Kukanushwa madai ya Israeli na serikali ya Uturuki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i111680-kukanushwa_madai_ya_israeli_na_serikali_ya_uturuki
Kufuatia kufichuliwa kufutwa vikwazo vya kiuchumi na kibiashara vya Uturuki dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Israel, mivutano kati ya pande hizo mbili imeshtadi katika vyombo vya habari vya eneo na kimataifa.
(last modified 2024-05-12T07:00:17+00:00 )
May 12, 2024 07:00 UTC
  • Kukanushwa madai ya Israeli na serikali ya Uturuki

Kufuatia kufichuliwa kufutwa vikwazo vya kiuchumi na kibiashara vya Uturuki dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Israel, mivutano kati ya pande hizo mbili imeshtadi katika vyombo vya habari vya eneo na kimataifa.

Omer Bolat, Waziri wa Biashara wa Uturuki amesema kuhusiana na madai hayo ya Israel kuwa kupunguzwa vikwazo vya kibiashara vya Ankara dhidi ya utawala huo wa kibaguzi ni ndoto tu na wala hayana ukweli  wowote. Kwa kuchapisha taarifa kwenye mitandao ya kijamii, Omar Bolat amesema kauli ya Israel Katz, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel ni  uongo mtupu usio na ikweli wowote. Israel Katz alisema hivi karibuni kuwa, serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki imefuta vikwazo vingi vya nchi hiyo dhidi ya Israel. Iwapo madai ya utawala wa kibaguzi wa Israel ni ya kweli, tunaweza kusema kuwa serikali ya Erdogan inatekeleza siasa za kundumakuwili katika biashara yake na utawala huo ghasibu. Hii ni licha ya ukweli kwamba mnamo Januari 2009, Tayyip Erdoğan ambaye kipindi hicho alikuwa Waziri Mkuu wa Uturuki alimhutubu Shimon Peres aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israeli wakati huo katika mkutano wa Davos nchini Uswizi kwa kumwambia: "Nyinyi ni wauaji wazuri."

Maandamano ya wananchi wa Uturuki dhidi ya utawala wa Kizayuni

Inafaa kusema kuwa tarehe 9 Aprili mwaka huu, Wizara ya Biashara ya Uturuki iliweka vikwazo kwa aina 54 za bidhaa za kibiashara dhidi ya Israel. Bidhaa hizo ni pamoja na vifaa vya ujenzi, viwandani na bidhaa za chuma, ambazo katika maandamano ya viongozi wa vyama vya Uturuki  na  wananchi katika miji mbalimbali ya nchi hiyo, waliitaka serikali ya Erdogan ijiepushe kuzipeleka Israel, bidhaa ambazo zinazotumika katika utengenezaji wa mabomu na silaha za maangamizi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina. Kufuatia hatua hiyo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala wa Kizayuni aliandika katika ukurasa wake wa X kwamba serikali ya Erdogan imeondoa vikwazo vingi vya kibiashara dhidi ya Israel. Pamoja na hayo, utekelezwaji wa siasa zisizoeleweka na zisizo na uwazi na maafisa wa serikali ya Ankara, umepelekea wataalamu wengi na viongozi wa vyama vya Uturuki kuzikejeli na kuwatuhumu viongozi wa serikali ya Ankara kuwa wanatumia vibaya matukio muhimu ya kikanda kujinufaisha kisiasa. Mustafa Kara Alioglu mchambuzi na mwandishi wa Kituruki anasema kuhusiana na jambo hilo kuwa: "Kugeuzwa suala la Gaza kuwa suala la kampeni za uchaguzi za chama tawala ni kitendo cha kusikitisha na siasa hizo zinawaharibia jina wanasiasa wanaotawala nchini Uturuki."

Meli za usafirishaji bidhaa

Bidhaa muhimu zaidi ambazo serikali ya Recep Tayyip Erdogan inasafirisha Israeli ni mafuta ghafi. Jamhuri ya Azerbaijan ambayo ni mwitifaki wa karibu wa serikali ya Erdogan nchini Uturuki, ina uhusiano wa karibu sana na utawala wa kibaguzi wa Israel. Kwa hakika, mafuta mengi yanayohitajika na Israel yanadhaminiwa na serikali ya Rais Ilham Aliyev. Serikali ya Erdoğan pia inakidhi mahitaji ya viwanda vya kutengeneza silaha za mauaji ya umati za Israel. Viongozi wa vyama vya Uturuki na wananchi Waislamu wa nchi hiyo wameitaka serikali ya Ankara kupiga marufuku usafirishaji wa mafuta ghafi kwa utawala wa Israel, lakini serikali bado inapeleka bidhaa hiyo ya kistratijia kwa Israel. Hii ni katika hali ambayo, mataifa ya Kiislamu na mengine mengi yasiyo ya Kiislamu na hata idadi kubwa ya Mayahudi wanaoishi Marekani na Ulaya wanatilia mkazo kufutwa utawala huo katili na wa kibaguzi wa Israel. Jambo la kusikitisha ni kuona kuwa baadhi ya serikali za Kiislamu na wanachama wa Jumuiya za Kiislamu bado wanaendelea kuupa utawala huo wa Kizayuni bidhaa na misaada muhimu na hivyo kuwapa nguvu watawala wa kikatili wa Israel kuendelea kuwaua kwa umati Waislamu. Viongozi wa kundi hili la nchi za Kiislamu hata wamewapa kisogo raia wao wakidhani kwamba urafiki wao na utawala wa kibaguzi wa Israel unaweza kuwadhaminia malengo yao ya muda mrefu ya kuendelea kusalia madarakani.

Kwa ujumla tunapasa kusema kuwa kwa kuzingatia kufichuliwa sera za nyuma ya pazia za serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na utawala wa Kizayuni, inatarajiwa kuwa wanasiasa wa Ankara watajitenga na utawala huo wa kibaguzi wa Israel kwa maslahi ya umma wa Kiislamu. Kwa hakika, kukatwa mishipa ya kibiashara na kiuchumi ya utawala wa Kizayuni kunaweza kuboresha na kufikiwa haraka na inavyotarajiwa matakwa ya mataifa ya Kiislamu na hata ya Mayahudi halisi duniani kote.