Jumamosi, 23 Machi, 2019
Leo ni Jumamosi tarehe 16 Rajab 1440 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 23 Machi 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 367 iliyopita sawa tarehe 23 Machi mwaka 1652, yalianza mashambulizi ya manowari za kijeshi za Uingereza dhidi ya majeshi ya Uholanzi. Amri ya shambulizi hilo ilitolewa na Oliver Cromwell aliyekuwa dikteta wa wakati huo wa Uingereza. Akipata uungaji mkono wa Bunge la Uingereza, Cromwell alimpindua mfalme wa Uingereza na kisha kulivunja bunge la nchi hiyo. Inasemekana kuwa, lengo la kutekeleza shambulio hilo lilikuwa ni kulimaliza nguvu jeshi la Uholanzi ambalo lilikuwa na nguvu kubwa ya majini. ***
Katika siku kama ya leo miaka 270 iliyopita, alizaliwa Pierre-Simon Laplace mwanahisabati mashuhuri wa Kifaransa. Baada ya kuhitimu masomo alijishughulisha na kufundisha hisabati. Laplace alitumia sehemu kubwa ya umri wake kutwalii na kufanya uhakiki kuhusiana na elimu za nujumu na hisabati. ***
Miaka 100 iliyopita katika siku kama ya leo, ilianzishwa harakati ya Ufashisti nchini Italia kwa uongozi wa Benito Mussolini. Ufashisti kwa ujumla ni utawala wa kidikteta wenye kufuata aidolojia ya kibaguzi na kiutaifa, kuwakandamiza wapinzani, kuondoa uhuru na kuzipotosha itikadi na fikra za wananchi. Hayo yalijiri baada ya Mussolini kunyakua wadhifa wa uwaziri mkuu nchini Italia, mwaka 1922 na kuanza duru ya udikteta nchini humo. Muda mfupi baadaye Mussolini alishirikiana na Adolph Hitler, na kuandaa mazingira ya kuanzishwa Vita vya Pili vya Dunia. ***
Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita yaani tarehe 3 Farvardin 1301 Hijria Shamsia, Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mjini Qum Iran kilianzishwa na Ayatullah Sayyid Abdul Karim Hairi Yazdi. Mji wa Qum ulikuwa kitovu cha kueneza elimu, maarifa ya dini na kulea maulama mashuhuri tangu mwanzoni mwa karne za awali za kudhihiri dini Tukufu ya Kiislamu. Kuweko Haram ya Bibi Fatma Maasuma AS dada wa Imam Ridha AS katika mji wa Qum, kumezidi kuufanya mji huo uwe na umuhimu mkubwa. Baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Hawza ya Qum iligeuka na kuwa kituo muhimu cha mafunzo na uenezaji wa elimu za Kiislamu na utamaduni wa Kishia. ***
Katika siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, liliasisiwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani 'WMO'. Shirika hilo linafungamana na Umoja wa Mataifa na taasisi zote za hali ya hewa ulimwenguni hushirikiana na shirika hilo. Miongoni mwa malengo ya kuanzishwa shirika hilo ni kutoa msaada wa elimu ya hali ya hewa kwa wataalamu wa anga, mabaharia, wakulima na shughuli nyingine za kibinadamu. Ni kwa ajili hiyo ndio maana siku ya leo yaani tarehe 23 Machi ikajulikana kuwa Siku ya Hali ya Hewa Duniani. **
Miaka 63 iliyopita katika siku kama hii ya leo katiba mpya ya Pakistan ilibuniwa na kwa mujibu wake utawala wa nchi hiyo ulibadlishwa kutoka utawala wa Gavana Mkuu na kuwa na mfumo wa Jamhuri. Liaquat Ali Khan Waziri Mkuu wa wakati huo wa Pakistan alichukua madaraka ya kuiongoza nchi hiyo mwaka 1948 kufuatia kifo cha Muhammad Ali Jinnah aliyekuwa mwasisi na Gavana Mkuu wa nchi hiyo. Liaquat Ali Khan naye pia aliuawa na raia mmoja wa Afghanistan mwaka 1951. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, sawa na tarehe 3 Farvardin 1384 Hijria Shamsia, alifariki dunia Allamah Sayyid Jalaluddin Ashtiyani, mwanafalsafa na mwanafikra wa Kiislamu baada ya kuugua kwa muda mrefu. Allamah Ashtiyani alizaliwa Ashtiyan katikati mwa Iran na kupata elimu ya msingi katika eneo hilo. Baadaye alielekea katika mji wa Qum na kupata elimu kwa wanachuoni wakubwa kama vile Imam Ruhullah Khomeini, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai. Baadaye alielekea katika mji mtakatifu wa Mash'had na kujishughulisha na kulea wanafunzi hadi mwisho wa uhai wake. ***