Jumatatu, 18 Machi, 2019
leo ni Jumatatu tarehe 11 Rajab mwaka 1440 Hijria sawa na Machi 18 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, hatimaye mapambano ya wananchi Waislamu wa Algeria yaliyoanzishwa kwa lengo la kuikomboa nchi hiyo na kukomesha uvamizi wa kikoloni wa Ufaransa yalipata ushindi baada ya miaka minane ya vita vikali. Watu milioni moja waliuawa katika vita hivyo. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa pili wa Evian, Ufaransa ilitambua uhuru wa Algeria na kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo. Hata hivyo jeshi la siri la Ufaransa liliendeleza operesheni za kigaidi kwa muda nchini Algeria. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Algeria wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Yusuf bin Khada na baadaye nchi hiyo ikawa chini ya utawala wa Ahmad bin Bella.
Miaka 161 iliyopita siku kama leo, alizaliwa mvumbuzi mashuhuri wa Kijerumani, Rudolf Diesel, ambaye alibuni injini ya diseli. Diesel alifanya utafiti na uhakiki mkubwa kuhusu injini za mitambo mbalimbali na akafanikiwa kuvumbua chombo ambacho kinaweza kuzalisha nishati kubwa zaidi bila ya kuhitaji umeme lakini kwa kutumia nishati ya kawaida na rahisi zaidi. Chombo hicho ambacho kilipewa jina lake mwenyewe la Diesel kilileta mabadiliko makubwa katika sekta ya viwanda na usafirishaji kwa kadiri kwamba licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia lakini injini za diseli zingalia zinatumika kwa kuwa ni zenye nguvu kubwa na zinazotumia nishati ndogo. Rudolf Diesel alifariki dunia mwaka 1913.
Miaka 869 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia mjini Damascus, Syria mwanahistoria mkubwa na mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu Ibn Asakir. Alisoma elimu za Qur'ani, hadithi, fiq'hi na usulu fiq'hi kwa wasomi wakubwa wa mjini Damascus. Baada ya hapo Ibn Asakir alianza safari ndefu yenye lengo la kukamilisha masomo yake na kupata kusoma katika vituo vya kielimu vya mijini Baghdad, Kufa, Mosul, Neishabur, Marv, Isfahan na Hamedan. Msomi huyo ameandika vitabu 134 kikiwemo kile cha "Tarikh Dimeshqi."
Na miaka 1169 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 11 Rajab mwaka 271 Hijiria, alizaliwa Abubakr Muhammad maarufu kama Ibin Anbari mwanafasihi, mtaalamu wa lugha na mfasiri wa Qur'ani Tukufu katika mji wa Baghdad. Alijifunza lugha na elimu ya Qur'ani na baadaye hadithi. Ibn Anbari alikuwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi mambo na pia alifanya kazi ya kufundisha kwa unyenyekevu. Miongoni mwa vitabu vyake ni Adabul Katib na Dhamairil Qur'ani. Ibn Anbari alifariki dunia mwaka 328 Hijiria.