Aya na Hadithi (7)
Assalaam Aeikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 7 ya kipindi hiki cha Aya na Hadithi ambacho huchambua Aya tofauti za Qur'ani na kisha kuzifafanua kwa Hadithi za Mtume na Maimamu Watoharifu wa Nyumba ya Mtume (saw). Karibuni.
Wapenzi wasikilizaji, kuna Aya za Qur'ani ambazo zinasema wazi kwamba Mwenyezi Mungu kutokana na rehemu kubwa aliyonayo kwa waja wake, aliteremsha kwenye Qur'ani hiyo wongofu na shufaa (ponyo). Hivyo tutazifahamu vipi Aya hizo na je, kuna mifano yoyote inayothibitisha wongofu na ponyo hilo la Qur'ani?
Ili kupata jibu la swali hili hebu kwanza tusikilize kwa makini Aya hizo Tukufu ambazo kwa utaratibu ni Aya ya 57 ya Surat Yunus, Aya ya 82 ya Surat al-Israa na Aya ya 44 ya Surat al-Fuswilat. Zinasema: Enyi watu! Hakika yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu, na ponyo la yale yaliyomo vifuani mwenu na mwongozo na rehema kwa waumini. Na tunateremsha katika Qur'ani ambayo ni ponyo na rehema kwa waumini. Wala haiwazidishii madhalimu ila khasara. Na lau tungeliifanya Qur'ani kwa lugha ya kigeni wangelisema: Kwa nini Aya zake hazikupambanuliwa? Yawaje lugha ya kigeni na Mwarabu? Sema: Hii Qur'ani ni uwongofu na ponyo kwa wenye kuamini. Na wasioamini umo uziwi katika masikio yao, nayo kwao imezibwa hawaioni. Hao wanaitwa nao wako pahala mbali.
Wapenzi wasikilizaji, kama mnavyoona, Aya hizi Tukufu zinabainisha wazi kwamba Qur'ani ni chanzo cha wongofu na ponyo au poza, bila kushurutisha jambo hilo na suala jingine lolote. Hii ina maana kwamba Qur'ani inaongoza kwenye haki na kuponya kila magonjwa yawe ni ya kimaanawi au ya kiroho ambayo hueda matabibu wote wakawa wameshindwa kuyaponya. Sharti la kufikiwa wongofu na ponyo hilo la Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni kuwa na imani na hiyo ndio maana ya kutengewa waumini rehema hiyo na kusisitizwa kwamba madhalimu hawapati ila hasara.

Ndugu wasikilizaji tumefikia hakika hii kutokana na Hadithi Tukufu ambazo kwanza zinasisitiza kwamba Qur'ani Tukufu ndio chanzo cha ponyo la maradhi ya kimaanawi yaliyomo kwenye vifua vya waumini kama ilivyotumika katika ibara ya Qur'ani katika Aya tuliyosoma ya Surat Yunus, na pili ni kuwa zinasisitiza kwamba Qur'ani ni ponyo la magonjwa yote yakiwemo yale ya kinafsi (kiroho) na kimwili. Tunaona kutoshurutishwa kwa jambo hili na kitu kingine chohcote katika Hadithi ya Mtume (saw) ambayo imenukuliwa katika kitabu cha Kanz al-Ummal ambapo Mtukufu Mtume amesema: 'Qur'ani ndiyo dawa.'
Kauli hii inafanana na ya Ameer al-Mu'mineen Ali (as) ambayo imenukuliwa katika hotuba yake ya 157 katika kitabu cha Nahjul Balagha ambapo anasema: "Na shikamaneni na Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa kuwa ni kamba iliyo madhubuti, nuru inayobainisha na Shifaa (dawa/ponyo) inayonufaisha (inayofaa).''
************
Hadithi Tukufu zimeyapa magonjwa ya kimaanawi umuhimu wa kwanza kwa kuwataka waumini wanufaike na ponyo la Qur'ani katika kutibu maradhi yaliyomo vifuani huku zikiashiria mifano ya wazi ya maradhi hayo. Kuhusu suala hilo Imam Ali (as) amenukuliwa akisifu Qur'ani Tukufu katika hotuba yake ya 176 ya Nuhjul Balagha kwa kusema: 'Hakika humo mna shifaa (tiba/ponyo) ya magonjwa makubwa zaidi nayo ni kufuru, unafiki, maasi na upotovu.'
Na katika vitabu vya al-Bihar na al-Kafi imenukuliwa Hadithi kutoka kwa mjukuu wa kwanza wa Mtume Muhammad (saw) al-Imam al-Hassan al-Mujtaba (as) akisema: 'Hakika kwenye hii Qur'ani mna taa za nuru na shifaa ya vifua. Hivyo basi anayetembea na aangaze moyo wake kwa nuru yake (ya Qur'ani) na kufungamanisha moyo wake na sifa zake (za Qur'ani), kwa sababu kutadabari (kufikiria/kuzingatia Qur'ani kwa makini) ndio uhai wa moyo wa mtu aliye na mwamko kama anavyotembea kwenye giza mtu aliye na nuru.

Kwa kuzingatia suala hili wasikilizaji wapenzi, Ahlul Beit wa Mtume Mtukufu (as) wamezingatia na kuwadhaminia waumini dua na Aya za Qur'ani ambazo zinaweza kuwaondolea hofu na maradhi mengine ya kimaanawi. Kwa mfano Muhammad bin al-Faraj amenukuliwa katika kitabu cha al-Kafi akisema: 'Abu Jaffar bin Ridha (as) – yaani Imam Jawad – aliniandikia dua ifuatayo na kusema: Mtu anayeisoma baada ya swala ya Alfajiri haombi haja yoyote ila hukidhiwa haja hiyo, na Mwenyezi Mungu kumuondolea kila linalomtatiza moyoni. Dua hiyo ni:
بسم اللّه و باللّه و صلى اللّه على محمد و آله و افوض امرى الى اللّه ان اللّه بصیر بالعباد، فوقاه اللّه سیئات ما مكروا، لا اله الا انت سبحانك انى كنت من الظالمین فاستجبنا له و نجیناه من الغم و كذلك ننجى المؤمنین، حسبنا اللّه و نعم الوكیل، فانقلبوا بنعمة من اللّه و فضل لم یمسسهم سوء ما شاء اللّه لا حول و لا قوه الا باللّه (العلى العظیم) ما شاءاللّه لا ما شاء الناس، ما شاء اللّه و ان كره الناس حسبى الرب من المربوبین، حسبى الخالق من المخلوقین، حسبى الرازق من المرزوقین، حسبى الذى لم یزل حسبى منذ قط، حسبى اللّه الذى لا اله الا هو، علیه توكلت و هو رب العرش العظیم
Ndugu wasikililizaji, ama shifaa ya maradhi ya kimwili kwa kutegemea Qur'ani Tukufu ni suala tutakalolijadili katika kipindi chetu kijacho cha Aya na Hadithi Inshallah.
Mmekuwa mkisikiliza kipindi hiki ambacho kimekuwa kikujieni moja kwa moja Kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Assalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakaatuh.