasmi nchini hiyo, Jomo Kenyata aliongoza harakati za kupigania uhuru dhidi ya Uingereza. Hatua ya wazungu hao wakoloni ya kuhodhi madaraka ya nchi na mivutano ya ndani vilikaribia kuitumbukiza Kenya katika mapigano ya ndani katika muongo wa 1950. Baada ya kupamba moto wimbi la kupigania uhuru la wazalendo wa Kenya, kulipasishwa katiba ambayo ilidhamini usawa wa watu wa rangi zote nchi humo. Nchi hiyo ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza tarehe 12 Disemba 1963 chini ya uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta na siku hii inajulikana kwa jina la Jamhuri Day au Siku ya Jamhuri.

Bendera ya Kenya

Tarehe 23 Rabiul Awwal miaka 29 iliyopita aliaga dunia alimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Ayatullah Mirza Jawad Agha Tehrani. Msomi huyo wa Kiislamu alizaliwa mwaka 1322 Hijria katika familia ya kidini mjini Tehran na akapata elimu katika vyuo vya kidini vya Qum, Iran na Najaf huko Iraq. Miongoni mwa sifa kubwa zaidi za mwanazuoni huyo ilikuwa zuhudi, ucha-Mungu na kuwapenda sana Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni Kanuni za Maisha na Mizanul Matalib.

Ayatullah Mirza Jawad Agha Tehrani