Ulimwengu wa Spoti, Mei 7
Huu ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita..
Iran yaibuka ya 3 soka ya viziwi Korea Kusini
Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya wanaume wenye matatizo ya kusikia imemaliza katika nafasi ya tatu ya mashindano ya kimataifa ya mchezo huo yaliyifanyika nchini Korea Kusini. Timu hiyo ya mpira wa miguu ya Iran ilichabanga Thailand mabao 8-0 katika mchuano wa kumtafuta mshindi wa tatu uliopigwa katika Uwanja wa Changwon Center, kusini mashariki mwa nchi siku ya Jumapili. Kiungo Shahin Fasihi ndiye aliyefungua mvua ya mabao ya Iran, dakika tano tu baada ya kupulizwa kipenga cha kuanza kitimutimu.
Dakika 8 baadaye, Hossein Mesbahi aliongeza la pili, kabla ya Ali Akbar Ahmadvand kuonyesha umbuji wake wa soka kwa kufunga mabao matatu ya hatrick, katika dakika za 23, 56 na 61. Mabao mengine ya Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya wanaume wenye matatizo ya kusikia yalifungwa na Iman Mohebbi, Alireza Basih na Mohsen Farzi. Wakati huo huo, Saudi Arabia iliibamiza Malaysia mabao 2-0 katika mechi ya kuwania nafasi za tano na sita za mashindano hayo, yanayofahamika kwa Kimombo kama Asia Pacific Deaf Football Championships yaliyoanza Aprili 23 na kufunga pazia lake Mei 7.
Esteqlal watwaa Kombe la Hazfi (Mtoano)
Klabu ya soka ya Esteghlal ya Tehran imetwaa Kombe la Mtoano (Hazfi) kwa mara ya saba sasa, baada ya kuizaba Khooneh be Khooned bao moja la uchungu bila jibu siku ya Alkhamisi. Katika mchuano huo wa aina yake uliopigwa katika Uwanja wa Naftogaz Arvandan katika mji wa Khorramshahr mkoani Khuzestan kusini mashariki mwa nchi, vijana wa Tehran wanaovalia majezi ya samawati waliitandaza ngozi ingawaje walipoteza fursa kibao za kuongeza magoli. Bao hilo la pekee katika mchuano huo na la ushindi kwa The Blues wa Tehran lilipachikwa kimyani na mchezaji Mame Baba Thiam kunako dakika ya 35.
Esteqlal ndiyo klabu iliyotwaa Kombe la Hazfi mara nyingi katika historia ya taji hilo la muondoana lililoasisiwa mwaka 1975 na Shirikisho la Soka Iran. Hivi ndivyo hali iliyokuwa wakati klabu hiyo ya Tehran ikikabidhiwa kombe.
Riadha: Wakenya watamalaki, Semenya ang'ara licha ya makelele
Wanariadha wa Kenya walitamalaki mbio za mita 800 kwa upande wa wanaume katika Ligi ya Almasi mjini Doha nchini Qatar siku ya Ijumaa. Emmanuel Korir aliibuka kidedea katika mbio hizo kwa kutumia dakika moja, sekunde 45 na nukta 21, huku akiwaongoza Wakenya wenzake Elijah Manangoi na Nicholas Kipkoech waliomaliza katika nafasi za pili na tatu kwa usanjari huo.
Kwa msingi huo Wakenya hao watatu walipanda wote jukwani na kuzoa medali zote tatu. Kadhalika katika mbio za mita elfu 3 kwa upande wa akina dada, Caroline Kipkirui aliwaongoza wenzake Agnes Tirop na Hyvin Kiyeng kutwaa medali zote za dhahabu, fedha na shaba katika mashindano hayo ya Diamond League yaliyofanyika Ijumaa mjini Doha.
Hata hivyo wanariadha wa kike wa Kenya hawakuwa na lao katika mbio za mita 1,500 kwani walionyeshwa kivumbi. Mwanariadha kutoka nchini Afrika Kusini Caster Semenya, aliweka rekodi kwa taifa lake kwa kushinda katika michuano ya awali ya mbio za msimu za mita 1500 kwa wanawake kwenye michuano ya Diamond League, kwa kutumia dakika tatu sekunde 59 tisa na nukta za kuhesabika katika mbio hizo.
Semenya ambaye amekuwa akizungukwa na utata wa jinsia ameibuka kidedea katika hali ambayo, yumkini akapata pigo kutoka na sheria mpya zinazowakabili wanariadha wa kike wenye homoni nyingi za kiume. Mkenya Nelly Jepkosgei aliibuka wa pili katika mbio hizi huku Habitam Alemu wa Ethiopia akifunga orodha ya tatu bora.
Katika hatua nyingine, bingwa mara tatu wa dunia katika mbio za 1,500 Asbel Kiprop, mwanariadha kutoka nchini Kenya, amekanusha madai kuwa amekuwa akitumia dawa zilizopigwa marufuku za kumwongezea nguvu mwilini, kumsaidia kushinda mashindano mbalimbali ya Kimataifa. Ofisi ya Maadili na Kupambana na Pufya ya Shirikisho la Riadha Duniani IAAF imesema iwapo mwanariadha huyo atapatikana na hatia, huenda akafungiwa njeya riadha kwa miaka mine na hata kutozwa faini. Hata hivyo Kiprop mwenye umri wa miaka 28 anasisitiza kuwa mwili wake hauna hata chembe ya pufya na kwamba hawezi kuharibu jina na kipaji chake kwa kutumia dawa hizo haramu.
Katika taarifa, Kiprop ameongeza kuwa, “Nimesoma ripoti ikinihusisha na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini, mimi nimekuwa katika mstari wa mbele kupinga matumizi ya dawa hizo.”
Dondoo za hapa na pale
Tuanzie nchini Kenya ambapo, Shirikisho la Soka nchini humo FKF limemtangaza Mfaransa Sebastian Migne kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Harambee Stars. Migne anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mbelgiji Paul Put aliyejizulu mwezi Februari, miezi mitatu tu baada ya kuhudumu katika nafasi hiyo. Raia huyo wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 45, kabla ya kuteuliwa kuifunza Harambee Stars, alikuwa kocha wa timu ya taifa ya Congo-Brazaville.
Mbali na hayo, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) zinashiriki katika mashindano ya pikipiki yaliyoitishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel yaliyoanza Ijumaa. Shirika la habari la IRIB limeripoti kuwa, mashindano hayo yanafanyika kama sehemu ya sherehe za kuadhimisha miaka 70 ya kuundwa utawala pandikizi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina. Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina ililalamikia vikali kufanyika mashindano hayo yanayofahamika kama Giro d'Italia Cycling, lakini nchi za Kiarabu za Bahrain na Imarati zimepuuza jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya Waarabu wenzao na zimeamua kushiriki kwenye maadhimisho hayo, suala ambalo linathibitisha kivitendo kuwa zinakubaliana na jinai na uvamizi wa Israel. Wakati huo huo, Kamati ya Olimpiki ya Palestina POC imeitaja hatua hiyo ghalati ya Bahrain na Imarati kama 'fedheha'.
Na hatimaye klabu ya Manchester City imetunukiwa Taji la Ligi Kuu ya soka Uingereaza, licha ya kulazimishwa sare ya mtungi kwa mtungi na Huddersfield. City ilitangazwa bingwa wa Ligi ya EPL kwa mara ya tano sasa, baada ya watani wao wa jadi ambao wapo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa EPL, klabu ya Manchester United kupoteza mchuano muhimu wakiwa nyumbani wiki chache zilizopita. Mashetani Wekundu walizabwa bao moja la uchungu bila jibu na West Brom katika kitimutimu hicho kilichosakatwa ugani Old Trafford. Hawa hapa wachezaji na mashabiki wa Man City wakishangilia Kombe la EPL msimu huu siku ya Jumapili, Etihad.
City watakuwa wenyeji wa Brighton nyumbani Etihad siku ya Jumatano kabla ya kumaliza msimu kwa mchuano wa ugenini mnamo Mei 13, watapotoana udhia na klabu ya Southampton.
…………………..TAMATI………………