Aya na Hadithi (1)
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.
Karibuni kusikiliza kipindi cha kwanza katika mfululizo wa vipindi hivi vipya ambavyo vitakuwa vikizungumzia Aya za Quráni Tukufu na Hadithi za Watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (saw). Lengo la vipindi hivi wapenzi wasikilizaji ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kupata kujua baadhi ya Aya za Quráni Tukufu ambazo zina sifa maalumu na tukufu katika maisha ya mwanadamu na kulinda harakati na mwenendo wake katika njia bora na iliyo nyooka. Aya hizi zitakuwa zikibainishwa na kufafanuliwa zaidi na Hadithi ambazo zimepokelewa kutoka wa watukufu wa Nyumba ya Mtume (saw) na ambazo zimenukuliwa katika vitabu vya Hadithi vya kuaminika. Kama tulivyoashiria katika vipindi vilivyopita vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain, Ahlul Beit wa Mtume ndio Kizito cha Pili tulichoachiwa na mtukufu huyo ambacho alisema kuwa hakitatengana na Kizito cha Kwanza yaani Quráni Tukufu hadi vitakapokutana naye vyote viwili kwenye Hodhi, Siku ya Kiama.

Tunaanza kulijadili suala hili kwa kutupia jicho aya ya kwanza ambayo ilisifiwa na Mtume (saw) kuwa ni ‘Bwana wa Aya za Quráni’, na ambayo si nyingine bali ni Aya mashuhuri ya al-Kursiy. Hii ni aya ya 255 ya Surat al-Baqarah. Maulama wanasema kuwa ubora wa athari za Aya hii unakamilika kwa kuiunganisha na aya nyingine mbili za 256 na 257 za Sura hiyohiyo kama anavyoashiria suala hilo Allama Tabatabai katika Tafsir yake ya al-Mizaan.
Kabla ya kuendelea hebu tukimye kidogo na kusikiliza kwa makini Aya hizo:
Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye Aliye hai, Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na kusinzia wala kulala. Ni vyake pekee vyote vilivyomo mbinguni na ardhini. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilivyo katika ujuzi wake, ila kwa alitakalo mwenyewe. Enzi yake imetanda mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye Mtukufu aliye Mkuu. Hakuna kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anayemkataa taghuti na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisichovunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. Mwenyezi Mungu ni mtawala wa walioamini. Huwatoa gizani na kuwaingiza mwangazani. Lakini waliokufuru, watawala wao ni mataghuti. Huwatoa kwenye mwangaza na kuwaingiza gizani. Hao ndio watu wa Motoni, na humo watadumu.
Kama mnavyoona wapenzi wasikilizaji Aya hizi tatu zinajumuisha nguzo zote za Tauhidi halisi tokea Uungu mutlaki hadi kweye Umola wa Mwenyezi Mungu ambao huwaondoa waumini kutoka gizani hadi kwenye mwangaza. Ni kwa msingi huo ndipo usomaji wa Aya hizi na kuzifanyia kazi ni katika njia bora zaidi za kuimarisha imani na mawasiliano na Mwenyezi Mungu pamoja na kuingia kwenye ngome yake iliyo madhubuti. Hii ndio sababu zikachukuliwa kuwa miongoni mwa akiba ya thamani muhimu na kutengewa mahsusi Umma wa Muhammad ambao ni mwaminifu katika imani yake kwa Mwenyezi Mungu, Mtume na mawasii wake (saw). Hebu sasa na tusikilize kwa pamoja Hadithi Tukufu ifuatayo ambayo imenukuliwa na Sheikh Tusi (MA) katika kitabu chake cha al-Aamali ambapo Abu Umamah al-Bahili amenukuliwa akisema kuwa alimsikia Imam Ali bin Abu Talib (as) akisema kwamba hakuna mtu anayeufahamu vyema Uislamu au kuzaliwa katika Uislamu anayelala usiku wake wote bila ya kusoma Ayat al-Kursiy. Kisha (as) alisoma Aya nzima ya Kursiy na kusema: ‘’Kama mngeliijua – au alisema: kama mngelijua kilichoma ndani yake – basi msingeiacha kwa hali yoyote ile. Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) aliniambia: ‘Nilipewa Aya ya Kursiy kutoka kwenye hazina iliyo chini ya Arshi na wala hakupewa Nabii yoyote aliyenitangulia.’’ Ali (as) akasema: ‘’Tokea wakati niliposikia kauli hiyo kutoka kwa Mtume (saw) sikuwahi kulala hata usiku mmoja bila kuisoma Aya hii.” Kisha akasema: ‘’Ewe Abu Umamah! Mimi huisoma mara tatu katika nyakati tatu tofauti kila usiku.’’ Nikasema: Ewe mwana wa Ami ya Mtume (saw)! Wewe huisoma vipi (wakati gani)? Akasema mimi huisoma kabla ya rakaa mbili baada ya kuswali swala ya Ishaa ya mwisho. Wallahi! Sijawahi kuacha kuisoma tokea niliposikia habari hiyo kutoka kwa Mtume wenu (as) na hadi sasa ambapo ninakwambieni.”

Ndugu wasikilizaji, mwishoni mwa Hadithi hii kuna nukta ya kuvutia sana kutokana na athari waliyoipata wapokezi wa Hadithi hii ya Mtume (saw) kupitia kwa wasii wake Imam Ali (as). Wote waliizingatia na kuifanyia kazi kivitendo. Abu Umamah anaapa mwishoni mwa Hadithi hiyo aliyowahadithia watu wengine kwamba hakuacha kuisoma Aya hiyo tokea alipoisikia kutoka kwa Imam Ali (as) hadi wakati alipowajulisha wenzake.
Naye Qassim alisema: ‘’Na mimi pia sikuacha kuisoma Aya hii kila usiku tokea aliponifahamisha fadhila zake Abu Umamah hadi leo.’’
Ali bin Yazid anasema: ‘’Na ninakujulisha ya kwamba sikuwahi kuacha kuisoma kila usiku tokea aliponifahamisha fadhila zake Qassim.’’
Ibn Abu al-Atikah anasema: ‘’Sikuwahi kamwe kuacha kuisoma kila usiku tokea yaliponifikia yaliyonifikia kuhusiana na fadhila zake.’’
Ibn Shabur anasema: ‘’Na mimi pia sikuwahi kuacha kuisoma kila usiku tokea iliponifikia kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kuhusiana na fadhila za kuisoma.”
Ibrahim bin Amru bin Bakr anasema: ‘’Na mimi pia sikuwahi kuacha kuisoma tokea iliponifikia Hadithi hii ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw).’’
Abu Muhammad Abdallah bin Abi Sufyan anasema: ‘’Na mimi pia sikuwahi kuacha kuisoma tokea nilipoandika Hadithi hii kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kuhusu fadhila za kuisoma.”
Na Abu al-Fadhl anasema: ‘’Na mimi kwa neema ya Mola wangu sikuwahi kuacha kuisoma tokea niliposikia Hadithi hii kutoka kwa Abdallah bin Abi Sufyan kutoka kwa Nabii (saw) hadi nilipokuhadithieni.’’
Tunamwomba Mwenyezi Mungu atupe taufiki ya kuweza kufanya kama walivyofanya wapokezi hawa wema wa Hadithi hii tukufu ya Mtume (saw), taufiki ya kusoma kila siku Aya ya Kursiy ili kwa kufanya hivyo tuweze kuwa tumetekeleza nasaha za Mtume wetu Mtukufu (saw) pamoja na za mrithi na wasii wake Ali al-Murtadha (as).
Huenda uzingatiaji wetu wa jambo hili, yaani kusoma kila siku Aya ya Kurisy na kuzingatia maana yake ukaimarika zaidi tutakaposoma Hadithi nyingine ambazo zinaashiria athari muhimu zinazotokana na usomaji wa Aya hii. Hii ndiyo itakayokuwa maudhui ya kipindi chetu cha juma lijalo cha Aya na Hadithi Inshallah. Basi hadi tutakapokutana tena wakati huo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kusema Wassalaam Aleikum Warhmatullahi Wabarakatuh.