Ulimwengu wa Spoti, Jan 8
Hujambo mpenzi msikilizaji na karibu tuangazie matukio mawili matatu ya spoti yaliyogonga vichwa vya habari ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa. Tuandamane sote hadi tamati ya kipindi……Karibu…….
Handiboli, Iran yakubali kushindwa na Slovenia
Timu ya taifa ya handiboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekubali kushindwa na Slovenia katika mchuano wa kirafiki uliopigwa katika mji wa Ljubljanan siku ya Alkhamisi. Iran ililemewa na mwenyeji Slovenia kwa kuzabwa magoli 31-19. Wiki iliyopita, Iran ilifanikiwa kuigaragaraza Slovenia katika mchuano wa kirafiki licha ya kuupigia ugenini. Iran imeizaba Slovania alama 33-32 katika mchuano wa kujiandaa Mashindano ya Mabingwa wa Handiboli ya Asia mwaka huu 2018 nchini Korea Kusini. Timu hiyo ya mpira wa mikono ya Iran iliekea Slovania kwa ajili ya kujitutumua misulu ikisubiri mashindano hayo ya kimataifa yanayofahamika kwa Kimombo kama Asian Men's Handball Championship yang'oe nanga baadaye mwezi huu. Iran ipo katika Kundi A pamoja na Iraq na Japan, huku Kundi B likizijumuisha Australia, Bahrain, Oman na Uzbekistan. Mwenyeji Korea Kusini ipo katika Kundi C pamoja na Bangladesh, Imarati na India huku Kundi D likizileta pamoja China, New Zealand, Qatar na Saudi Arabia. Duru ya 18 ya mashindano hayo ya kikanda itapigwa mjini Suwon, huko Korea Kusini kati ya Januari 18 na 28, na mabingwa wataliwakilisha bara Asia katika mashindano ya dunia mwaka ujao 2019.
Salah wa Misri, mchezaji bora wa soka barani Afrika
Mchezaji nyota wa timu ya taifa ya soka ya Misri, anayecheza soka la kulipwa nchini Uingereza katika klabu ya Liverpool Mohamed Salah, ndiye mchezaji bora barani Afrika kwa mwaka wa 2017. Salah mwenye umri wa miaka 25, aliwashinda wenzake Pierre-Emerick Aubameyang kutoka Gabon anayechezea klabu ya Borussia Dortmund pamoja na Sadio Mane kutoka Senegal lakini pia mchezaji wa Liverpool nchini Uingereza katika tuzo hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la soka barani Afrika (CAF). Mchezaji huyo wa Misri, alishinda taji hilo kutokana na mchango wake katika klabu ya Liverpool, ambako amefunga mabao 17 hadi sasa lakini pia aliisadia timu yake kufuzu katika michuano ya kombe la dunia itakayofanyika mwezi Juni mwaka huu nchini Urusi.
Taji la mwanamke bora, lilimwendea Mnigeria Asisat Oshoala anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Dalian Quanjian nchini China, huku tuzo ya mwanasoka chipukizi ajaye kwa kasi ikimuendea Patson Daka raia wa Zambia. Mafanikio ya Mohamed Salah mapema msimu huu akiwa Liverpool yameifanya Real Madrid kuvutiwa naye. Vijana wa Zinedine Zidane wameshindwa kufanya maajabu mbele ya goli na wanatafuta utatuzi wa tatizo hilo, mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri anapewa nafasi kubwa kutua Bernabeu. Madrid wanatambua kuwa kukamilika kwa dili hilo kwa uhamisho wa Januari ni vigumu kwa hiyo wanajipanga kwa ajili ya majira ya joto.
Kombe la Mapinduzi
Klabu ya soka ya Azam ya Tanzania Bara imetinga nusu fainali katika michuano inayoendelea huko Visiwani Zanzibar ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kuisasambua klabu ya Simba. Azam waliichapa Simba bao 1-0 lililofungwa na Idd Kipagwile katika dakika ya 59.
Kocha msaidizi wa kikosi hicho Idd Suleiman Cheche amesema siri ya ushindi katika mchezo huo ni kujituma na umoja wa wachezaji wake. Azam inakuwa timu ya tatu kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ambayo ilianza Disemba 29 mwaka jana, ambapo timu nyingine ni Yanga na Singida United zote kutoka Kundi B. Fainali ya michuano hiyo itafanyika Jumamosi ya Januari 13 mwaka huu. Ikumbukwe kuwa Azam FC ndio mabingwa watetezi waliochukua kombe hilo mwaka jana kwa kuifunga Simba bao 1-0. Ili kufufua matumaini ya kusonga mbele, Simba hawana budi kuwangurumia watoza ushuru wa URA wa Uganda. Januari 2, mabingwa wa kihistoria wa Kombe la Mapinduzi, Simba, walianza vibaya mashindano hayo baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mwenge kwenye Uwanja wa Amaan. Simba waliandika bao la kwanza kupitia kwa Jamal Mwambeleko baada ya mpira wa krosi wa Mohamed Hussein katika dakika ya pili tangu kuanza kwa mchezo huo. Katika dakika ya 28, Mwenge walipata bao la kusawazisha lililofungwa na Humudu Abdurahman Ali baada ya kupiga shuti katikati ya mabeki wa Simba na mpira kujaa wavuni.
Coutinho kuwa mchezaji wa pili mwenye thamani kubwa zaidi
Klabu ya Barcelona imetangaza habari ya kukakamilisha usajili wa Philippe Coutinho kwa mkataba wa miaka mitano kutoka Liverpool. Miamba hao wa La Liga walimkosa Mbrazili huyo kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya joto licha ya kutoa ofa tatu nono, lakini baada ya tetesi za muda mrefu hatimaye wamefanikiwa kuipata saini yake kwa dau linalokadiriwa kuwa pauni milioni 142 hadi 145. Liverpool wamethibitisha kuwa wamefikia makubaliano na Barcelona kumuuza mchezaji huyo wa miaka 25, kutua Camp Nou.
Coutinho amefunga magoli 54 katika mechi 201 katika kipindi chake cha miaka mitano Liverpool, baada ya kujiunga na klabu hiyo akitokea Inter Milan kwa kiasi cha pauni milioni 8.5 tu mwaka 2013. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazili anakuwa mchezaji soka wa pili mwenye thamani kubwa zaidi nyuma ya Neymar aliyejiunga na PSG ya Ufaransa hivi karibuni. Klabu itakayotaka kumnunua Coutinho italazimika kutoa kitita cha pauni milioni 355, sawa na yuro milioni 400 hivi. Ripoti zimedai kuwa bosi wa Liverpool Jurgen Klopp yumkini akamleta Thomas Lemar kutoka Monaco kuziba pengo la Coutinho, au pia Riyadh Mahrez, mshambuliaji wa Leicester City raia wa Algeria.
…………………………TAMATI…………………..