Ijumaa tarehe 15 Juni 2018
Leo ni Ijumaa tarehe Mosi Shawwal 1439 Hijria sawa na Juni 15, mwaka 2018.
Leo ni Ijumaa tarehe Mosi Shawwal inayosadifiana na Idi tukufu ya al-Fitr. Idul Fitri ni miongoni mwa sikukuu kubwa katika dini tukufu ya Kiislamu. Baada ya kukamilisha ibada ya funga, kuomba na kujipinda kwa ibada katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, Waislamu hufanya sherehe katika siku hii kubwa wakimshukuru Mola manani kwa kuwawezesha kukamilisha ibada huyo. Iddi al Fitr ni kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa ibada na kujisafisha. Aidha katika siku kama hii ya leo ni haramu kufunga saumu yoyote na Waislamu baada ya juhudi za mwezi mzima za kupambana na nafsi na kuchuma matunda ya ucha-Mungu hukusanyika pamoja na kusali Sala ya Iddul Fitr. Kuhusiana na utukufu wa siku hii Mtukufu Mtume (saw) anasema: "Mtu yeyote atakayemuasi Mwenyezi Mungu katika siku ya Idi, basi ni kama mtu aliyemuasi Mwenyezi Mungu siku ya miadi- yaani Siku ya Kiama." Kwa mnasaba wa siku hii adhimu, Redio Tehran inatoa mkono wa pongezi, heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani.

Siku kama ya leo miaka 1186 iliyopita mpokezi mashuhuri wa hadithi wa Ahlusunna, Imam Bukhari aliaga dunia. Abu Abdullah Muhammad Ismail aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Imam Bukhari ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa hadithi wanaoaminiwa na Ahlusunna. Alisafiri sana kwa ajili ya kutafuta hadithi za Mtume (saw). Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni kile cha Jamius Swahih maarufu kama Sahihi Bukhari. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni: Al Adabul Mufrad, Tarikhul Ausat na As Sunan.

Miaka 833 iliyopita katika siku kama hii ya leo ya tarehe Mosi Shawwal alifariki dunia Abu Abdallah Muhammad bin Omar Razi mashuhuri kwa jina la Fakhrurazi msomi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu. Alizaliwa katika mji wa Rey jirani na Tehran na alifanikiwa kwa haraka kujifunza elimu mbalimbali za Kiislamu kama Fiqihi, Tafsiri, Falsafa na Mantiki kutokana na kipaji kikubwa alichokuwa nacho. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vya Fakhrurazi ni Sherh Nahaj al-Balagha, Nihayat al-Uquul wa Siraj al-Quluub.

Siku kama ya leo miaka 170 iliyopita sawa na tarehe 15 Juni 1848, Otto von Bismarck Kansela wa Ujerumani aliuchagua mji wa kihistoria na maarufu wa Berlin, kuwa mji mkuu wa nchi hiyo. Kuteuliwa mji wa Berlin kuwa mji mkuu wa Ujerumani, kulitokana na utekelezaji wa mpango wa kuziunganisha Ujerumani mbili, uliobuniwa na Kansela Bismarck. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Ujerumani iligawanyika katika sehemu mbili za Mashariki na Magharibi. Mwezi Septemba 1990 baada ya kuvunjwa ukuta wa Berlin, kuliandaliwa mazingira ya kuunganishwa pande hizo mbili, na hatimaye Berlin kurejea tena na kuwa mji mkuu wa Ujerumani.

Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, mwafaka na tarehe 15 Juni 2000, idadi kubwa ya askari wa kikosi maalumu cha jeshi la Uingereza iliondoka kwenye ardhi ya Sierra Leone, magharibi mwa Afrika. Amri ya kuondoka vikosi hivyo vya Uingereza ilitangazwa na John Prescott, Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza. Wanajeshi wengine 300 wa nchi hiyo waliendelea kubaki nchini Sierra Leone kwa wiki kadhaa kwa shabaha ya kutoa mafunzo kwa jeshi la nchi hiyo.