Apr 09, 2018 06:09 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Apr 9

Hujambo mpenzi msikilizaji na karibu tuangazie matukio muhimu yaliyojiri viwanjani ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa.....

Persepolis yatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Iran

Klabu ya Persepolis ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka hapa nchini kwa mwaka wa pili mfufulizo, baada ya kuichachafya klabu ya Padideh bao 1-0 katika mchezo uliopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Samen al-Aeme mjini Mashhad, kaskazini mashariki mwa nchi. Katika kipute hicho cha kukata na shoka, vijana wa Persepolis au ukipenda waite Wekundu wa Tehran wanaonolewa na Branko Ivankovic walianza kwa kasi nzuri na kutawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa, ingawaje walipoteza fursa chungu nzima ya kufunga mabao mengi. Bao hilo la kipekee na la ushindi la Persepolis lilifungwa kwa kichwa na kiungo wa kati wa klabu hiyo mwenye umri wa miaka 30, Vahid Amiri, zikiwa zimesalia dakika 18 mchezo umalizike.

Wachezaji wa Persepolis wakishangilia bao

 

Hii ni mara ya 11 kwa Wekundu wa Tehran kutwaa taji hilo. Mwaka jana, klabu hiyo ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka hapa nchini baada ya kuichachafya klabu ya Machine Sazi ya Tabriz mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Yadegare-Imam mkoani Tabriz, kaskazini mashariki mwa nchi, na hiyo kutia kikomo ukame wa miaka tisa wa kutoshinda taji hilo. Persepolis ilishinda taji hili kwa mara ya kwanza katika msimu wa ligi ya mwaka 2001-2002 huku wakitwaa ubingwa huo mara ya pili katika msimu wa mwaka 2007 na 2008.

Klabu ya Sepahan ndiyo imetwaa Ligi Kuu ya Soka ya Iran inayofahamika pia kama Persian Gulf Pro League mara nyingi zaidi, ikizingatiwa kuwa imetwaa taji hilo mara tano; katika misimu ya mwaka 2002-03, 2009-10, 2010-11, 2011-12 and 2014-15. 

 

Mkenya ashinda tena Paris Marathon

Mwanariadha nyota wa Kenya, Paul Lonyangata amehifadhi taji la mbio za Paris Marathon baada ya kuibuka kidedea tena mwaka huu. Katika mashindano hayo siku ya Jumapili katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris, Lonyangata alikata utepe wa ushindi baada ya kukimbia kilomita 42 na kwa kutumia saa 2, dakika 6 na sekunde 21. Lonyangata anakuwa Mkenya wa kwanza kushinda taji hilo kwa mwaka wa pili mfululizo, baada ya Muingereza Steve Brace kushinda taji hilo mwaka 1989 na 1990.

Lonyangata (Kulia) na Saina

 

Mwanariadha chipukuzi wa kike wa Kenya, Betsy Saina ameibuka kidedea upande wa wanawake kwa kutumia saa 2, dakika 22 na sekunde 56, hili likiwa ni shindano lake kuu la riadha kushiriki na kuibuka mshindi.  Betsy anashinda taji hili baada ya panda shuka nyingi katika safari yake ya riadha.

Kenya imeshinda taji la Paris Marathon upande wa wanaume na wanawake mwaka huu, kama ilivyofanya mwaka jana, na hivyo kudhihirishia dunia kuwa nchi hiyo inasalia kuwa moto wa kuotea mbali katika mbio za masafa marefu.

Wachezaji wa Israel wapigwa marufuku Tunisia

Mahakama moja nchini Tunisia imewapiga marufuku wanamichezo wa taekwondo wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuingia nchini humo. Vuguvugu la kupinga kufanywa wa kawaida uhusiano wa Tunisia na Israel liitwalo National Commission for Supporting Arab Resistance and Opposing Normalisation and Zionism lilienda mahakamani kumshtaki Rais wa Shirikisho la Taekwondo nchini humo, Ahmed Gaaloul, likitaka asiruhusiwe kuwaalika wanamichezo hao wa Israel kushiriki mashindano ya mchezo huo katika eneo la Hammamet mwezi huu wa Aprili. Sofiane Selliti, Msemaji wa Mwendesha Mashitaka katika kesi hiyo ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, uamuzi huo wa mahakama unamaanisha kuwa, Shirikisho la Taekwondo limepigwa marufuku kuwaalika, kuwapokea au kuwa mwenyeji wa wanatakekwondo wanne wa Kizayuni ambao walitazamiwa kushiriki mashindano hayo yanayomalizika Aprili 13.

Watunisia wakiandamana kuwaunga mkono Wapalestina

 

Mwezi Februari mwaka huu, mamia ya wanaharakati wa kisiasa na kijamii wa nchini Tunisia walifanya maandamano wakilitaka bunge la nchi hiyo lifanye haraka kupitisha sheria ambayo itatamka wazi kuwa ni uhalifu kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel. Waandamanaji hao walikuwa wamebeba bendera za Palestina na mabango yenye maandishi ya kuilaani vikali Israel na kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina.

Wambura maji shingoni, TFF yamshupalia

Kamati ya Rufaa za Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetupilia mbali rufaa ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa shirikisho hilo, Michael Wambura, hivyo adhabu aliyopewa na Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo itaendelea.  Wambura alifungiwa kutojihusisha na kujishughulisha na masuala ya mpira wa miguu maisha yake yote na Kamati ya Maadili ya TFF kwa makosa matatu ikiwemo la kupokea au kuchukua fedha za shirikisho hilo kwa malipo ambayo hayakuwa halali. Akisoma hukumu hiyo Aprili 6, Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa za Maadili ya TFF, Ebenezer Mshana amesema wamesikiliza pande zote mbili za mrufani na mjibu rufani na kuzitupilia mbali rufaa zote za Wambura kutokana na kutokuwa na hoja za msingi.

Mshana amesema rufaa ya Wambura iliyopelekwa mbele ya kamati yao haina mashiko hivyo wameridhia adhabu aliyopewa katika Kamati ya Maadili kama ilivyoamuliwa ya kufungiwa maisha kujihusisha na soka. Makosa mengine yaliyomtia hatiani Wambura mbali na kuchukua fedha za TFF, ni kugushi barua ili alipwe fedha za kampuni ya Jeck System na kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya shirikisho hilo. Hata hivyo, Wambura ameshutumu vikali uamuzi huo alioutaja kama wa kishabiki.

Man City watolewa tonge mdomoni

Klabu ya Machester City imetolewa tonge mdomoni! Ni sentensi fupi lakini yenye kufikisha maana kamili, iwapo ungeliulizwa kueleza mchezo uliopigwa wikendi kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, kati ya klabu ya Man City na Machester United. Aghalabu ya mashabiki na wafuatiliaji wa soka walikuwa wakiamini kuwa Man City wataondoka na ushindi, baada ya dakika 45 za kwanza kumalizika wakiwa wanaongoza kwa magoli 2-0. Na kwa kuwa kutangulia sio kufika, mambo yaliwageukia ndani nje katika kipindi cha pili. Katika mchuano huo ambao iwapo City wangelishinda, wangelitwaa Taji la EPL msimu huu, kiungo Vincent Kompany aliiweka City kifua mbele kwa bao lake alilolifunga kunako dakika ya 25. Dakika tano baadaye, Ilkay Gundogan aliongeza la pili na hivyo City ikaende mapumzikoni meno yote yakiwa nje.Katika kipindi cha pili, Man United ambao walikuwa wanaupiga ugenini katika Uwanja wa Etihad waliingia na ari na kasi mpya.

Mchezaji nyota wa Man U, Paul Pogba

 

Baada ya pasi za hapa na pale, walifanikiwa kucheka na nyavu za City mara mbili, chini ya dakika 10 baada ya kipindi cha pili kuanza, kupitia kiungo Paul Pogba aliyefunga katika dakika ya 53 na dakika ya 55. Mabao hayo ya Pogba yalivuruga mahesabu ya City ambao katika dakika 25 za mwisho, mambo yalionekana kugeuka kuwa mazito kwao. Mashetani Wekundu walizidisha kasi ya mchezo na hatimaye wakapata goli la ushindi katika dakika ya 69 kupitia kwa beki wao Chris Smalling, na hivyo ndivyo City wakaakhirishiwa kutwaa Taji la EPL kama ilivyotazamiwa na wengi.

Kwengineko Arsenal ilipata ushindi kama huo wa Man U wa mabao 3-2 waliposhuka dimbani kuvaana na Southampton Jumapili, huku Chelsea wakilazimishwa sare ya 1-1 na West Ham. Liverpool pia ilipigwa stop na Everton na mchezo wao kuishia sare tasa. City wanasalia kileleni mwa jedwali la ligi wakiwa ana alama 84, wakifuatiwa na Man U wenye alama 71. Liverpool na Tottenham zipo katika nafasi ya tatu na nne kwa usanjari huo, licha ya wote kuwa na alama 67, ingawaje wanatofautiana kwa mabao. Orodha ya tano kwa bora kwa sasa inafungwa na The Blues wenye alama 57.

……………………..TAMATI……………….