Jan 24, 2018 14:01 UTC
  • Aya na Hadithi (9)

Assalaam Aleikum wasikilizaji wepenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 9 ya kipindi hiki kinachozungumzia Aya za Qur'ani Tukufu pamoja na Hadithi za Mtume Muhammad (saw) na Watu wa Nyumba yake tukufu (as).

Ndugu wasikilizaji, katika kipindi cha juma hili tutajadili Surat at-Takathur na hasa ile sehemu inayosema wazi kuwa Siku ya Kiama Mwenyezi Mungu atamuuliza mwanadamu alifanyia nini neema alizompa. Hivyo na tusikilize kwa makini Aya hizo tukufu: Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu. Kumekushughulisheni kujifaharisha kwa wingi! Mpaka mkayazuru makaburi! Sivyo hivyo! Mtakujajua! Tena sivyo hivyo! Mtakujajua! Sivyo hivyo! Lau mngelijua kwa ujuzi wa yakini. Basi bila ya shaka mtaiona Jahannamu! Tena, bila ya shaka, mtaiona kwa jicho la yakini. Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema.

Wapenzi wasikilizaji, kama mnavyoona mtiririko wa Aya za Sura hii tukufu unatuelekeza katika utambuzi wa ukweli huu kwamba neema ambazo Mwenyezi Mungu atawauliza waja wake ni zile zinazopaswa kumuokoa mwanadamu na kutomtumbukiza kwenye Moto wa Jahannam. Hivyo neema hizo ni zile zisizokuwa za kawaida tunazozijiua sisi ambazo mwanadamu hujifaharisha nazo na mwishowe kumtumbukiza motoni. Hivyo neema hizo ni zipi? Endeleeni kuwa nasi ili tupate kujua jibu la swali hili muhimu.

 

Ndugu wasikiliza tunarejea katika Hadithi Tukufu ili tupate jibu la swali hili na ambalo linaenda sambamba na Aya Tukufu tulizotangulia kuzisoma. Tunaanza na ile Hadithi ambayo imenukuliwa na Fakhr ar-Razi katika Tafisri yake mashuhuri ambapo anasema:

'Jabir al-Ju'fi amepokelewa akisema: Nilifika mbele ya (Imam) Baqir naye akaniuliza: Wanasema nini wajuzi wa tafsiri kuhusiana na kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema? Wanasema maana yake ni kivuli na maji baridi…… Akasema, je, ikiwa utamuingiza mtu kwenye nyumba yako na kisha kumketisha kwenye kivuli na kumpa maji baridi utakuwa umemfanyia neema na ihsani? Nikasema: Hapana….. Akasema: Mwenyezi Mungu ni Mkarimu zaidi kuliko hivyo, hivi kwamba hawezi kumpa mja wake chakula na kumnywesha na kisha kumuuliza juu ya vitu hivyo. Nikasema: Basi tafsiri yake ni nini? Akasema: Neema hapa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Aliwaneemesha walimwengu kwa Mtume huyo na kuwaokoa kutokana na upotovu kupitia kwake. Je, hamsikii kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Hakika Mwenyezi Mungu amewaneemesha waumini kwa kuwaletea Mtume aliye miongoni mwao wenyewe?'

**********

Kama mnavyoona wapenzi wasikilizaji, Imam Baqir (as) anatolea hoja Qur'ani yenyewe na yale yaliyonukuliwa katika Aya nyinginezo za kitabu hicho cha mbinguni na dalili nyingine ambazo zinafungamana moja kwa moja na Surat at-Takaathur katika kuainisha kuwa ni Mtume Mtukufu (saw) ndiye kusudio la juu kabisa la Aya hiyo inayozungumzia suala la kuulizwa waja Siku ya Kiama juu ya neema waliyopewa na Mwenyezi Mungu na kutonufaika nayo kama walivyopaswa kufanya ili wapate kunusurika kutokana na Moto mkali wa Jahannam. Jambo hili pia linasadiki juu ya Maimamu Watoharifu wa Nyumba ya Mtume (as) kwa sababu wao ndio safina ya wongofu kama ilivyonukuliwa katika Hadithi nyingi za Kiislamu.

Imepokelewa katika kitabu cha Tafsiri ya Abu Hamza ath-Thumali na vilevile katika kitabu cha al-Mahasin cha Barqi kutoka kwa Abu Hamza kwamba alisema: 'Tulikuwa tumefika kundi mbele ya Aba Abdillah al-Imam Swadiq (as) ambapo alituitishia chakula kitamu na kizuri ambacho tulikuwa hatujawahi kukionja tena kabla ya hapo. Baada ya kushiba na kukinai tuliletewa tende ambazo tulikuwa tukiona nyuso zetu juu yake kutokana na usafi na ubora wazo. Hapo mtu mmoja akasema: Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema. Neema hii ambayo mmeneemeka nayo kwa mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Hapo Aba Abdillah as-Swadiq (as) akasema: Mwenyezi Mungu ni mkarimu na mtukufu zaidi kuliko akupeni chakula na kukunufaisheni nacho kisha akuulizeni kuhusiana nacho, bali alikuneemesheeni Muhammad na kizazi cha Muhammad (saw).'

 

Ni wazi wasikilizaji wapenzi kwamba Hadithi hizi zinategemea pia tafsiri ya kitabu cha Mwenyezi Mungu kutokana na maarifa sahihi ya Mola Mlezi. Na tutazame yale yaliyopokelewa katika Tafsiri ya Furat al-Kufi ambapo Sudeir as-Swairafi amepokelewa akisema: 'Nilikuwa kwa Ja'ffar as-Swadiq (as) naye akatuletea chakula ambacho nilikuwa sijawahi kukila katika maisha yangu yote. Akaniuliza: Ewe Sudeir umekionaje chakula chetu hiki? Nikasema: Baba na mama yangu wawe fidia kwako ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Nilikuwa sijawahi kula chakula kitamu kama hiki maishani mwangu na wala sidhani nitawahi kula chakula kama hiki tena maishani. Kisha machozi yalinilengalenga na nikalia. Aliniuliza: Ewe Sudeir! Ni nini kinachokuliza? Nikasema: Ewe Mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu nimekumbuka Aya moja katika kitabu cha Mwenyezi Mungu: Akauliza: Ni Aya gani hiyo? Nikajibu: Kauli ya Mwenyezi Mungu katika kitabu chake inayosema: Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema. Hivyo niliogopo chakula hiki kisije kikawa ni miongoni mwa neema hizo ambazo tutaulizwa juu yake na Mwenyezi Mungu.

Imam akasema: Ewe Sudeir! Hamutaulizwa juu ya chakula kizuri, nguo laini wala harufu nzuri, bali vitu hivi vimeumbwa kwa ajili yetu na sisi kwa ajili yavyo, hivyo na tuamiliane navyo kwa ajili ya kutii (Mwenyezi Mungu)….Nikamwambia: Baba na mama yangu wawe fidia kwako ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Basi maana ya neema ni nini? Akasema: Mwenyezi Mungu atawauliza Siku ya Kiyama juu ya mapenzi yao kwa Ali na Aali zake (kwa kusema): Je, mlinishukuru vipi nilipokuneemesheni kwa mapenzi ya Ali na Aali zake?''

***********

Na kufikia hapa, hatuna budi kukushukuruni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki cha Aya na Hadithi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kuwa mmenufaika vya kutosha na yale tuliyokuandalieni kwenye kipindi hiki. Basi hadi tutakapokutana tena katika kipindi kijacho panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.