Jan 06, 2019 02:44 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 820, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass 'Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 161 hadi 163 ambazo zinasema:

فَإِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ

Basi hakika nyinyi na mnao waabudu

مَا أَنتُمْ عَلَيْهِ بِفَاتِنِينَ

Hamwezi kuwapoteza.

إِلَّا مَنْ هُوَ صَالِ الْجَحِيمِ

Isipo kuwa yule atakaye ingia Motoni.

Katika darsa iliyopita tulizungumzia imani na itikadi potofu za washirikina kuhusu malaika na majini. Aya hizi tulizosoma zinasema: Nyinyi waabudu masanamu hamwezi kuwapotosha na kuwapoteza watu wengine kwa fikra zenu hizo potofu. Kwa sababu, watu wenye akili na mantiki na nyoyo safi hawayakubali maneno yenu wala hawatokuwa tayari kufuata hayo muyasemayo, yasiyo na mantiki yoyote. Tab'an kwa wale wanaokhitari njia ya watu wa Motoni, wao wanaweza kwa hiari yao kufuata itikadi ya washirikina na kushika njia na mwenendo wao wa upotofu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu akiwa kiumbe huru. Kwa hivyo katika kuchagua njia na mfumo wake wa maisha, mtu amepewa uwezo na hiari ya kuchagua; na wala hakuna yeyote awezaye kumlazimisha mwenzake kuchagua njia ya kufuata. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuchagua njia ya kufuata kuko kwenye mamlaka ya mtu mwenyewe, lakini hatima na malipo ya chaguo alilofanya, yako nje ya mamlaka yake. Kwa hivyo haiwezekani mtu achague kufuata njia ya ukafiri, dhulma na shirki kisha atarajie kuingia kwenye Pepo ya milele.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 164 hadi 166 ambazo zinasema:

وَمَا مِنَّا إِلَّا لَهُ مَقَامٌ مَّعْلُومٌ

Na hapana katika sisi ila anapo mahali pake maalumu.

وَإِنَّا لَنَحْنُ الصَّافُّونَ

Na hakika bila ya shaka sisi ndio wajipangao safu.

 وَإِنَّا لَنَحْنُ الْمُسَبِّحُونَ

Na hakika sisi ndio wenye kusabihi.

Washirikina walikuwa na imani potofu kuhusu Malaika. Walikuwa wakiwachukulia watoto wa kike kuwa ni viumbe dhaifu na duni, na kuwaitakidi Malaika kwamba ni mabinti wa Mwenyezi Mungu; na kwa njia hiyo, wakawanasibisha na Yeye Mola aliyetukuka na kutakasika. Aya tulizosoma zinanukuu maneno ya Malaika wenyewe wakisema:

Kinyume na mnavyodhania nyinyi waabudu masanamu, sisi Malaika hatuna jinsia ya kike wala ya kiume. Ni viumbe wenye nguvu, ambao Allah SW ametupangia kila kundi kati yetu, kazi na majukumu maalumu; na sisi, muda wote tunatii na kutekeleza amri yake. Sisi tunamtakasa Allah na kila aina ya fikra na imani potofu mlizonazo nyinyi washirikina, na daima ni wenye kumsabihi na kumhimidi Yeye Mola. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Mwenyezi Mungu anayaendesha mambo yote ya ulimwengu kwa kutumia sababu na visababishi vya kimaada na kimaanawi; na Malaika wana nafasi muhimu katika uendeshaji masuala ya ulimwengu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Malaika si watoto wa Mwenyezi Mungu. Wao wameumbwa na Yeye Mola wakiwa na majukumu ya kutekeleza amri zake; na katika kufanya hivyo hujipanga kwenye safu zenye nidhamu na umakini maalumu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, katika ulimwengu wa Malaika, kuna utaratibu maalumu wa vyeo na daraja; na kila mmoja wao ana hadhi, nafasi na jukumu lake maalumu.

Zifuatazo sasa ni aya za 167 hadi 170 ambazo zinasema:

وَإِن كَانُوا لَيَقُولُونَ

Na hakika wao walikuwa wakisema:

لَوْ أَنَّ عِندَنَا ذِكْرًا مِّنَ الْأَوَّلِينَ

Tungeli kuwa na Ukumbusho kama wa watu wa zamani,

 لَكُنَّا عِبَادَ اللَّـهِ الْمُخْلَصِينَ

Bila ya shaka tungeli kuwa ni waja wa Mwenyezi Mungu waliotakaswa. 

فَكَفَرُوا بِهِ ۖ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ

Lakini waliukataa. Basi watakuja jua.

Kwa mujibu wa historia ni kwamba, kabla ya kubaathiwa na kupewa Utume Nabii Muhammad SAW na kuteremshwa Qur’ani tukufu, washirikina wa Makka walikuwa wakiwaambia Mayahudi na Manasara waliokuwa wakiishi Bara Arabu: Kama Mwenyezi Mungu atatuletea Mtume na kututeremshia Kitabu, sisi tutamwamini na kumfuata. Aya tulizosoma zinasema: Hakika Mwenyezi Mungu amelifanya hilo kwa kuwateremshia Qur’ani ya kuwaongoza kuufikia uongofu, lakini walikataa kuifuata haki kwa visingizio mbalimbali na badala yake wakakhitari kushika njia ya ukafiri na ukanushaji. Kwa hivyo watayaona matokeo ya waliyoyafanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Allah SW ameondoa dhima kwa waja wake kwa kuwapelekea Mitume na kuwateremshia Vitabu vya mbinguni, ili asije mtu yeyote kupata kisingizio cha kumbebesha dhima Yeye kwa sababu ya mtu huyo kufuata ukafiri na ushirikina na kuipa mgongo njia ya haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wanaojigamba kwa maneno ni wengi mno, lakini watendaji wa kweli ni wachache sana. Kuna watu wengi wanaodai kwa ndimi zao kuwa wanaifuata dini, lakini katika matendo yao wanaikana haki na kuipinga dini ya Allah.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 171 hadi 173 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ سَبَقَتْ كَلِمَتُنَا لِعِبَادِنَا الْمُرْسَلِينَ

Na bila ya shaka neno letu lilikwisha tangulia kwa waja wetu walio tumwa.

إِنَّهُمْ لَهُمُ الْمَنصُورُونَ

Ya kuwa wao bila ya shaka ndio watakao nusuriwa. 

وَإِنَّ جُندَنَا لَهُمُ الْغَالِبُونَ

Na kwamba jeshi letu ndilo litakalo shinda. 

Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kuhusu ukafiri na ukanushaji wa washirikina na kueleza kwamba: Waumini wasiingiwe na shaka yoyote katika imani zao au kuwa na ajizi na kuwa dhaifu katika ufanyaji amali zao. Kwa sababu Mwenyezi Mungu SW ameshatoa ahadi kwamba, ikiwa waumini watakuwa imara na wenye istiqama katika kuwafuata Mitume, wakaendelea kuwa thabiti na kudumu katika msimamo wao huo, mwisho wake haki itashinda na batili itatoweka. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kaida na utaratibu uliowekwa na Allah ni wa haki kuishinda batili na imani kuishinda kufru. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ushindi wa Mitume na dini zao dhidi ya itikadi na mifumo mingine ya maisha ni jambo la hakika. Kwa maneno mengine ni kwamba, mustakabali wa wanadamu utashuhudia ushindi wa Mitume na kushindwa kusio na shaka kwa maadui zao. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kwamba, hata kama waumini watakuwa wachache, watapata auni na msaada wa Allah; lakini makafiri hawawezi kupata neema hiyo ya msaada wa Mola. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 820 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah aupe izza na nguvu Uislamu na Waislamu, na aufanye dhalili na dhaifu ukafiri na wafuasi wake. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags