Nov 03, 2018 11:16 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (75)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 75 na ya mwisho.

Kwa wafuatiliaji wa kawaida wa kipindi hiki bila shaka mnakumbuka kuwa katika majumuisho tuliyofanya katika sehemu ya 74 ya mifululizo ya kipindi hiki kuhusu uchukuaji hatua za kivitendo za kupatikana umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu, tulisema kuwa, taarifa ya mwishoni mwa mkutano 13 wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) uliofanyika mjini Istanbul, Uturuki ilikuwa kielelezo cha kufikia upeo wa juu kiwango cha hitilafu, utengano na mpasuko kati ya nchi za Kiislamu.

 Baada ya Saudi Arabia kulitumia jeshi la Misri kuiangusha serikali halali iliyochaguliwa na wananchi wa nchi hiyo na kuusaidia utawala wa Aal Khalifa kuyakandamiza mapinduzi ya Waislamu wa Kishia nchini Bahrain iliendeleza hujuma zake kwa kujiingiza kwenye masuala ya ndani ya Yemen na Syria ili kuweza kufikia malengo yake ya kuziweka madarakani tawala vibaraka zenye kutii na kukidhi matakwa yake; hata hivyo iligonga mwamba kutokana na muqawama wa wananchi wa mataifa hayo mawili. Baada ya sakata la maafa ya Mina na kumnyonga Sheikh Nimr Baqir An-Nimr, kiongozi wa Waislamu wa Kishia nchini Saudi Arabia, utawala wa Aal Saud ulikabiliwa na wimbi la mashinikizo ya fikra za waliowengi katika eneo, ndani ya umma wa Kiislamu na katika taasisi za kimataifa. Ni kwa sababu hiyo, ndipo ukaamua kuchukua hatua ya kuvunja uhusiano wake wa kisiasa na Iran ili kujivua na hali ya kutengwa na kufifisha jinai zake dhidi ya dini na dhidi ya binadamu. Lakini pia ikatumia mbinu ya kuzitisha na kuzirubuni nchi za Kiislamu ili kuzichochea zichukue msimamo wa pamoja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia kikao cha 13 cha viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kilichofanyika Istanbul, Uturuki.

 

Katika kikao hicho, nchi ambazo zenyewe zinalihami na kuliunga mkono kundi la kitakfiri la Desh na magaidi wengine katika eneo, zilieneza sumu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa lengo la kuibana isiendeleze sera zake za kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa, wa Palestina, Yemen na Bahrain. Lakini mbali na hilo, kulingana na matakwa ya viongozi wa Saudi Arabia, misimamo ya Iran kuhusiana na adhabu za vifo zilizotekelezwa nchini Saudia ilikosolewa vikali, na raia wa nchi hiyo walionyongwa kinyama, akiwemo kiongozi wa Waislamu wa Kishia Sheikh Nimr Baqir An-Nimr, walitajwa kuwa eti ni "magaidi".

Wapenzi wasikilizaji, bila ya shaka mngali mnakumbuka kuwa baada ya kuuhakiki utendaji wa Jumuiya ya OIC tulieleza kwamba kama tunataka kutathmini mafanikio iliyopata jumuiya hiyo kulingana na malengo na misingi iliyoainishwa kwenye hati ya kuasisiwa kwake, hadi kipindi cha mwaka 2011 ulipoanza Mwamko wa Kiislamu katika nchi za Kiarabu, inapasa tuseme kuwa mafanikio ya OIC katika kipindi chote hicho yalikuwa ya kiwango cha wastani. Ndiyo kusema kwamba Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu haikuweza kuyafikia kikamilifu malengo iliyojiwekea. Kwa ufafanuzi zaidi ni kuwa, katika suala la “kudhamini usalama wa pamoja kwa ajili ya nchi wanachama” ambalo ni moja ya malengo muhimu ya OIC, jumuiya hiyo haina rekodi ya kuridhisha, kwa sababu katika matukio mengi imekuwa na nafasi ya kudhibiti tu hali ya mambo na si kuipatia suluhisho la utatuzi. Katika kufikia lengo la “kutatua tofauti kwa njia za amani” pia Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, si tu haijafanikiwa, lakini katika baadhi ya kadhia imechukua hatua za kushadidisha mzozo, vita na umwagaji damu baina ya nchi wanachama.

Ikiwa Jumuiya ya OIC haijapata mafanikio makubwa katika kufikia malengo yake, ni mambo gani yaliyokwamisha suala hilo? Tukichunguza matukio ya kisiasa ya Ulimwengu wa Kiislamu katika vipindi tofauti tutabaini kuwa moja ya sababu kuu zinazoikwamisha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu kufikia malengo yake ni kutanguliza mbele nchi wanachama maslahi ya kitaifa kuliko maslahi ya pamoja na ya jumuiya. Katika hali ambayo, kimsingi hakuna mtazamo mmoja baina ya nchi za Kiislamu kuhusu ufahamu wao juu ya Uislamu, ukweli ni kwamba kuzingatia manufaa na maslahi yao ya pamoja ndiko kunakoweza kuwa chachu ya kuziunganisha na kuleta umoja kati yao; lakini hata msingi huo pia umedhoofishwa katika jumuiya ya OIC, kiasi kwamba kufadhilisha na kuweka mbele manufaa ya kitaifa badala ya manufaa ya jumuiya na ya pamoja kumesababisha utengano na misimamo kinzani katika stratejia na mikakati ya jumuiya hiyo ya nchi za Kiislamu na kuzusha hitilafu na mfarakano baina ya nchi wanachama.

 

Si hayo tu, lakini pia kutawala mielekeo na misimamo ya kufurutu mpaka katika fikra na mienendo ya nchi za Kiislamu kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine kufanya mapatano na adui mkuu na wa pamoja wa umma wa Kiislamu, yaani Israel, vimekuwa na taathira kubwa katika kuleta mfarakano ndani ya OIC. Tukiipitia historia tutagundua kuwa, katika vipindi ambavyo kumekuwepo na aina fulani ya utumiaji busara ya kutekeleza mambo kiwastani na kwa kufuata misingi na usuli baina ya nchi wanachama wa OIC na kutilia mkazo utambulisho wa asili wa jumuiya hiyo, yaani kuzingatia malengo matukufu ya Palestina, hali ya utangamano na mshikamano imeongezeka baina ya nchi za Kiislamu. Muelekeo huu uko mkabala na dhidi ya harakati nyingine mbili ambazo daima zimekuwa zikivuruga umoja na mshikamano wa Ulimwengu wa Kiislamu. Ya kwanza ni ya tapo la misimamo ya kufurutu mpaka katika kuamiliana na dunia nzima kupitia makundi kama Taliban; na ya pili ni ya wafanya mapatano na maadui hususan Israel. Bila ya shaka kuwekwa kando harakati mbili hizo na kupata nguvu ndani ya OIC mrengo wa mmea huo wa misimamo ya busara na wastani na wenye itikadi ya msingi wa muqawama wa kukabiliana na Israel kutawezesha kuongezeka hamu ya kuleta umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu na ndani ya jumuiya yenyewe, na kutoa fursa kwa viongozi wa nchi za Kiislamu ya kutumia uwezo na fursa hizo kwa ajili ya kuleta umoja na mshikamano zaidi, sambamba na kutumia suhula zilizoko katika OIC ili kuweza kufikia lengo hilo.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 75 na ya mwisho ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Ni matumani yangu kuwa mumenufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi chetu hiki huku tukiwa na matarajio ya kushuhudia baada ya muda si mrefu katika siku za usoni mwisho wa mifarakano, ugomvi, vita na utengano baina ya nchi za Kiislamu; na badala yake kupatikana umoja na mshikamano kwa ajili ya kuhuisha na kurejesha izza, adhama na heshima ya Waislamu duniani. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

Tags