Jun 30, 2018 08:57 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (57)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 57.

Kwa wale wasikilizaji na wafuatiliaji wa kawaida wa kipindi hiki bila shaka mngali mnakumbuka kuwa katika vipindi kadhaa vilivyopita tumezungumzia chimbuko na malengo ya kuundwa ile iliyokuwa ikijulikana kama Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, ambayo sasa inajulikana kama Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), ikiwa ni moja ya nembo na vielelezo vya kupatikana sauti moja na muelekeo mmoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Katika vipindi hivyo kadhaa tumezungumzia marhala na awamu nne tofauti za historia ilizopitia jumuiya ya OIC katika utendaji wake, ambapo tulibainisha kwamba katika kipindi cha kwanza utambulisho wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ulijikita kwenye lengo tukufu la kadhia ya Palestina na kupelekea kupatikana aina fulani ya umoja na mshikamano baina ya nchi za Kiislamu. Lakini tukafafanua pia kwamba katika awamu ya pili ya umri na harakati za OIC, ambayo inahusiana na kipindi cha baina ya mkutano mkuu wa tatu wa jumuiya hiyo hadi ule uliofanyika mjini Tehran mnamo mwaka 1997, kwa sababu ya mizozo iliyojitokeza kati ya nchi wanachama, aina fulani ya mpasuko na utengano ilishuhudiwa ndani ya jumuiya hiyo na kufifisha mwanga wa matumaini ya kupatikana umoja uliokuwa umejitokeza hapo kabla. Kipindi chetu cha leo kitaendeleza mjadala tulioanza katika kipindi kilichopita kwa kuhakiki na kuchambua hatua muhimu zaidi ilizochukua na harakati ambazo jumuiya hiyo ya nchi za Kiislamu ilizifanya katika vipindi na awamu zilizofuatia.

 

Katika awamu ya pili ya harakati za OIC, ukweli uliokuwa umejificha katika uhusiano wa nchi za Kiislamu ulidhihirika na kuufanya utambulisho wa jumuiya hiyo ukabiliwe na changamoto mpya. Hitilafu na tofauti hizo zilizokuwepo zilifikia kiwango cha kuitenga na kuiweka mbali OIC na malengo na madhumuni ya kuasisiwa kwake na kuibua hali fulani ya utengano kati ya nchi wanachama. Matukio kadhaa yakiwemo ya uvamizi na vita vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, kuuliwa shahidi mahujaji wa Kiirani katika Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu huko Makka na uungaji mkono wa wazi kabisa wa OIC kwa hatua hiyo isiyo ya kiutu iliyofanywa na Saudi Arabia, hatua ya Iraq ya kuivamia kijeshi Kuwait na kulegezwa msimamo katika lengo tukufu la kuikomboa Quds na msingi mkuu wa kuwahami Wapalestina na kuyaunga mkono kwa hali na mali mapambano ya wananchi hao pamoja na kurejeshewa tena Misri kiti chake cha uwanachama wa OIC ni miongoni mwa mambo yaliyozusha hitilafu za ndani baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu; na au kwa lugha ya uwazi zaidi zilidhihirisha na kuweka wazi hitilafu zilizokuwepo kati ya nchi hizo.

Katika hali ambayo matukio ya miaka ya mwanzoni mwa muongo wa 1990 hususan la Iraq kuivamia Kuwait yalikamilisha mduara wa hali ya utengano baina ya nchi za Kiislamu, kukabidhiwa Iran uenyekiti wa OIC kulifungua ukurasa mpya wa uhusiano wa maelewano baina ya nchi wanchama. Mazingira hayo yalijitokeza katika hali ambayo, baada ya kusambaratika na kuvunjika Shirikisho la Kisovieti la Urusi na Kambi ya Mashariki, Marekani iliyobaki kuwa mshindani asiye na mpinzani duniani, ilianza kutafuta mpinzani “mwengine” wa kujaza nafasi ya kambi ya Mashariki, ambaye hakuwa mwingine isipokuwa Ulimwengu wa Kiislamu. Wanafikra watajika kama Samuel Huntington alitangaza nadharia ya Makabiliano ya Staarabu kwa kimombo The Clash of Civilizations, hatua ambayo iliandaa mazingira ya kifikra ya kuibua makabiliano hayo. Kwa mujibu wa nadharia ya Huntington, baada ya kumalizika enzi za Vita Baridi yaani Cold War, dunia ilikuwa imeingia kwenye zama zingine mpya ambazo sifa yake kuu si makabiliano ya kiidiolojia yaliyokuwepo baina ya kambi mbili kuu za Mashariki na Magharibi, bali ni mpambano wa staarabu, ambapo katika mpambano huo makabiliano makuu ni kati ya staarabu mbili za Uislamu na Magharibi.

Umoja huleta mapenzi

 

Japokuwa kimsingi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikukubaliana na nadharia hiyo, lakini iliitumia anga hiyo iliyojitokeza katika uga wa fikra za waliowengi duniani na katika mataifa ya Waislamu kwa ajili ya kuimarisha uhusiano mzuri kati ya nchi za Kiislamu. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo wakati huo, ilikuwa ikishikilia pia uenyekiti wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, mbali na kuchukua msimamo wa kukabiliana na nadharia ya mpambano wa staarabu, ilipendekeza kwa mara ya kwanza katika mkutano wa OIC uliofanyika mjini Tehran, nadharia mbadala ya Mazungumo Baina ya Staarabu. Na baada ya hapo ikaendelea kuitangaza nadharia hiyo hasa kutokana na kupokewa na serikali na mataifa ya ulimwengu na kuwezesha mwaka 2001 kutangazwa na Umoja wa Mataifa kuwa Mwaka wa Mazungumzo Baina ya Staarabu yaani Dialogue Among Civilizations; na kwa njia hiyo kuandaa mazingira mazuri kifikra ya kupatikana sauti moja na muelekeo wa pamoja. Ulipofanyika mkutano wa nane wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu hapa mjini Tehran, na kwa kuzingatia hali halisi ilivyokuwa katika Ulimwengu wa Kiislamu na udharura ambao haukuweza kukanushika wa kuimarisha anga ya mazungumzo na hali ya kuaminiana kati ya nchi za Kiislamu, Rais wa wakati huo wa Iran alitoa pendekezo la kuundwa kamati maalumu ya kufuatilia suala hilo, pendekezo ambalo lilipokelewa kwa uungaji mkono mkubwa wa viongozi wa nchi za Kiislamu.

Kamati hiyo iliweza katika vikao vyake vya utendaji na vya wataalamu kuandaa hati iliyojumuisha misingi mikuu ya ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kati ya nchi za Kiislamu. Kutokana na anga ya hali ya kutoaminiana ambayo ilikuwa kila mara ikisababisha nchi za Kiislamu kutazamana kwa shaka na jicho baya au hata kuvaana kwa vita, kamati hiyo iliweza kuanzisha misingi ya kifikra na kisiasa ya kuleta utengamano na mshikamano wa ndani. Wakati wa kipindi cha uenyekiti wake katika OIC, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilevile iliipa uzito na mazingatio makubwa migogoro iliyokuwepo katika Ulimwengu wa Kiislamu, na kwa mashauriano na maelewano na nchi nyingine wanachama ikaweza kupunguza matatizo ya Ulimwengu wa Kiislamu na kuzidisha utengamano na mshikamano wa ndani ya OIC.

Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya sehemu ya 57 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu umefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumai kuwa mumefaidika na kunufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi chetu cha leo. Basi hadi wiki ijayo inshaallah tutapokutana tena katika sehemu ya 58 ya mfululizo huu nakuageni huku nikikutakieni heri na fanaka maishani…/

 

Tags