Nov 30, 2018 23:07 UTC
  • Jumamosi, Mosi Disemba, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 23 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1440 Hijria inayosadifiana na tarehe Mosi Disemba 2018 Miladia.

Siku kama yya leo miaka 1239 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Bibi Fatma Maasuma dada wa Imam Ali bin Mussa al-Ridha AS aliwasili katika mji wa Qum, Iran. Mwakka mmoja baada ya safari ya kubaidishiwa kaka yake huko katika mji wa Marv, Bibi Maasuma alifunga safari kwa ajili ya kwenda kuonana na kaka yake huyo. Baada ya kuiwasili Qum, aliishi katika mji huo kwa siku 17 na katika wakati huo alijishughulisha na ibada, dua na kujikurubisha kwa Mola Muumba. Eneo alilokuwa akifanyia ibada bibi huyo mtukufu hadi leo linajulikana kama 'Baitul Nur, na hadi leo linatembelewa na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (SAW). Mwishowe tarehe 10 Rabiul Thani mwaka 201 Hijiria, ikiwa ni kabla hajakutana na kaka yake  Imam Ridha AS, Bibi Fatima Maasuma alifariki dunia huku akiwa katika upweke na majonzi makubwa. Hii leo haram ya BibI  Fatma Maasuma AS mjini Qum ni moja ya maeneo matakatifu ambapo watu kutoka katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu wa Kiislamu huenda kufanya ziara katika eneo hilo. ***

Katika siku kama ya leo miaka 193 iliyopita, muungano wa kihistoria wa nchi za Ulaya uliojulikana kama Muungano Mtakatifu ulisambaratika baada ya kujiengua utawala wa Kikaitsar (Tsarist) wa Russia katika muungano huo. Baada ya kuanguka kwa utawala wa Napoleon, muungano huo ukaunda Congress ya Vienna, kati ya tawala za Russia, Austria na ufalme wa Pros na serikali hizo zikaafikiana kwamba nchi zilizo chini ya utawala wa muungano huo na katika uhusiano wa kimataifa zifuate misingi ya dini ya Kikristo. ***

Nchi zilizokuwa zikiunda Muungano Takatifu 1840

Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo David Ben-Gurion mmoja wa waasisi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Waziri Mkuu wa kwanza wa utawala huo ghasibu aliaga dunia. Ben-Gurion alizaliwa tarehe 16 Oktoba 1886 katikka mji wa Plonsk huko Uholanzi ambayo katika zama hizo ilikuwa sehemu ya ardhi ya ufalme wa Russia. Alielekea katika ardhi za Palestina mwaka 1906 akiwa na umri wa miaka 20 na kuasisisi harakati ya Kiyahudi. ***

David Ben-Gurion

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Ayatullah Mirza Javad Agha Tehrani alimu na mwanazuoni mchaji-Mungu. Alizaliwa mjini Tehran katika familia iliyokuwa imeshikamana kikamilifu na dini. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali alielekea katika mji wa Qum Iran na baadaye Najaf Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Akiwa katika huko Ayatullah Tehrani alihudhuria darsa na masomo ya walimu mahiri wa zama hizo. Miongoni mwa sifa alizopambika nazo Ayatullah Mirza Javad Agha Tehrani ni uchaji Mungu, kuipa kwake mgongo dunia na mapenzi yake makubwa kwa Ahlul-Beit AS. Msomi huyo wa Kiislamu hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi wa vitabu. ***

Ayatullah Mirza Javad Agha Tehrani

Na katika siku kama ya leo ya tarehe Mosi Disemba nchi mbalimbali duniani huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ukimwi. Kuweko Siku ya kimataifa ya Ukimwi kulifikiriwa kwa mara ya kwanza mwezi Agosti mwaka 1987 na James W.Bunn na Thomas Netter, maafisa wawili wa habari wa Kitengo cha Kimataifa cha Kupambana na Ukimwi cha Shirika la Afya Duniani (WHO) huko Geneva Uswisi. Maafisa hao wawili waliwasilisha wazo hilo kwa Dakta Jonathan Mann, Mkurugenzi wa Shirika la UNAIDS na baadaye akakubali pendekezo hilo, na kuliidhinisha. Na hatimaye akaafiki siku ya kwanza ya kimataifa ya Ukimwi iadhimishwe duniani kote tarehe Mosi Disemba mwaka 1988. Kuanzia wakati huo kila mwaka siku ya kimataifa ya Ukimwi huadhimishwa duniani kote kila ifikapo tarehe Mosi Disemba.***

Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ukimwi