Nov 03, 2018 11:11 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (74)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 74.

Kwa wasikilizaji wa kawaida wa kipindi hiki bila ya shaka mngali mnakumbuka kuwa katika vipindi viwili vilivyopita vya majumuisho ya kipindi chetu cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu, tumezungumzia uga wa nadharia wa suala la umoja wa Kiislamu na tukabainisha kwamba umoja ni mafundisho ya msingi katika dini ya Uislamu na kwamba wanafikra na warekebishaji umma wengi wa Kishia na Kisuni wametilia mkazo ulazima wa Waislamu kuungana na kuwa wamoja kwa ajili ya kukabiliana na hujuma na njama za maajinabi na kufufua hadhi na adhama ya umma wa Kiislamu duniani. Kama nilivyokuahidini katika kipindi kilichopita, katika kipindi chetu cha leo tutaugeukia upande wa pili wa suala hilo, yaani uga wa uchukuaji hatua za kivitendo. Kuhusiana na hilo tutazungumzia uundwaji wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, ambayo ni kielelezo muhimu na mfano hai zaidi wa kupatikana msimamo na sauti moja kati ya nchi za Kiislamu, ili kuona ni kwa kiwango gani OIC imeweza kuondoa mifarakano na utengano baina ya Waislamu na kuwafungulia njia ya kufikia kwenye umoja na mshikamano wa Kiislamu.

Tulieleza huko nyuma kwamba kilipoanza kipindi cha nusu ya pili ya karne ya 20, viongozi wa nchi za Kiislamu walihisi, kuna haja na udharura wa kuanzisha jumuiya ambayo itaweza kujenga umma mmoja kutokana na majimui ya nchi zaidi ya 50 za Kiislamu; na badala ya mifarakano na utengano, kuleta umoja na mshikamano baina ya nchi hizo. Lakini kitu ambacho kilikuwa ndio chachu ya kuasisiwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, OIC ni tukio lililojiri mwaka 1969 la kuchomwa moto msikiti mtukufu wa Al-Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu duniani.

Shikamaneni nyote na kamba moja ya Mwenyezi Mungu na wala msifarikiane

 

Hujuma hiyo ambayo ilifanywa na Myahudi mmoja mwenye taasubi, iliamsha hasira za Waislamu duniani. Utawala wa Kizayuni wa Israel ulimhusisha mtalii mmoja kutoka Australia na tukio hilo la kuchomwa moto msikiti wa Al-Aqsa, na katika kuendesha kesi yake, mahakama ya utawala huo ikadai kwamba, wakati alipofanya jinai hiyo, mtalii huyo Muaustralia alikuwa na matatizo ya akili; na kwa mujibu wa sheria za ndani ya Israel hawezi kuhukumiwa. Suala hilo liliwaghadhibisha Waislamu duniani; na ili kutoa jibu maridhawa kwa malalamiko ya umma, viongozi wa mataifa ya Kiislamu waliufikisha kwa walimwengu wito wa malalamiko na hasira za Waislamu. Katika zama hizo, Saudi Arabia na Morocco zilikuwa miongoni mwa nchi zilizofanya juhudi kubwa za kuwezesha kuitishwa kikao cha kujadili suala hilo, na hatimaye mnamo mwezi Septemba mwaka 1969, kikao hicho kilifanyika katika mji mkuu wa Morocco, Rabat na hivyo ndivyo ilivyoundwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, OIC ambayo baadaye ilibadilishwa jina na kuitwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu.

Umri wa jumuiya ya OIC unaweza kugawanywa katika vipindi au awamu nne kuu. Awamu ya kwanza ni ya muongo wa kuasisiwa jumuiya hiyo. Sifa muhimu zaidi iliyokuwa nayo Jumuiya ya Nchi za Kiislamu katika kipindi hicho ilikuwa ni kujengeka utambulisho wake kwa kujikita kwenye lengo tukufu la Palestina. Awamu ya pili ya umri wa jumuiya ya OIC ni ya kipindi cha mkutano wa tatu hadi ulipofanyika mkutano wa nane wa jumuiya hiyo mwaka 1997 hapa mjini Tehran ambayo inajumuisha vipindi kadhaa vilivyoshuhudia mabadiliko katika Ulimwengu wa Kiislamu, ambapo kutokana na mizozo na migogoro iliyozuka baina ya nchi wanachama, hali fulani ya mgawanyiko na utengano ilijitokeza ndani ya jumuiya ya OIC na kufifisha nuru ya mwanga wa matumaini ya kupatikana umoja iliyokuwa imejitokeza hapo kabla. Kwa hakika tunaweza kusema kuwa hitilafu na tofauti kati ya nchi za Kiislamu zilishtadi na kupamba moto katika kipindi hicho na katika baadhi ya matukio kupelekea kuzuka mizozo na mapigano kati yao. Mbali na mizozo ya kisiasa na kijeshi, kulijitokeza pia namna fulani ya makabiliano ya kifikra na kiitikadi baina ya mirengo ya ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu, ambapo Jumuiya ya OIC sio tu haikufanikiwa kuyazima lakini wakati mwengine, yenyewe ilisababisha pia kushadidi mizozo hiyo. Uvamizi wa kijeshi wa Iraq dhidi ya Iran mwaka 1980 na uvamizi wa Iraq pia dhidi ya Kuwait mwaka 1990 ni mifano muhimu zaidi ya hali hiyo.

 

Awamu ya tatu ya umri wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ilianza sambamba na Iran kukabidhiwa uenyekiti wa jumuiya na kufunguliwa ukurasa mpya katika uhusiano wa kiumoja baina ya nchi wanachama. Mazingira hayo mwafaka yalijitokeza katika hali ambayo, baada ya kusambaratika na kuvunjika Shirikisho la Kisovieti la Urusi na Kambi ya Mashariki, Marekani iliyobaki kuwa mshindani asiye na mpinzani duniani, ilianza kutafuta mpinzani “mwengine” wa kujaza nafasi ya kambi ya Mashariki, ambaye kwa mtazamo wake, hakuwa mwingine isipokuwa Ulimwengu wa Kiislamu. Japokuwa kimsingi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikukubaliana na nadharia hiyo, lakini iliitumia anga hiyo iliyojitokeza katika uga wa fikra za waliowengi duniani na katika mataifa ya Waislamu kwa ajili ya kuimarisha uhusiano mzuri kati ya nchi za Kiislamu. Wakati wa kipindi cha uenyekiti wake katika OIC, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliipa uzito na mazingatio makubwa migogoro iliyokuwepo katika Ulimwengu wa Kiislamu, na kwa mashauriano na maelewano na nchi nyingine wanachama kwa upande mmoja, na kwa upande mwengine kwa kushauriana na jumuiya za kimataifa na mataifa mengine, ikaweza kupunguza matatizo ya Ulimwengu wa Kiislamu na kuzidisha utengamano na mshikamano wa ndani ya OIC. Mwenendo chanya wa matukio ya kuleta mshikamano, muelekeo mmoja na sauti moja baina ya nchi wanachama wa OIC uliendelea pia baada ya kikao cha Tehran. Wakati wa tukio la Septemba 11 mwaka 2001 na kushambuliwa majengo pacha katika mji wa NewYork, Marekani, japokuwa tukio hilo liliibua uhasama na uadui usio na sababu dhidi ya Ulimwengu wa Kiislamu, lakini kwa namna fulani lilipelekea pia kupatikana umoja na mshikamano kati ya nchi za Kiislamu.

Na kipindi cha nne cha umri wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu kinahusiana na wakati nchi nyingi zenye tawala za kiimla na kidikteta zilipochukua hatua ya kukabiliana na matukio yaliyojulikana kama Mwamko wa Kiislamu, ulioanza mwaka 2011 nchini Tunisia na kuenea katika nchi zingine, ambapo mifarakano na utengano ulishamiri katika Ulimwengu wa Kiislamu na baina ya nchi wanachama wa OIC. Taarifa ya mwishoni mwa mkutano uliofanyika Istanbul, Uturuki inadhihirisha kufikia upeo wa juu kiwango cha hitilafu hizo.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 74 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Inshallah tutakutana wiki ijayo katika siku na saa kama ya leo ili kukuleteeni sehemu ya 75 na ya mwisho ya kipindi hiki. Basi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri la maishani…/

Tags