Iran: Israel haijawahi kutengwa kiasi hiki katika historia yake bandia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i111664-iran_israel_haijawahi_kutengwa_kiasi_hiki_katika_historia_yake_bandia
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria hatua ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA ya kupasisha rasimu ya azimio la kutaka kutazamwa upya suala la taifa la Palestina kupewa uanachama kamili katika umoja huo na kusema kuwa, utawala haramu wa Israel haujawahi kutengwa kwa kiwango kikubwa kama cha sasa katika historia yake bandia.
(last modified 2024-05-11T23:40:10+00:00 )
May 11, 2024 23:40 UTC
  • Iran: Israel haijawahi kutengwa kiasi hiki katika historia yake bandia

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria hatua ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA ya kupasisha rasimu ya azimio la kutaka kutazamwa upya suala la taifa la Palestina kupewa uanachama kamili katika umoja huo na kusema kuwa, utawala haramu wa Israel haujawahi kutengwa kwa kiwango kikubwa kama cha sasa katika historia yake bandia.

Nasser Kan'ani amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X jana Jumamosi na kuongeza kuwa: Uungaji mkono wa kishindo wa jamii ya kimataifa wa kupewa Palestina uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa ni ishara ya wazi ya kutengwa kikamilifu utawala wa Kizayuni na Marekani.

Ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha na inaunga mkono kikamilifu suala la Palestina kupewa uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa.

Kan'ani amesema serikali ya Marekani imetengwa na kuachwa katika njia panda na hata wananchi wenyewe wa nchi hiyo, kwa kuuunga mkono kipofu utawala wa Kizayuni wa Israel.

Juzi Ijumaa, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) hatimaye liliipigia kura ya ndio rasimu ya uanachama kamili wa Palestina katika umoja huo baada ya Marekani kukwamisha suala hilo kwa miaka kadhaa.

Rasimu ya azimio la kuunga mkono uanachama kamili wa Palestina katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambayo imepasishwa kwa kura 143 za ndio, 9 za hapana na nchi 25 zikijizuia kupiga kura inaipatia Palestina haki na mafao zaidi katika Umoja wa Mataifa. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa, uungaji mkono wa hali na mali wa Marekani kwa jinai za utawala mtenda jinai wa Israel katika Ukanda wa Gaza unafanyika wakati huu ambapo jamii ya kimataifa kwa sauti moja imetengaza bayana kusimama na wananchi madhulumu wa Palestina.