Mar 06, 2018 11:19 UTC
  • Aya na Hadithi (14)

Assalaam Aleikum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tuna furaha kukutana nanyi tena katika sehemu hii ya 14 ya kipindi hiki cha Aya na Hadithi, ambayo itazungumzia Aya takatifu na Hadithi tukufu ambazo zinamtahadharisha mwanadamu dhidi ya kujishughulisha na mambo yanayompelekea kumsahau Muumba wake na matokeo mabaya ya jambo hilo.

Kwanza tunaanza kwa kutegea sikio kwa makini Aya mbili za 18 na 19 za Surat al-Hashr ambapo Mwenyezi Mungu anasema: Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kila nafsi iangalie inayoyatanguliza kwa ajili ya Kesho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayoyatenda. Wala msiwe kama wale waliomsahau Mwenyezi Mungu, na Yeye akawasahaulisha nafsi zao. Hao ndio mafasiki.

Ni wazi kutokana na Aya hizi kwamba uchaji Mungu hauambatani hata kidogo na kumsahau Mungu Muumba na ndio maana anatuhadharisha dhidi ya kumsahau, jambo ambalo humtumbukiza mwanadamu kwenye ufasiki na unafiki na kumpelekea kukumbwa na mwisho mbaya na mashaka humu duniani na Akhera. Kuhusiana na jambo hilo Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 67 ya Surat at-Tauba: Wanafiki wanaume na wanaafiki wanawake, wote ni hali moja. Huamrisha maovu na huyakataza mema, na huifumba mikono yao. Wamemsahau Mwenyezi Mungu, basi na Yeye pia amewasahau. Hakika wanafiki ndio mafasiki.

Aya hii inasema wazi kwamba kumsahau Mwenyezi Mungu humtumbukiza mtu kwenye unafiki, ubakhili na kuamrisha maovu na kuyakataza mema, yaani kutembea kwenye njia iliyo kinyume kabisa na matakwa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

 

Hebu tutazame hapa kwa pamoja Hadithi tukufu ili tupate kujua maana halisi ya kumsahau Mwenyezi Mungu kwa wale wanaomsahau. Tunasoma katika kitabu cha Tauhid cha Sheih as-Swaduq ambaye amenukuu Hadithi ndefu kutoka kwa Ameer al-Mu'mineen Ali (as) ambayo inasema: 'Mtu mmoja alimuuliza maana ya Aya ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu ambayo alikuwa hajaifahamu vyema. Imam (as) alimwambia: Ama kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema 'Wamemsahau Mwenyezi Mungu, basi na Yeye pia amewasahau', ina maana kwamba walimsahau Mwenyezi Mungu duniani kwa kutotekeleza yale aliyotaka basi Naye pia akawasahau huko Akhera. Yaani hakuwatengea thawabu na hivyo wakawa wamesahaulika kwenye malipo mema na ya kheri.'

Kwa maelezo hayo ndugu wasikilizaji, tunapata kufahamu kwamba Mwenyezi Mungu kuwasahau wale waliomsahau kuna maana ya wao kutozingatiwa katika malipo maalumu ambayo Mwenyezi Mungu amewatengea waja wake wema. Hili linatokana na kwamba watu hao waliomsahamu Mwenyezi Mungu huwa hawafai kupata malipo hayo mema kutokana na kughafilika kwao na malipo hayo ambayo tayari wameahidiwa kuyapata iwapo watatii maamrisho na makato ya Mwenyezi Mungu humu duniani na pia kumsahau Muumba wao Mtukufu. Hii ndiyo maana tunayoipata katika Qur'ani kwa msingi wa maarifa ya Mwenyezi Mungu. Maana hii pia ndiyo tunayoifahamu katika ufafanuzi wa kina wa Hadithi nyingine iliyonukuliwa na Sheikh as-Swaduq katika kitabu chake cha Maani al-Akhbar, ambapo Abdul Aziz bin Muslim amenukuliwa akisema: 'Nilimuuliza (Imam) Ridha (as) kuhusiana na kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema 'Wamemsahau Mwenyezi Mungu, basi na Yeye pia amewasahau' naye akasema, hakika Mwenyezi Mungu hasahau wala kupitiwa na jambo bali ni viumbe ndio wanaosahau na kughafilika kumsikiliza. Mwenyezi Mungu anasema: 'Na Mola wako si mwenye kusahau', bali huwalipa wale waliomsahau na pia kusahau Siku ya kukutana Naye kwa kuwasahaulisha nafsi zao kama anavyosema Mwenyezi Mungu mwenyewe: Wala msiwe kama wale waliomsahau Mwenyezi Mungu, na Yeye akawasahaulisha nafsi zao. Hao ndio mafasiki, na kauli yake Mungu Mtukufu inayosema: 'Basi leo Sisi tutawasahau kama walivyosahau kukutana na Siku yao hii, na kwa sababu ya kule kuzikataa Ishara zetu.' Yaani tutawaacha kama walivyoacha kujitayarisha kwa ajili ya kukutana na Siku yao hii.

 

Na mnaona wasikilizaji wapenzi kwamba, Imam Ridha (as) anatuwasilishia kwenye Hadithi hii mfano bora wa kutafsiri Qur'ani kwa Qur'ani na hili ni jambo ambalo Ahlul Beit (as) wametufundisha katika kuzifahamu vyema Aya Mutashabihat katika Qur'ani, yaani zisizofahamika moja kwa moja, bali zinahitaji ufafanuzi zaidi kutoka kwa wajuzi wa kitabu hicho cha mbinguni, na kwa kutegemea Aya Muhkamat, yaani zilizo wazi na zisizohitaji ufafanuzi wa kina. Mifano ya jambo hili ni mingi mno kwenye hadithi za Ahlul Beit (as). Mfano ni Hadithi hii iliyonukuliwa na mwanazuoni wa Kishafi' Muhammd bin Talha katika kitabu cha Matwalib as-Suuli fi Manaqib Aal ar-Rasuuli, ambapo Allama al-Waahidi katika tafsiri yake ya al-Wasit amemnukuu mtu mmoja akisema: 'Niliingia msikiti mmoja katika mji wa Madina ambapo nilikuta mtu mmoja akimzungumzia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) huku watu wakiwa wamemzunguka. Nikamwambia: Hebu nieleze maana ya Aya, Na kwa shahidi na chenye kushuhudiwa! Akasema: Nam….Ama kuhusu shahidi, maana yake ni siku ya Ijumaa na chenye kushuhudiwa maana yake ni siku ya Arafa. Nikaachana naye na kumwendea mwingine ambaye pia alikuwa akimzungumzia Mtume (saw).....Nikamwambia: Nifafanulie maana ya, Na kwa shahidi na chenye kushuhudiwa!....Akasema: Nam, ama kuhusu shahidi ni siku ya Ijumaa na chenye kushuhudiwa ni siku ya kuchinja. Nikaachana na wawili hao na kumwendea kijana mmoja ambaye uso wake ulikuwa unang'ara kama dinari, yaani ulikuwa unapendeza na kuvutia sana. Naye pia alikuwa akimzungumzia Mtume (saw). Nikasema: Hebu nifahamishe maana ya, Na kwa shahidi na chenye kushuhudiwa! Akasema: Nam, ama kuhusu shahidi, ni Muhammad (saw) na chenye kushuhudiwa ni Siku ya Kiama. Je, haujasikia Mwenyezi Mungu Mtukufu akisema: Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekutuma uwe shahidi na mbashiri na mwonyaji? Pia Mwenyezi Mungu anasema: Hiyo ndiyo Siku itakayokusanyiwa watu, na hiyo ndiyo Siku itakayoshuhudiwa. Mpokezi wa Riwaya hii akasema: Nikauliza mtu yule wa kwanza alikuwa ni nani wakaniambia alikuwa ni Ibn Abbas, nikaulizia kuhusu wa pili wakaniambia alikuwa ni Ibn Omar na kuhusu wa tatu, wakaniambia alikuwa ni al-Hassan bin Ali bin Abi Talib, na bila shaka kauli ya al-Hassan ilikuwa bora zaidi.'

*********

Na kwa Riwaya hiyo wasikilizaji wapenzi, ndio tunafikia mwisho wa kipindi cha juma hili cha Aya na Hadithi ambacho mmekuwa mkikisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi juma lijalo panapo majaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.