Aya na Hadithi (18)
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni kusikilizaji sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Aya na Hadithi.
Katika kipindi kilichopita, tulijadili baadhi ya Aya na Hadithi ambapo tuliona kwamba ibada ya Mwenyezi Mungu ndilo lengo kuu lililopelekea kuumbwa kwa wanadamu na majini ikiwa ni katika rehema za Mwenyezi Mungu kwao kwa sababu ndiyo njia pekee ya kuwaletea mafanikio na kupata daraja za juu kabisa za riziki inayodumu milele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa kuzingatia hayo je, ni ibada gani inayoweza kumfikisha mwanadamu kwenye lengo hilo. Hili ndilo suala tutakalolijadili katika kipindi chetu cha leo na kwanza tutatafuta jibu lake kutoka kwenye kitabu kitakatifu cha Qur'ani ambapo tunasoma Aya ya 5 hadi 8 za Surat al-Bayyinah ambapo Mwenyezi Mungu anasema: Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu, na wasimamishe Swala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Dini ya kisawasawa. Hakika waliokufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu na washirikina wataingia katika Moto wa Jahannamu wadumu milele humo. Hao ndio viumbe waovu kabisa. Hakika walioamini na wakatenda mema, hao ndio bora wa viumbe. Malipo yao kwa Mola wao ni Bustani za milele, ambazo hupita mito chini yake. Wakae humo milele. Mwenyezi Mungu yuko radhi nao, na wao wako radhi Naye. Hayo ni kwa anayemwogopa Mola wake.

Inabainika wazi kutokana na Aya hizi tukufu kwamba kumtakasia Mwenyezi Mungu dini na ibada ndiko kunakofanya ibada kuwa njia na wasila wa kumfanya mwanadamu afuzu na kufanikiwa kupata radhi za Mwenyezi Mungu pamoja na riziki zake kwa daraja za juu kabisa. Lakini je, utakasaji huo hufikiwa vipi? Hebu tuzingatie Hadithi kadhaa ili tupate jibu la swali hili. Tunasoma katika kitabu cha Ilal as-Sharai' Hadithi ambayo imepokelewa kutoka kwa Imam Swadiq (as) ambaye ananukuliwa akisema: 'Hussein bin Ali (as) alifika mbele ya masahaba wake na kuwaambia: Enyi Watu! Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuumba wanadamu ila wapate kumjua, na wanapomjua humwabudu na wanapomwabudu huwa hawana tena haja ya kumwabudu asiyekuwa Yeye. Mtu mmoja akamuuliza: Ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw)! Baba na mama yangu wawe fidia kwako! Je, nini maana ya kumjua Mwenyezi Mungu? Akasema (Imam): Ni watu wa kila zama kumtambua Imam wao ambaye wanapasa kumtii.'
Kwa hivyo wapezi wasikilizaji maarifa ya Mwenyezi Mungu ambayo mwanadamu anayapata kutoka kwa Imam maasumu na khalifa aliyekamilika pande zote na ambaye ameteuliwa na Mmwenyezi Mungu Mtukufu ndiyo yanayompelekea kuepuka kila aina ya shirki na kumuabudu Mwenyezi Mungu mmoja tu ambaye kwake huona kila aina ya ukamilifi, jamali, huruma, rehema na utulivu. Kwa msingi huo maarifa haya yanapotimia ndipo ikhalsi ya mwanadamu kwa Mwenyezi Mungu nayo huwa imethibiti. Imam Swadiq (as) anasema katika Hadithi ambayo imepokelewa kutoka kwake katika kitabu cha al-Kafi: 'Lau watu wangelijua kile kilichoko kwenye fadhila za maarifa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, wasingeelekeza macho yao katika yale aliyowaneemesha Mwenyezi Mungu maadui katika mapambo ya maisha ya dunia na neema zake. Dunia kwao ingekuwa ni yenye thamani duni kuliko wanayoyakanyaga kwa miguu yao na wangelineemeka kwa maarifa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kunufaika kwa ladha yake kama ile ladha wanayonufaika nayo wale walio pembeni ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu Peponi. Hakika maarifa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ni faraja kutokana na kila hofu, sahibu katika kila upweke, nuru katika kila giza, nguvu katika kila udhaifu na ponyo katika kila maradhi.'

Ndugu wasikilizaji, kile kinachomfikisha mwanadamu katika maarifa na ikhlasi hii kwa Mwenyezi Mungu ni kumfuata Imam wa haki ambaye anamdhihirishia Mwenyezi Mungu ikhlasi kwa njia bora zaidi katika ibada zake na hili ndilo jambo ambalo tunalishuhudia kwa uwazi mkubwa katika maisha ya Maimamu watoharifu wa kizazi cha Muhammad (as). Suala hili linathibitishwa wazi na kauli ya Imam Ali (as) ambaye anasema katika moja ya dua zake: 'Ewe Mungu Wangu! Mimi sikuabudu kwa sababu ya kuhofu adhabu yako wala kutokana na tamaa ya thawabu zako bali nimekuona kuwa unayestahiki kuabudiwa nami nikakuabudu.'
Kauli hii inafanana na kauli ya Imam as-Swadiq (as) ambaye imepokelewa akisema katika kitabu cha Ilal as-Sharai': 'Watu humuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu katika hali tatu: Kuna kundi linalomwabudu kwa tamaa ya kupata thawabu zake, nayo ni ibada ya walio na shauku, ambayo ni tamaa, na wengine humuabudu kwa kuhofia moto nayo ni ibada ya watumwa, ambayo ni hofu. Lakini mimi humuabudu kutokana na mapenzi yangu kwake nayo ni ibada ya watukufu, ambayo ni amani kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu inayosema: Nao watasalimika na mfadhaiko wa siku hiyo (27:89) na kauli yake inayosema: Sema: Ikiwa mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni, Mwenyezi Mungu atakupendeni na ataghufirieni madhambi yenu….(3:31). Hivyo mtu anayempenda Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenyezi Mungu humpenda na mtu anayependwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu huwa miongoni mwa watu waliosalimika na mfadhaiko.'
Nam wapenzi wasikilizaji, Mtu anayewafuata wema hawa katika kizazi cha Mtume Mtukufu (saw) huwa miongoni mwa viumbe wema na bora waliozungumziwa katika Aya za Surat al-Bayyinah. Wafasiri wa Qur'ani kutoka pande zote mbili za Suni na Shia wanasema kuwa Aya hizi ziliteremka kumsifu Imam Ali (as). Kwa mfano as-Suyuti amenukuu katika Tafsiri yake ya ad-Dur al-Manthur Hadithi iliyopokelewa na Jabir bin Abdallah al-Answari akisema: 'Tulikuwa mbele ya Mtume (saw) naye Ali akawa amefika. Hapo Mtume (saw) akasema: Naapa kwa jina la yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake kuwa hakika huyu na Mashia (wafuasi) wake ndio watakaofuzu Siku ya Kiama na hapo ikateremka Aya ya: Hakika walioamini na wakatenda mema hao ndio viumbe bora. Tokea hapo masahaba wa Mtume (saw) kila alipokuwa akifika sehemu Ali, walikuwa wakisema: Amekuja mbora wa viumbe.'

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Aya na Hadithi kwa juma hili, kipindi ambacho mmekisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.