Apr 17, 2018 09:21 UTC
  • Aya na Hadithi (17)

Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 17 ya kipindi hiki cha Aya na Hadithi ambapo kwa leo tutajadili na kupitia maandiko matakatifu yanayotufahamisha lengo kuu la kuumbwa kwetu wanadamu humu duniani na faida tutakazopata ikiwa tutafikia lengo hilo.

Lengo hilo linabainishwa wazi na Qur'ani Tukufu ambapo inasema katika Aya za 56 hadi 58 za Surat adh- Dhariyaat: Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi. Sitaki kwao riziki, wala sitaki wanilishe. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti.

Hivyo wapenzi wasikilizaji Mwenyezi Mungu ndiye anayetoa riziki na ambaye ni mkwasi na wala hawahitajii waja wake katika suala lolote lile. Amejalia ibada ya waja hao, yaani watu na majini kwake kuwa lengo kuu na la mwisho la kuwaumba, ili kwa ibada hiyo waweze kukwea na kufikia daraja za juu zaidi katika kupata riziki ya Mwenyezi Mungu. Je, ni daraja zipi hizi za riziki maalumu ya Mwenyezi Mungu?

Ili kupata jibu la swali hili muhimu tunachunguza Hadithi kadhaa ambapo tunaanza na hii ambayo imenukuliwa na al-Hurr al-Amili katika kitabu chake cha at-Tuhfatu al-Qudsiyya ambapo Mtume Mtukufu (saw) amenukuliwa akisema: 'Mwenyezi Mungu amezungumzia nafsi yake kwa kusema: Mimi huketi na mtu anayenikumbuka, nikumbukeni nami nitakukumbukeni kwa neema yangu, nikumbukeni kwa utiifu na ibada nami nitakukumbukeni kwa neema, ihsani, rehema na maridhio…….Akasema: Na imepokelewa katika Hadithi Qudsi: Ewe mwanadamu! Mimi ni mkwasi asiyepungukiwa na lolote, hivyo nitii katika yale niliyokuamuru nitakufanya kuwa mkwasi asiyepungukiwa na lolote, ewe mwanadamu! Mimi ni hai asiyekufa, nitii katika yale niliyokuamrisha nitakufanya hai asiyekufa, mimi huliambia jambo (kitu) kuwa na linakuwa, nitii katika yale niliyokuamrisha nitakufanya uliambie jambo (kitu) kuwa na linakuwa.'

 

Kufikia hapa wapenzi wasikilizaji inafahamika wazi kwamba katika rehema za Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni kufanya ibada kuwa lengo lao la mwisho na la juu zaidi ambalo ikiwa watalifikia basi huwa wamejiandalia uwanja wa kufikia utajiri, ukwasi na maisha ya milele yenye saada na nguvu kubwa na tukufu isiyokuwa na mwisho kutokana na kuungana kwake moja kwa moja na Mwenyezi Mungu Muweza wa kila kitu. Je, kuna neema nyingine gani iliyo bora na tukufu kuliko hii?!

Hivyo basi rehema ya Mwenyezi Mungu ndilo lengo la kuumbwa wanadamu na majini kwa sababu waja hufanya juhudi za kuifikia rehema hiyo. Sheikh Swaduq amenukuu katika kitabu cha Ilalu ash-Sharai' Hadithi kutoka kwa Abu Baswir ambaye amesema: 'Nilimuuliza Abu Abdillah (Imam Swadiq) (as) maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu inayosema: Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi', akasema: Aliwaumba ili awaamuru kutekeleza ibada. Akasema: Na nilimuuliza maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Lakini hawaachi kukhitalifiana, isipokuwa wale ambao Mola wako amewarehemu; na kwa hiyo (rehema) ndio Mwenyezi Mungu amewaumba (Hud: 118-119). Akasema: Ili wafanye yale yatakayowaletea rehema yake (Mwenyezi Mungu) na hivyo kuwarehemu.' Yaani wamwabudu Mwenyezi Mungu na hivyo kupata rehema zake.'

Tunasoma katika kitabu hichohicho, Hadithi iliyopokelewa na Muhammad bin Ammara ambaye anasema: 'Nilumuuliza as-Swadiq Ja'ffar bin Muhammad (as) ni kwa nini Mwenyezi Mungu aliumba viumbe? Akasema: Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuwaumba ovyoovyo viumbe na wala hakuwaacha hivihivi bali aliwaumba kwa ajili ya kudhihirisha nguvu zake na kuwakalifisha utiifu kwake, ili kwa hilo wapate radhi zake. Wala hakuwaumba kwa ajili ya kupata manufaa yoyote kutoka kwao wala kujikinga nao madhara, bali aliwaumba ili awanufaishe na kuwafikisha kwenye neema za kudumu milele.'

 

Wapenzi wasikilizaji, rehema za Mwenyezi Mungu zinakamilika kwa Yeye kuwarahisishia waja wake utekelezaji wa ibada hiyo kwa kuweka kwenye maumbile ya viumbe uzingatiaji wa Mungu Muumba. Suala hili linaashiriwa na Hadithi iliyonukuliwa katika kitabu cha Tauhid, ambayo imepokelewa na Muhammad bin Abi Umeir ambapo anasema: 'Nilimuuliza Abu al-Hassan Musa bi Ja'ffar (as), je, nini maana ya kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) inayosema: 'Jitahidini kwa sababu kila kiumbe kitafanikiwa katika kile kilichoumbwa kwa ajili yake? Akasema: Hakika Mwenyezi Mmungu Mtukufu aliwaumba wanadamu na majini ili wapate kumuabudu na wala hakuwaumba ili wamuasi, na hilo linatokana na kauli yake Mwenyezi Mungu inayosema: Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi. Hivyo alikifanikisha kila kiumbe kwa kile kilichoumbwa kwa ajili yake. Hivyo basi ole wake yule anayechagua upotovu badala ya uongofu!'

Kama ambavyo urahisishaji huu wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake katika utekelezaji wa ibada zao hudumu na kuendelea kupitia uongozi wake kwa waja hao, kwa namna ambayo kila mmoja hunufaika na baraka zake kwa kiwango kinachomfaa. Tunarejea kitabu cha Ilalu as-Sharai' ambapo tunasoma Hadithi nyingine kutoka kwa Mtume (saw) ambayo aliipokea kutoka kwa Malaika Jibril (as) inayosema: 'Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: Mja wangu hanikaribii mathalan, kwa kutekeleza yale niliyomuamrisha na kuendelea kuniomba dua ila mimi humpenda na ninayempenda, mimi huwa ni sikio, jicho, mkono na kimbilio lake. Akiniomba dua mimi humjibu na akiniomba jambo humpa. Hakika katika waja wangu waumini, kuna mtu anayeuendea mlango kwenye ibada (yake) na mimi humzuia ili asije akaingiwa na majivuno ambayo huenda yakamharibu, na hakika katika waja wangu waumini, kuna mtu ambaye imani yake haiwi sawa ila kwa umasikini na lau kama ningemtajirisha hilo lingemuharibu. Na hakika katika waja wangu waumini, kuna kuna mtu ambaye imani yake haitengenei ila kwa utajiri na lau ningemfanya kuwa masikini hilo lingempotosha. Hakika katika waja wangu waumini, kuna mtu ambaye imani yake hautengenei ila kwa kumjalia maradhi sugu na lau ningerekebisha afya ya mwili wake, hilo lingempotosha. Na hakika katika waja wangu waumini kuna mtu ambaye imani yake haiwi sawa ila kwa kumpa siha na lau ningemjalia maradhi sugu lingempotosha hilo. Mimi huwapanga waja wangu kwa mujibu wa elimu niliyonayo juu ya nyoyo zao, hakika mimi ni Mwenye kujua, Mwenye habari.'

 

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi cha Juma hili cha Aya na Hadithi. Tunakushukuruni nyote kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi hiki ambacho kama kawaida mumekitegea sikio kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwatangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaliwa kukutana tena juma lijalo, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.