Nov 03, 2018 11:03 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (73)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 73.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu kipindi chetu hiki bila shaka mngali mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulisema, licha ya dhulma mbalimbali walizofanyiwa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika zama tofauti za historia, Waislamu hao wamekuwa siku zote wakipigania umoja baina ya Waislamu; na maulamaa na wanafikra wa Kishia wa zama zote wamejitahidi, kwa kushirikiana na wanafikra wa Kisuni, kutatua baadhi ya masuala yanayochochea mifarakano, na badala yake kuimarisha umoja kati ya Shia na Suni. Ayatullah Bourujerdi, Allamah Amini, Imam Khomeini na Ayatullah Khamenei ni miongoni mwa viongozi na wanafikra wa Kishia ambao katika uga wa nadharia na kivitendo pia wameifanyia kazi na kuitekeleza fikra ya kuleta umoja wa Kiislamu.

Imam Khomeini (RA), kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, naye pia alifuatilia kinadharia na kivitendo fikra na mkakati wa kuleta umoja wa Kiislamu. Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, umoja wa Waislamu ni suala la kimkakati na kistratejia na kwa sababu hiyo alibuni mikakati ya kivitendo ili kufikia umoja wa Kiislamu. Mikakati hiyo ni ya awamu mbili, wa kwanza ni "mkakati wa kiutamaduni na kiitikadi" na wa pili ni "mkakati wa kisiasa na kivitendo".  Kutokana na uelewa wa kiuhalisia na wa pande zote aliokuwa nao kuhusu matatizo ya kifikra na kiakhlaqi ya jamii za Kiislamu na serikali zinazotawala mataifa ya Waislamu, ili kuweza kufikia lengo la umoja wa umma wa Kiislamu na kupatikana umma mkubwa wa Uislamu, Imam Khomeini aliamua kabla ya jambo lolote lile, kushughulikia kwanza urekebishaji wa imani za kidini na kisiasa za Waislamu na kupendekeza waungane na kushikamana na mhimili mmoja wa Uislamu halisi wa asili. Imam Khomeini anaitakidi kuwa utengano na mfarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu sababu yake ni serikali na wananchi wa mataifa ya Waislamu kujiweka mbali na mafundisho ya wahyi ya Uislamu na badala yake kutegemea madola ya kiistikbari ya Magharibi na Mashariki. Kwa hivyo njia pekee ya kuondokana na masaibu hayo ni kurejea kwenye nukta tatu muhimu na za msingi, ambazo ni Uislamu, Uhuru na Kujitawala, kwa sababu kwa mtazamo wa mrekebishaji umma huyo, kurejea kwenye nukta tatu hizo kutawawezesha kuujenga tena upya utambulisho wao wa Kiislamu uliosahaulika.

 

Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, kuchukua hatua maulamaa, wataalamishaji, viongozi na wale walioko mstari wa mbele katika masuala ya kifikra, kidini na kitaifa, za kupanua na kuimarisha vyombo vya tablighi na uenezi na vilevile kuanzisha vuguvugu la Hizbullah na Hizbul-Mustadh'afin katika upeo wa Ulimwengu wa Kiislamu na ulimwengu mzima kwa ujumla ni miongoni mwa mikakati na stratejia za utekelezaji ili kuweza kupatikana umoja baina ya Waislamu.

Ayatullah Khamenei, kiongozi wa sasa wa Mapinduzi ya Kiislamu, yeye pia anaitakidi kuwa umoja wa Kiislamu ni hitajio muhimu zaidi kwa Waislamu katika dunia ya leo. Katika kuelezea maana ya umoja, Ayatullah Khamenei hakubaliani na mtazamo usioendana na uhalisia wa mambo unaotilia mkazo umoja kwa msingi wa kuweka kando hitilafu na tofauti za kifikra na kihistoria zilizopo baina ya madhehebu tofauti za Kiislamu na kusisitiza kwamba, tafsiri hiyo ya umoja haimaanishi kuwa na muelekeo na mtazamo mmoja Waislamu katika kukabiliana na maadui wa nje. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameivunja hoja ya watu wanaotumia kisingizio cha kuleta umoja kwa lengo la kuzuia na kuzima mijadala baina ya madhehebu za Kiislamu kwa kueleza kwamba: Umoja baina ya Waislamu maana yake si kuweka kando mitazamo tofauti ya kiitikadi. Ilivyo hasa, inapasa kuwepo na mijadala ya kitaaluma baina ya maulamaa wa madhehebu; isipokuwa midahalo hiyo isiwe na hali ya kihasama; bali mara zote ifanyike kwa ujengaji hoja; na miongozo mikuu ya midahalo ya aina hiyo inapasa iwe Qur'ani na Mtume wa Allah pamoja na akili ya burhani. Na sababu yake ni kwamba Qur'ani tukufu yenyewe pia imelingania kutumia akili. Kwa hivyo haiwezekani kutumia kisingizio cha kulinda umoja ili kuzima mijadala ya kimadhehebu; wala haiwezekani kutumia kisingizio cha mijadala ya aina hiyo kuutia doa umoja.

Umoja wa Kiislamu

 

Ayatullah Khamenei anasisitiza kuwa mfarakano ni sumu hatari na angamizi kwa Ulimwengu wa Kiislamu na anaamini kwamba mikono michafu ya wakoloni wenye nia ya kupora maliasili na utajiri wa nchi za Kiislamu ndiyo inayochochea hitilafu na mifarakano hiyo. Kwa mtazamo wa Ayatullah Khamenei, uadui wa maajinabi kwa Mashia na Masuni unafanywa kwa madhumuni ya kufikia lengo moja, ambalo ni kukabiliana na Uislamu wenyewe. Na ndiyo maana anatanabahisha na kusisitiza kuwa hatua za kutusiana na kuvunjiana heshima zinazofanywa na baadhi ya mapote ya Kishia na Kisuni zinalenga kufanikisha malengo ya maadui wa dini hiyo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anayaasa matapo yote mawili na kuyataka yajihadhari na kujiingiza kwenye masuala hayo kwa kusema: "Suni na Shia kila moja wana hafla zao za kimadhehebu, desturi zao, ada zao na majukumu yao ya kidini wanayotekeleza na inapasa wayatekeleze; lakini mstari mwekundu ni kwamba haifai abadani kusemwa kitu cha kusababisha wao kutengana kwa sababu ya hatua za kuyatusi matukufu ya upande mmojawapo, iwe inayochukuliwa na baadhi ya Mashia kwa sababu ya kujisahau, au inayochukuliwa pia na baadhi ya Masuni kama Masalafi na mfano wao kutokana na kujisahau. Hili ndilo jambo analotaka adui. Hapa pia inapasa kuwepo na umakini".

Wapenzi wasikilizaji, sehemu 73 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Ni matumaini yangu kuwa mumenufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi chetu cha leo. Kama nilivyokuahidini, katika sehemu ijayo ya 74 ya kipindi hiki tutakuja kufanya majumuisho na hitimisho la yale tuliyozungumza katika mifululizo yote iliyopita kwa kuashiria suala la umoja na mshikamano wa Kiislamu katika uga wa uchukuaji hatua za kivitendo. Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani…/

Tags