Oct 16, 2018 02:39 UTC
  • Jumanne,  16 Oktoba, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 6 Safar 1440 Hijria sawa na Oktoba 16, mwaka 2018.

Katika siku kama ya leo miaka 806 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa, mnajimu na tabibu mashuhuri wa Kiislamu Qutbuddin Mahmoud Shirazi katika mji wa Shiraz nchini Iran. Alianza kujifunza tiba akiwa bado mdogo na alianza kutibu wagonjwa katika moja ya hospitali za Shiraz baada ya kufariki dunia baba yake. Katika kipindi cha miaka kumi ya kazi ya utabibu, Qutbuddin Shirazi alitalii vitabi mbalimbali vya tabibu mwingine wa Kiislamu Bin Sina na vitabu vingine vya tiba na falfasa. Baada ya kuasisiwa kituo cha utafiti wa elimu ya nujumu katika eneo la Maraghe kaskazini magharibi mwa Iran, Qutbuddin Shirazi aliishi kipindi kirefu na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Khaja Nasiruddin Tusi na kupata elimu ya nujumu. Katika kipindi chote cha umri wake, tabibu huyo wa Kiislamu alitembelea miji na nchi mbalimbali na kukutana na wasomi na maulamaa wa maeneo hayo. Ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Jaamiul Usul na Nihayatul Idrak. Alifariki dunia mwaka 710 Hijria.

Qutbuddin Mahmoud Shirazi

Siku kama ya leo miaka 225 iliyopita, yaani tarehe 16 Oktoba mwaka 1793, alinyongwa kwa kukatwa kichwa na shoka, malikia wa Ufaransa Marie Antoinette kupitia amri ya baraza la katiba la nchi hiyo na pia amri ya Maximilien Robespierre. Louis wa 16 alikuwa mume wa  Antoinette ambaye naye miezi 10 kabla ya hapo alikumbwa na hatma hiyo hiyo iliyomkuta mke wake. Marie Antoinette, alikuwa binti wa Maria Theresa Walburga, mtawala wa Austria na Ufaransa. Antoinette aliolewa na Louis, mrithi wa kiti cha ufalme wa Ufaransa, mnamo mwaka 1770 Miladia akiwa na umri wa miaka 14. Hatua ya Louis ya kumuoa mwanamke huyo ilikuwa ni kujaribu kuzikurubisha pamoja nchi za Austria na Ufaransa ambazo wakati huo zilikuwa zikishindana barani Ulaya. Hata hivyo Wafaransa wengi hawakuridhia ndoa hiyo kiasi cha kuwafanya kuendelea kumwita kwa lakabu ya ‘Muaustria’ hata kipindi alipokuwa tayari ni malikia wa Ufaransa. 

Marie Antoinette

Siku kama ya leo miaka 164 iliyopita alizaliwa Oscar Wilde mwandishi mashuhuri Dublin huko Ireland. Oscar Wilde alipata elimu ya msingi katika mji wa Skyline kaskazini mwa Ireland na akajiunga na chuo kikuu cha Trinity na baadaye Oxford. Oscar Wilde alipata umaarufu baada ya kuandika mfululizo wa vitabu vya kisa cha Mwanamfalme Mwenye Bahati. Mwandishi huyo pia ameandika vitabu vingi vya mashairi.

Oscar Wilde

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita liliasisiwa Shirika la Chakula Duniani (FAO). Hati ya kuasisiwa shirika hilo ilipasishwa Oktoba 16 mwaka 1945 katika mji wa Québec nchini Canada. Lengo ya kuasisiwa shirika la FAO ni kuzisaidia nchi wanachama kukusanya taarifa, ripoti na takwimu zinazohusiana na chakula, kilimo, utunzaji wa misitu na uvuvi na kufanya tathmini kuhusu uzalishaji wa chakula, ugavi wake na juhudi za kuboresha uzalishaji, masoko ya chakula, kulinda maliasili, kupanga sera zinazohusiana na kilimo na chakula na kadhalika. Siku hii pia inatambuliwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Chakula.

Shirika la Chakula Duniani (FAO)

Miaka 72 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 16 Oktoba 1946, kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Nuremberg walinyongwa viongozi 10 wa Ujerumani ya utawala wa Kinazi baada ya kupatikana na hatia za kutenda jinai za kivita. Herman Goering aliyekuwa Kamanda Mkuu wa kikosi cha Jeshi la Anga la Ujerumani na msaidizi wa dikteta Adolphe Hitler ambaye alikuwa amehukumiwa adhabu ya kifo, pia aliamua kujinyonga yakiwa yamebakia masaa machache kabla ya kutekelezwa hukumu hiyo ya kifo. Hali kadhalika mahakama hiyo iliwahukumu adhabu ya kifungo cha muda mrefu viongozi wengine 9 wa Ujerumani ya Wanazi na wengine watatu hawakupatikana na hatia. Mahakama ya Nuremberg iliyoundwa na wawakilishi wa Marekani, Urusi ya zamani, Uingereza na Ufaransa kwa shabaha ya kuwahukumu maafisa 22 wa Manazi wa Ujerumani kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita ilikamilisha shughuli zake tarehe 30 Septemba mwaka 1946.

Na siku kama ya leo tarehe 24 Mehr miaka 40 iliyopita, kulitokea maafa makubwa kwenye Msikiti Mkuu wa Kerman, huko magharibi mwa Iran baada ya polisi na askari usalama wa utawala wa mfalme Muhammad Reza Pahlavi kuwashambulia kwa risasi wananchi waliokusanyika kwenye eneo hilo la msikitini kwa shabaha ya kuadhimisha 40 ya mashahidi waliouawa tarehe 17 Shahrivar mjini Tehran. Shambulio hilo la askari usalama wa Shah liliamsha hasira na wimbi jipya la harakati za wananchi za kupinga utawala kibaraka wa Mfalme Muhammad Reza Pahlavi.

Wananchi wa Kerman wakipambana na askari wa utawala wa Shah.