Nov 03, 2018 10:59 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (72)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 72.

Kwa wale wasikilizaji wetu wanaofuatilia kwa karibu kipindi chetu hiki, bila shaka mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita, ambacho ni sehemu ya kwanza ya majumuisho ya yale tuliyozungumzia katika mifululizo 71 ya kipindi hiki, tulieleza kwamba  licha ya jitihada na hatua za uelimishaji zilizochukuliwa na warekebishaji umma wa Kiislamu, hususan wanafikra mashuhuri kama Sayyid Jamaluddin Asad Abadi, Iqbal Lahore na Imam Khomeini (RA), kwa kutilia mkazo udharura wa kuzinduka Ulimwengu wa Kiislamu na kuwepo umoja baina ya nchi za Kiislamu kwa kuzingatia misingi na usuli, itikadi  madhubuti za dini yao na masuala yanayowaunganisha pamoja kama imani yao juu ya Mungu mmoja pekee, yaani Tauhidi, Utume wa Nabii Muhammad SAW, Qur’ani moja iliyohifadhika na kuongezwa au kupunguzwa chochote na pia kibla chao cha pamoja, la kusikitisha ni kwamba, hadi sasa Ulimwengu wa Kiislamu haujaweza kuchukua hatua za dhati kwa ajili ya kuleta umoja na mshikamano; na ndiyo maana Waislamu wengi wanateseka na kutaabika kwa ufakiri na ukata wa kiuchumi, kwa kuwa na nafasi duni kisiasa katika uga wa kimataifa na pia kwa kuandamwa na matatizo na masaibu mbalimbali yanayosababishwa na uingiliaji wa kisiasa na kijeshi wa madola yenye nguvu.

 

Lakini katika zama hizi, suala la Umoja wa Kiislamu limekuwa na mfungamano wa ajabu na kadhia ya Ukoloni. Ushahidi wa historia unaonyesha kuwa, japokuwa kuingia kwa ukoloni katika Ulimwengu wa Kiislamu kulishadidisha mifarakano na utengano baina ya nchi za Kiislamu, lakini pia kuliandaa mazingira ya kuchukuliwa baadhi ya hatua chanya kwa ajili ya kuleta umoja. Katika hatua walizochukua kukabiliana na kukoloniwa nchi za Kiislamu na madola ya kikoloni, maulamaa wa dini, wanafikra na warekebishaji umma wa Ulimwengu wa Kiislamu, wakiwemo wa Kishia na Kisuni, si tu walibainisha mambo yanayowatenganisha na kuwafarakanisha Waislamu, lakini pia walipendekeza njia za kuufufua umoja wa kufikia kiwango cha ndoto na matarajio ya zama za mwanzoni mwa Uislamu. Sayyid Jamaluddin Asad Abadi ni shakhsia wa kwanza na muhimu zaidi miongoni mwa waleta mageuzi na kulingania umoja wa Kiislamu katika karne za karibuni. Katika zama zake, mwanafikra huyo alisimama kuyaamsha na kuyazindua mataifa ya Ulimwengu wa Mashariki na ya Waislamu, ambapo Iran, utawala wa Othmaniyya na India zilikuwa zikikabiliwa na hujuma za kisiasa na kijeshi na hatari ya kuvamiwa na kukaliwa na madola ya Ulaya kama Urusi, Uingereza na Ufaransa; na mataifa mengine ya Waislamu yalikuwa kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja yakidhibitiwa na kukoloniwa na madola ya Magharibi yakiongozwa na madola hayo matatu tuliyoyataja.

Baada ya kuchunguza sababu za kuwa dhaifu nchi za Kiislamu na vizuizi vya umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu, Sayyid Jamaluddin alikuwa akisisitiza kwamba, kurejea Waislamu kwenye Uislamu wa asili, kuondoa khurafa katika imani na itikadi za dini, kuachana na akhlaqi potofu, kushikamana na akhlaqi na mwenendo wa kidini na kiutu, kuweka kando tofauti za kikaumu, kimadhehebu na kitaifa, kuanzisha mapambano dhidi ya watawala madikteta, kuwa na sauti wananchi katika maamuzi ya kisiasa, kufanya jitihada za kupiga hatua kimaendeleo na kufikia ustawi wa kielimu na kuhuishwa utambulisho wa Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na ukoloni wa Magharibi, ndiyo siri ya kupata maendeleo na nguvu nchi za Kiislamu na njia ya kupatikana umoja wa kukabiliana na ukoloni wa Magharibi. Sheikh Muhammad Abdou, naye pia kama alivyokuwa Sayyid Jamaluddin Asad Abadi, alikuwa akiamini kwamba, moja ya sababu kuu za kuwepo mfarakano na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu ni mpasuko wa kimadhehebu baina ya Shia na Suni; kwa hivyo alijitahidi, kwa kuandika sherhe ya Nahjul-Balaghah, kubuni mkakati wa kuleta umoja wa Kiislamu kwa njia ya kutatua hitilafu na tofauti za kimadhehebu kati ya Shia na Suni. Katika nadharia aliyobuni ya umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu, Sheikh Muhammad Abdou, alitilia mkazo misingi mitatu mikuu: Wa kwanza ni ulazima wa kuwepo mlingano baina ya akili na dini katika Uislamu. Pili ni udharura wa kuwepo Ijtihadi katika masuala ya kidini kwa kutegemea msingi wa Tauhidi na kuzingatia akili na mahitaji ya zama. Na tatu ni kufungamanisha uhuru na irada ya mtu sambamba na kukubali jukumu na masuulia.

Rashid Ridha, Iqbal Lahore, Kawakibi na wanafikra wengine wengi wa Kisuni, waliendeleza fikra na nadharia ya umoja wa Kiislamu kwa kufuata mitazamo ya Sayyid Jamaluddin na Sheikh Muhammad Abdou; lakini kwa upande wa maulamaa wa Kishia, nao pia wamefanya jitihada kubwa za kubainisha sababu za utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu sambamba na kupendekeza njia kadhaa za kujivua na hali hiyo. Licha ya dhulma mbalimbali walizofanyiwa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika zama tofauti za historia, Waislamu hao wamekuwa siku zote wakipigania umoja baina ya Waislamu; na maulamaa na wanafikra wa Kishia wa zama zote wamejitahidi, kwa kushirikiana na wanafikra wa Kisuni, kutatua baadhi ya masuala yanayochochea mifarakano, na badala yake kuimarisha umoja kati ya Shia na Suni. Ayatollah Bourujerdi, Allamah Amini, Imam Khomeini na Ayatullah Khamenei ni miongoni mwa viongozi na wanafikra wa Kishia ambao katika uga wa nadharia na kivitendo pia wameifanyia kazi na kuitekeleza fikra ya kuleta umoja wa Kiislamu.

 

Ayatullah Al-Udhma Bourujerdi, ni miongoni mwa marjaa taqlidi na ulamaa mkubwa wa ulimwengu wa Kishia ambaye alikuwa kila mara akilipa umuhimu na mazingatio makubwa suala la umoja wa Waislamu na kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu. Yeye alikuwa akiitakidi kwamba masuala ya kifqhi yasijadiliwe katika madhehebu za Shia Imamiyyah pekee, bali wigo wake upanuliwe mpaka kwenye madhehebu zote za fiqhi ya Kiislamu na kulinganishwa hoja za madhehebu zote katika kila suala muhimu zinalohitilafiana. Ayatullah Bourujerdi alikuwa mmoja wa waungaji mkono wakuu wa fikra ya kuanzisha jopo la kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu. Mtazamo wa kukurubisha pamoja madhehebu aliokuwa nao alimu huyo mkubwa wa Kiislamu ulikuwa na taathira kubwa katika kujenga maelewano baina yake na Sheikh Mahmoud Shaltut, mufti mkuu wa Misri na Shekhe Mkuu wa Al-Azhar kwa lengo la kupatikana muelekeo mmoja wa Waislamu na kubuni mikakati ya kinadharia kwa ajili ya umoja wa Kiislamu. Ilikuwa ni kutokana na muelekeo huo, ndipo Sheikh Shaltut akatoa fatua yake muhimu na mashuhuri inayojuzisha wafuasi wa madhehebu nne za Kisuni kufuata madhehebu nyingine ikiwemo ya Shia Ithnaasharia; kwa maana ya kufuata hukumu za kifiqhi zinazotolewa na mafaqihi wa madhehebu hizo.

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kuishia hapa nikitumai kuwa mumenufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi chetu cha leo. Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo inshaallah, katika siku na saa kama ya leo katika sehemu ya 73 ya mfululizo huu, nakuageni, huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu…/

Tags