Tahadhari kuhusu uwepo wa wanajeshi wa Marekani na Ufaransa nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i111656-tahadhari_kuhusu_uwepo_wa_wanajeshi_wa_marekani_na_ufaransa_nchini_nigeria
Msemaji wa kundi la viongozi wa kaskazini mwa Nigeria amemuonya rais wa nchi hiyo kuhusu madhara hatari ya kuwepo kwa wanajeshi wa Marekani na Ufaransa nchini Nigeria.
(last modified 2024-05-12T02:35:54+00:00 )
May 12, 2024 02:35 UTC

Msemaji wa kundi la viongozi wa kaskazini mwa Nigeria amemuonya rais wa nchi hiyo kuhusu madhara hatari ya kuwepo kwa wanajeshi wa Marekani na Ufaransa nchini Nigeria.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na shirika la habari la Iran Press mjini Abuja, Jabrin Ibrahim, amesema kuhusu madhara ya uwezekano wa kuwepo wanajeshi wa Marekani au Ufaransa nchini Nigeria kwamba, akiwa mzalendo, ana wasiwasi kuhusu mazungumzo kati ya Marekani na Ufaransa na serikali ya Nigeria juu ya kuanzisha kambi za kijeshi katika nchi hiyo, kwa sababu uwepo wa vikosi vya majeshi ya kigeni ni hatari kwa uhuru na kujitawala Nigeria.

Jabrin Ibrahim ameongeza kuwa: Uzoefu wa uwepo wa vikosi vya majeshi ya Marekani na Ufaransa nchini Niger na katika baadhi ya nchi za Kiafrika kama Mali na Burkina Faso, unaonyesha kuwa, licha ya kuwepo vikosi hivyo, ugaidi haukutoweka, bali umeongezeka zaidi; hivyo Rais wa Nigeria haipaswi kuruhusu kuwepo majeshi ya Marekani na Ufaransa katika ardhi ya nchi yake, kwa sababu hakuna thamani wala manufaa.

Msemaji wa kundi la viongozi wa kaskazini mwa Nigeria pia amesema: Serikali za Niger, Burkina Faso na Mali hazikuruhusiwa kufuatilia yaliyokuwa yakijiri katika kambi za kijeshi za kigeni na mipango yao katika nchi hizo, na kurudiwa uzoefu huu nchini Nigeria itakuwa changamoto kubwa kwa mamlaka ya kujitawala.

Wanajeshi wa Ufaransa wakiondoka Niger

Itakumbukwa kuwa majeshi ya Marekani na Ufaransa yamelazimishwa kuondoka katika nchi Niger, Burkina Faso na Mali kutokana na maandamano makubwa yaliyofanywa na wananchi na maamuzi ya serikali mpya zilizotwaa madaraka katika nchi hizo za Magharibi mwa Afrika.