Jumanne tarehe 18 Disemba 2018
Leo ni Jumanne tarehe 10 Rabiuthani 1440 Hijria sawa na Disemba 18 mwaka 2018.
Miaka 1239 iliyopita inayosadifiana na tarehe 10 Rabiuthani mwaka 201 Hijria, alifariki dunia Bibi Fatima Maasuma A.S, binti wa Imam Mussa bin Jaafar al-Kadhim (as). Bibi Fatima Maasuma alizaliwa mwaka 173 Hijria katika mji wa Madina. Alikuwa mwanamke mwenye fasaha katika uzungumzaji, alimu, hodari na zahidi na mcha- Mungu. Mwaka mmoja baada ya kaka yake yaani Imam Ali bin Mussa Ridha (as) kuwasili Khurasan nchini Iran, Bibi Maasuma aliondoka Madina kwa lengo la kumfuata kaka yake, lakini akiwa njiani alisimama katika mji wa Qum na kufariki dunia mjini humo kutokana na maradhi au kwa mujibu wa kauli nyingine, kutokana na sumu aliyeopewa.

Tarehe 10 Rabiuthani mwaka 1330 Hijria yaani siku kama hii ya leo miaka 110 iliyopita Haramu tukufu ya Imam Ali bin Mussa Ridhaa, mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Mash'had huko kaskazini mwa Iran ilishambuliwa kwa mizinga na wavamizi wa Kirusi. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Mmarekani, Morgan Shuster kuanzisha kikosi maalumu cha polisi ya Hazina Kuu ya Iran. Urusi iliitambua hatua hiyo kuwa ni kinyume na maslahi yake haramu nchini. Mashambulizi hayo yalisababisha hasara kubwa kwa haramu ya mjukuu huyo wa Mtume (saw) na mali za thamani za eneo hilo tukufu ziliporwa na wavamizi hao.

Miaka 116 iliyopita katika siku kama ya leo, kituo cha kwanza cha redio duniani kiliasisiwa na Guglielmo Marconi, mvumbuzi na mbunifu wa Kiitalia. Kwa utaratibu huo, kukaweko mawasiliano ya haraka baina ya Ulaya na Amerika. Katika zama hizo redio ilikuwa ikitumiwa zaidi kama chombo cha mafunzo. Marconi alifikia hatua hiyo kutokana na bidii na shauku kubwa aliyokuwa nayo tangu awali ya kufanya utafiti katika uwanja huo.
Miaka 104 iliyopita katika siku kama ya leo, Uingereza iliikoloni rasmi Misri. Inafaa kukumbusha kwamba, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa Othmania ulikuwa mwitifaki wa madola yaliyokuwa yakiipinga Uingereza yaani Ujerumani na Austria. Uingereza nayo ikiwa na lengo la kukabiliana na kitendo hicho, iliikalia kwa mabavu Misri, ambayo hadi katika kipindi hicho ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Othmania. Harakati za ukombozi za wananchi wa Misri dhidi ya mkoloni Mwingereza zilizaa matunda mwaka 1922, ambapo nchi hiyo ilijitangazia uhuru wake.
Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita msomi wa Ujerumani, Otto Hahn, alifanikiwa kupasua kiini cha atomu, hatua ambayo ilikuwa mwanzo wa zama za atomu. Mtaalamu huyo wa kemia alizaliwa mwaka 1879 huko Frankfurt na kupata shahada ya uzamivu katika taaluma ya kemia. Tangu wakati huo alijishughulisha na utafiti katika taaluma fizikia. Baada ya utafiti mkubwa na katika siku kama hii ya leo Otto Hahn alifanikiwa kupasua kiini cha atomu. Hatua hiyo iliibua nishati kubwa ambayo baadaye ilianza kutumika katika vinu na mabomu ya nyuklia. Mwaka 1944 Otto Hahn alitunikiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya kemia.
Tarehe 18 Disemba miaka 39 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha makubaliano ya kufuta aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake. Makubaliano hayo yana lengo la kuondoa dhulma zinazofanywa dhidi ya wanawake duniani. Hata hivyo makubaliano hayo, kama yalivyo mengine mengi ya kimataifa, yanatawaliwa na mitazamo ya kimaada ya Magharibi inayosisitiza usawa wa jinsia mbili za mwanamke na mwanaume katika kila kitu. Hii ni katika hali ambayo mwanamke na mwanaume wanatofautiana kimwili na kiroho. Kwa sababu hiyo dini za Mwenyezi Mungu hususan Uislamu zinasisitiza kuwa njia ya kuwakomboa wanawake ni kuwatayarishia mazingira ya uadilifu kwa kutilia maanani uwezo na sifa zao za kimwili na kiroho.

Na siku kama ya leo miaka 39 iliyopita na katika siku kama ya leo, Dakta Muhammad Mufatteh alimu, mwanaharakati na mwanamapambano wa Kiirani aliuawa shahidi na makundi ya kigaidi. Baada ya kumaliza masomo yake ya kimsingi alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum. Sambamba na kusoma masomo ya dini, Muhammad Mufatteh alikuwa akisoma pia katika Chuo Kikuu cha Tehran na kufanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika falsafa yaani PHD. Baada ya kupata shahada hiyo akaanza kufundisha kama mhadhiri huku akiendesha harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Shah uliokuwa ukitawala hapa nchini Iran.