Apr 15, 2016 12:38 UTC
  • Maswali Yetu Majibu ya Thaqalain 119

Assalaam Aleikum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 119 katika mfululizo wa vipindi hivi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambavyo kama mnavyojua huwa vinajadili na kuchambua maswali mbalimbali yanayohusiana na imani na itikadi ya Kiislamu.

Katika kipindi cha juma hili tutaendelea kujibu swali tulilouliza katika kipindi kilichopita ambalo lilisema je, ni masharti na sifa zipi anazopasa kuwa nazo Imam wa haki ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu ametwambia katika maandiko matakatifu kuwa hataiacha ardhi bila ya kuwa na Hujja na Imam kama huyo ambaye ndiye chanzo cha kuongoka na kufikia saada ya milele waja wake huko Akhera. Tulipata kujua sifa tatu kati ya sifa hizo kupitia aya tulizosoma katika kipindi kilichopita nazo ni kwamba Imam huyo anapasa kuwa ni mtu maasumu aliye na kinga ya Mwenyezi Mungu ya kutofanya dhambi na ambaye hajawahi kumshirikisha Mwenyezi Mungu wala kufanya dhambi hata kidogo na kuongozwa na Mwenyezi Mungu bila ya kuhitajia kuongozwa na mwanadamu au kiumbe mwingine yoyote. Sifa ya tatu ni kuwa anapasa kuwa miongoni mwa waja wema walio na yakini na wa daraja ya juu ambao Mwenyezi Mungu amewafungulia siri za mbingu zake nao kuwa watu wanaobeba Arshi yake. Baada ya kuzijua sifa hizo sifa ya nne ni ipi? Karibu tulijadili kwa pamoja sifa hiyo na sifa nyinginezo kadhaa. 

Ndugu wasikilizaji, sifa ya nne tunayopata kuijua kutokana na aya za Qur’ani Tukufu ni kwamba, subira ni miongoni mwa masharti na sifa muhimu ambazo mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwaongoza watu kwenye njia nyoofu na ya saada ya milele anapasa kuwa nazo. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 24 ya Surat as- Sajda: Na tukawafanya miongoni mwao maimamu wanaoongoza kwa amri yetu, waliposubiri na wakawa na yakini na Ishara zetu.

Na maana ya subira hapa iko wazi kabisa ambapo kusudio lake ni yale mambo yanayohusiana na majukumu ya Uimamu unaotoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu kuelekea Kwake. Ni kama ambavyo Manabii wa Mwenyezi Mungu (as) walivyosubiri na kustahamili machungu mengi kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa Mola wao kuonya pamoja na kuwabashiria wanadamu mambo waliyopasa kuyafahamu kuhusiana na mafundisho na amri za Mwenyezi Mungu. Imam Swadiq (as) anasema katika sehemu ya hadithi moja ndefu iliyonukuliwa kutoka kwake katika kitabu cha al-Kafi kama ifuatavyo: “Unapasa kuwa na subira katika mambo yako yote. Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu alimtuma Muhammad (saw) na kumuamuru kuwa na subira na mpole…..Hivyo Mtume akasubiri katika kila hali na kubashiriwa Maimamu katika kizazi chake ambao walisifika kwa kuwa na subira na Mwenyezi Mungu akasema: Na tukawafanya miongoni mwao maimamu wanaoongoza kwa amri yetu, waliposubiri na wakawa na yakini na Ishara zetu. Hapo Mtume (saw) akasema: Subira katika imani ni kama vile kichwa kilivyo kwenye mwili.”

Wapenzi wasikilizaji, ni wazi kuwa kuinasibisha aya tukufu tuliyoiashiria kwa Maimamu watoharifu wa Ahlul Beit wa Mtume (saw) ni kutokana na kuwa wao ndio mfano ulio bora zaidi na wa moja kwa moja wa aya hiyo. Hilo halizuii kunasibishwa aya hiyo kwa maimamu wa kaumu ya Nabii Musa (as) ambaye alinusuru na kuwaokoa Bani Israel kutokana na dhuluma waliyokuwa wakifanyiwa na Mafirauni wa Misri.

********

Ndugu wapendwa, hadithi tukufu zinaashiria suala muhimu mno hapa nalo ni kwamba Mwenyezi Mungu kuwateuwa waja wema hawa kuwa Maimamu kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu kunatokana na ufahamu na ujuzi wake mkubwa kwamba watukufu hawa wana uwezo wa kusubiri na kuvumilia matatizo katika majukumu yao ya kuwaongoza wanadamu.

Allama Sayyid Sharaf ad-Deen al Husseini amenukuu katika kitabu chake cha Ta’weel al-Ayaat al-Bahira fi Manaqib al-Itra at-Twahira kadithi kutoka kwa Imam Baqir (as) akisema: “Aya hii iliteremka mahususi kwa kizazi cha Fatima (sa). (Na tukawafanya miongoni mwao maimamu wanaoongoza kwa amri yetu, waliposubiri na wakawa na yakini na Ishara zetu, yaani waliposubiria balaa duniani na Mwenyezi Mungu alipoona subira miongoni mwao aliwafanya kuwa Maimamu wanaoongoza waja Wake kumtii Yeye kwa amri Yake, utiifu ambao unaelekeza kwenye Pepo, hivyo swala na salamu timilifu za Mola wao ziwe juu yao.”

Maana hii imebainishwa kwa uwazi zaidi katika ziara ya Bibi Fatima (sa) iliyopokelewa kutoka kwa Imam Baqir (as) ambapo anasema katika sehemu ya ziara hiyo: Salamu ziwe juu yako ewe uliyetahiniwa! Alikutahini aliyekuumba kabla ya kukuumba na ukawa umesubiria yale aliyokutahini kwayo. Sisi kwako ni mawalii wanaosadikisha, na kusalimu amri mbele ya yale yote aliyokuja nayo Baba yako (saw) na aliyokuja nayo Wasii wake (as).

********

Wapenzi wasikilizaji, kuna sifa nyingine muhimu ambayo tunaitambua kutokana na aya tuliyotangulia kusoma ambayo Imam wa haki anapasa kuwa nayo, nayo ni kwamba Imam huyo anapasa kuongoza kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Katika Tafsiri yake, Ali Bin Ibrahim (MA) amenukuu hadithi kutoka kwa Imam Baqir (as) akisema: “Maimamu katika kitabu cha Mwenyezi Mungu ni wa aina mbili: Imam wa uadilifu na imam wa dhulma. Mmweyezi Mungu amesema: Na tukawafanya miongoni mwao maimamu wanaoongoza kwa amri yetu (yaani) si kwa amri ya watu, wanafadhilisha amri ya Mwenyezi Mungu juu ya amri yao na hukumu ya Mwenyezi Mungu juu ya hukumu yao.”

Na imepokelewa katika kitabu cha al-Manaqib kwamba Mtume Mtukufu (saw) aliwaita Ali na Fatima (as) na kusema: “Allahumma! Imarisha umoja miongoni mwao na uunganishe nyoyo zao. Wajaalie wawili hawa pamoja na kizazi chao miongoni mwa warithi wa Pepo iliyojaa neema na waruzuku kizazi chema, kitoharifu na kilichobarikiwa. Jaalia kwenye kizazi chao baraka na ukijaalie kiwe cha Maimamu wanaoongoza kwa amri yako kuelekea utiifu wako na kuamrisha yale yanayokuridhisha.”

Maimamu pia wamesifiwa kwa sifa hii katika aya ya 73 ya Surat an-Anbiyaa ambapo Mwenyezi Mungu anasema: Na tukawafanya maimamu wakiongoza kwa amri Yetu. Na tukawapa wahyi watende kheri, na wasimamishe Swala, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu.

Ndugu wasikilizaji, tuliashiria katika kipindi kilichopita baada ya kubainisha maana ya uimamu kwamba, uongozaji unaotokana na amri ya Mwenyezi Mungu ni kuwasaidia waumini kufikia ukamilifu na kuthibiti kwa malengo ya ibada yao kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Makusudio ya amri ya mwenyezi Mungu katika istilahi ya Qur’ani Tukufu ni amri ya mbinguni na irada yake Mwenyezi Mungu mkabala na sheria ambazo zinahusu majukumu ya Manabii (as) katika kuonya, kubuni na kubainisha sharia.

Na maana nyingine inatokana na maana hii kuu, ambapo maana ya uongozaji kwa amri ya Mwenyezi Mungu ni ile iliyobainishwa katika hadithi ya Imam Baqir (as) ambapo Imam alisema Imam wa haki hutanguliza amri na hukumu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya amri na hukumu ya kila asiyekuwa Yeye.

********

Kwa kuzingatia yale tuliyosema wapenzi wasikilizaji, tunafupisha mambo tuliyojifunza katika kipindi hiki kwa kusema kwamba tumepata kujua sifa nyingine mbili ambazo anapasa kuwa nazo Imam wa haki, ambaye kumtambua na kumfuata humuepusha mja kufa kifo cha ujahili. Sifa hizo ni subira katika utekelezaji wa majukumu ya uimamu. Sifa ya pili ni kuongoza kwa amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na irada Yake, kwa maana ya msaada wake wa dhati na wa mbinguni kwa waumini katika njia yao ya kuelekea Kwake.

Kuna sifa nyingine ambazo anapasa kuwa nazo Imam wa haki ambazo zimezungumziwa kwa urefu katika maandiko matakatifu, sifa ambazo tutazizungumzia katika kipindi kijacho Inshallah. Basi hadi wakati huo tunakushukuruni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tunakukaribisheni mjiunge nasi tena kusikiliza kipindi kingine cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain juma lijalo, kwaherini.