Mar 05, 2018 07:17 UTC
  • Aya na Hadithi (12)

Assalaam Aleikum wapezi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhruri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Tuna furaha kukutana nanyi tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Aya na Hadithi ambapo tunanufaika na Aya pamoja na Hadithi Tukufu ambazo huchangamsha nyoyo zetu kutokana na imani sahihi juu ya rehema za Mwenyezi Mungu kwa waja wake ambao amewaamrisha wamtii na kutekeleza majukumu aliyowapangia kwa mujibu wa uwezo wao na kuwaondolea usumbufu. Wapendwa wasikilizaji, hebu tusikilize kwa makini Aya Takatifu zifuatazo za Qur'ani Tukufu ambazo kwa utaratibu ni Aya ya sita ya Surat al-Maida, Aya ya 78 ya Surat al-Haj na Aya ya 185 ya Surat al-Baqarah ambazo zinasema: Mwenyezi Mungu hapendi kukutieni katika taabu; bali anataka kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru. Na fanyeni juhudi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama inavyostahiki jihadi yake. Yeye ndiye ambaye amekuchagueni. Wala hakuweka juu yenu uzito katika Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibrahim. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mkamilishe idadi hiyo, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongozeni ili mpate kushukuru.

Kama mnavyoona wapenzi wasikilizaji, Aya hizi za Qur'ani Tukufu zinazungumzia masuala tofauti ya sheria za mkosho, wudhu, jihadi na saumu. Zinabainisha wazi kwamba lengo la sheria hizi za Mwenyezi Mungu ni kuwatakasa waja kutokana na udhaifu na udhia ikiwa ni katika kuwatayarisha kwa ajili ya kupata ufanisi na mafanikio ya kunufaika na neema kamili za Mwenyezi Mungu katika maisha yao ya humu duniani na huko Akhera. Mweyezi Mungu amewakalifisha waja kutekeleza majukumu yao ya kisheria na kiibada kwa mujibu wa uwezo wao. Hii ni kusema kuwa hajawakalifisha kutekeleza ibada yoyote ambayo iko nje ya uwezo wao. Kwa msingi huo iwapo itatokea kuwa mja hatakuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake ya kidini na kisheria kutokana na udhuru wowote wa kisheria basi taklifu ya kusimamisha ibada hiyo huwa imemuondokea kwa amri na ruhusa ya Mwenyezi Mungu. Kutokana na rehema yake, Mwenyezi Mungu Muumba humpa malipo na baraka za ibada hiyo kutokana na nia yake njema ya kutaka kuitekeleza.

 

Kwa kuzingatia suala hilo na kwa msingi wa kanuni hiyo ya Qur'ani Tukufu, Hadithi nyingi zimehimiza na kuwataka waumini wasijitese na kujisumbua kutekeleza majukumu ambayo nafsi zao hazina uwezo wa kuyatekeleza. Sharif Muratadha (MA) anasema katika juzuu ya pili ya kitabu cha ar-Rasail kwamba imepokelewa kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) akiwasihi Waislamu wafanye wepesi katika masuala yao ya kidini na wasiyafanya kuwa magumu kwa sababu hivyo ndivyo anavyotaka Mwenyezi Mungu ambaye amesema kwenye kitabu kitakatifu cha Qur'ani: Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito. Pia amesema: Mwenyezi Mungu anataka kukupunguzieni taabu. Mtume Mtukufu (saw) amesema: 'Fahamuni- Mwenyezi Mungu akurehemuni – kwamba kama Mungu angeliwakalifisha waja wake na mambo ambayo hawana uwezo wa kuyatekeleza basi hangekuwa anawatakia wepesi wala kuwapunguzia taabu kwa sababu wepesi na kutokuwa na taabu kwenye taklifu hakutimii kwenye mambo yaliyo nje ya uwezo wa mwanadamu.'

***********

Mtu anayetekeleza na kufuata wepesi huu ambao ametunukiwa na Mwenyezi Mungu katika majukumu yake ya kidini huwa amemridhia Muumba wake na kufuata maamrisho yake kama anavyotaka Yeye. Imam Ali (as) pia amenukuliwa katika vitabu vingi kikiwemo cha Man La Yahdhuruh ak-Faqih cha Sheikh Swaduq akisisitiza juu ya suala hilo la kuwepesishwa masuala ya kidini na kutoyafanya kuwa magumu kwa sababu huo ndio msingi wa dini. Kwa maana kwamba Mwenyezi Mungu anawatakia waja wake wepesi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kidin na sio kufanywa kuwa magumu. Kwa maneno mengine ni kuwa sheria za dini ni nyepesi na wala sio ngumu kama baadhi ya watu wanavyojaribu kuonyesha. Hilo ndilo lililokuwa kusudio la Mtume Mtukufu aliposema kuwa alitumwa kwa ajili ya kuwafikishia wanadamu dini iliyo rahisi na nyepesi kutekelezeka.

Hili ndilo suala analolisisitiza pia Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) katika Hadithi nyingine anapofutilia mbali wasiwasi wa kunajisika maji yaliyo karibu na najasa. Anamuruhusu muulizaji kutumia maji hayo madamu atakuwa hana habari ya kunajisika kwake. Anasema (as): Hakika dini si mashaka (taabu), kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema: ' Wala hakuweka juu yenu uzito katika Dini.

Muhammad, Mjumbe wa Allah

 

Maandiko matakatifu yanatahadharisha dhidi ya kufanya baadhi ya taklifu na majukumu ya kidini kuwa magumu na ya mashaka na kusisitiza kuwa hiyo ni moja ya njia za kuwatoa watu kwenye dini nyepesi na sahihi ya Mwenyezi Mungu kutokana na ujahili kama walivyofanya Makhawarij.

Imepokelewa katika kitabu cha al-Wasail kwamba Suleiman bin Ja'ffar al-Ja'ffari alimuuliza mja mwema wa Mwenyezi Mungu Musa bin Ja'ffar kuhusiana na mtu anayekwenda sokoni na kununua vazi la mnyama ambaye hajui kama amechinjwa kisheria au la, kwamba je, inasihi kuswali kwenye vazi hilo? Imam (as) alimjibu kwa kusema: 'Nam, hakuna tatizo katika hilo kwa sababu Abu Ja'ffar (as) alikuwa akisema: Hakika Makhawarij walijitaabisha kutokana na ujahili wao. Hakika dini ni pana zaidi kuliko hayo.'

Imeandikwa katika kitabu cha al-Kafi na vitavu vinginevyo vya kuaminika kwamba mtu mmoja alikatika kucha na kuweka dawa hapo kisha akamuuliza Imam Swadiq (as) namna alivyopasa kutawadha katika hali hiyo. Imam (as) alimjibu kwa kusema: Jambo hilo na mfano wake yanafahamika kutoka kwenye kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu ambapo anasema: Wala hakuweka juu yenu uzito katika Dini. Panguza juu yake.'

Na suala litakalotufungia kipindi hiki kwa leo wasikilizaji wapenzi ni Riwaya Tukufu ambayo inatuongoza kutambua kwamba kushikamana na Wilaya ya Maimamu Watoharifu na wa haki (as) ndio mfano bora na wa juu zaidi wa mafundisho haya aali ya Qur'ani kwa sababu watukufu hao wanamkinga mwanadamu dhidi ya kupotea njia na kisha kutoka kwenye dini ya haki. Imepokelewa katika kitabu cha al-Mahasin kutoka kwa Imam Swadiq (as) kwamba alisema kuhusiana na kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema, Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito: 'Wepesi ni Wilaya na uzito ni kinyume cha hivyo na kuwafuata maadui wa Mwenyezi Mungu.'

***********

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki cha Aya na Hadithi ambacho mmekitegea sikio kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.