Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain 120
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza sehemu ya 120 katika mfululizo huu wa vipindi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambavyo hukujieni kupitia Idhaa ya Kiswahiuli Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika vipindi kadhaa vilivyopita tumekuwa tukijadili suala la msharti na sifa anazopasa kuwa nazo Imam mwongozaji ambaye maarifa na kumjua kwake huongoa na kumnusuru mwanadamu kutokana na kifo cha ujahili.
Mwenyezi Mungu ameahidi kwamba hawezi kuiacha ardhi bila ya kuwa na Imam kama huyu ambaye ni hoja kwa viumbe na waja wake na ambaye ni sababu ya kuongoka na kuepuka kwao moto mkali wa Jahannam.
Na hili ni jambo ambalo limezungumziwa kwa mapana na marefu na maandiko matakatifu tunayoyasoma kwenye Qur’ani na hadithi tukufu za viongozi watoharifu wa dini. Hadithi hizi zimenukuliwa kwa wingi katika vitabu vya madhehebu yote mawili ya Kiislamu yaani Sunni na Shia. Katika vipindi vilivyopita tulipata kufahamu sifa tano kati ya sifa anazopasa kuwa nazo Imam mwema anayepasa na kustahiki kuuongoza umma wa Kiislamu. Sifa hizo tano ni kwamba Imam mstahiki anapasa kuwa maasumu ambaye katu hajawahi kumshirikisha Mwenyezi Mungu wala kufanya dhambi na kuongozwa na Mwenyezi Mungu tu bila ya kuongozwa na wanadamu wenzake. Sifa ya tatu ni kuwa anapasa kuwa miongoni mwa watu walio na yakini ambao Mwenyezi Mungu amewaonyesha siri za mbingu zake na hivyo kuwa miongoni mwa wabeba Arshi Yake. Sifa ya nne ni kuwa anapasa kuwa na kiwango cha juu zaidi cha subira katika utekelezaji wa majukumu yake ya mbinguni na wakati huohuo kustahamili machungu anayoyapitia kwenye njia hiyo. Na sifa ya tano ni kuwa anapasa kuongoza kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kuwasaidia waja wake kwa irada yake Muumba ili waweze kufanikisha majukumu yao ya kiibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Sifa nyingine za Imam ni zipi?
**********
Wapendwa wasikilizaji, jambo tunalojifunza kutokana a maandiko matakatifu ni kwamba moja ya sifa muhimu anazopasa kuwa nazo Imam wa haki aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwaongoza waja wake kwenye njia nyoofu ni kwamba anapasa kuwa wa kwanza katika kutekeleza maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu ili awe mfano bora kwa wale anaowaongoza na hivyo kuwashawishi watekeleze yale anayowafundisha. Sharti hili muhimu linaashiriwa na Mwenyezi Mungu katika aya ya 73 ya Surat al-Anbiyaa inayosema: Na tukawafanya maimamu wakiongoza kwa amri yetu. Na tukawapa wahyi watende kheri, na wasimamishe Swala, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu.
Tunaelewa kutokana na aya hii kwamba mtu anayeteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Imam huwa meidhinishwa na Mungu Muumba au kupitia njia inayojulikana kwenye dua kwa jina la taufiki ya utiifu. Hali hii humuwezesha kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa mambo mema na wala huwa hawaiti watu kufanya jambo jema ila kwanza yeye huwa amelitekeleza kama ilivyopokelewa kwenye hadithi mashuhuri kutoka kwa Imam Ali (as). Na sifa hii ni ya dharura kutokana na ukweli kwamba Imam huwa ndiye kamba inayounganisha ardhi na mbingu. Ni mfano ambao huigwa na mja anayetafuta saada na ukamilifu kwa ajili ya Akhera yake. Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa hoja ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake haitakuwa imekamilika iwapo Imam hatakuwa wa kwanza na kuwatangulia waja hao katika kutekeleza mambo mema na utiifu kwa Mwenyezi Mungu katika zama zake.
********
Maana hii ya sifa za Maimamu wapenzi wasikilizaji imebainishwa na kuzungumziwa na hadithi nyingi ambapo moja ni ile iliyopokelewa kutoka kwa Imam Ridha (as) katika kitabu cha Uyun al-Akhar ar-Ridha ambaye anasema: ‘Mwenyezi Mungu Mtukufu alituongoza kwa roho takatifu na safi kutoka kwake, roho ambayo hakupewa mfalme yoyote. Roho hiyo haikupewa mtu yoyote miongoni mwa watu waliopita isipokuwa Mtume Mtukufu (saw), nayo iko pamoja na Maimamu miongoni mwetu, inawaimarisha na kuwafanikisha.’
Na roho hii ya Mwenyezi Mungu inayoongoza na kumsaidia Imam wa Maimamu na Bwana wa Mitume Mtume Mtukufu (saw) pamoja na Maimamu wa kizazi chake (as) ndio njia bora zaidi ya kupata idhini ya Mwenyezi Mungu katika uongozaji wa waja. Idhini hii hutolewa kwa Maimamu na Manabii tofauti (as) kwa mujibu wa viwango na vyeo vyao.
*********
Na tunasoma kwa pamoja wapenzi wasikilizaji aya ya 32 ya Surat al-Fatir inayosema: Kisha tumewarithisha Kitabu hao ambao tumewateuwa miongoni mwa waja wetu. Kati yao yupo aliyejidhulumu nafsi yake, na yupo wa katikati, na yupo aliyetangulia katika mambo ya kheri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kuu.
Aya hii tukufu inabainisha wazi kwamba kutangulia katika mambo ya kheri ni bora zaidi kuliko mambo mengine ya ibada ambayo Mwenyezi Mungu amewafaradhishia aliowarithisha Kitabu. Na kutangulia huku hutimia kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, yaani kwa ruhusa yake kama tunavyoelewa hilo pia kutokana na aya tuliyotangulia kusoma katika Surat al-Anbiyaa.
Kuhusiana na aya hii Allama Tabatabai anasema katika Tafsiri yake ya al-Mizaan kwamba mgongano uliopo kati ya aliyejidhulumu nafsi, wa katikati na aliyetangulia katika mambo ya kheri katika aya hii unaweka wazi maana hii kwamba kusudio la aliyejidhulumu nafsi yake ni yule mja aliyefanya kiwango fulani cha dhambi miongoni mwa Waislamu. Kusudio la wa katikati ni yule aliye katika njia kuelekea ukweli na kusudio la aliyetangulia katika mambo ya kheri kwa idhini ya Mwenyezi Mungu ni yule aliyewatangulia dhalimu na wa katikati katika daraja ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, naye ni Imam wa wenzake kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na kutokana na kufanya kwake mambo mema na ya kheri. Mwenyezi Mungu anasema katika Surat al-Waqiah: Na waliotangulia ndio waliotangulia. Hao ndio watakaokaribishwa.
Vyanzo vyetu vya hadithi za kuaminika vimenukuu hadithi kadhaa zinazosema bayana kwamba makusudio ya aya hii ni kutangulia kwa Maimamu katika mambo ya kheri. Moja ya hadithi hizo ni ile iliyopokelewa katika kitabu cha al-Kafi ambapo Imam Ridha (as) amenukuliwa akisema: ‘Aliyetangulia katika mambo ya kheri ni Imam, wa katikati ni anayemjua Imam wake na aliyejidhulumu nafsi yake ni yule asiyemjua Imam wake.’
***********
Kwa hivyo wapenzi wasikilizaji, sifa ya sita anayopasa kuwa nayo Imam wa haki ambaye kumjua na kumfuata huongoa na kumuepusha mwanadamu kufa kifo cha ujahili ni kuwa anapasa kuwa katika mstari wa mbele na kumtangulia kila mtu katika utendaji wa mambo mema na ya kheri kwa idhini, uwezo na msaada wa Mwenyezi Mungu. Sifa hiyo humuwezesha kuwa kiongozi bora na anayefaa kufuatwa na watu kwa ajili ya kuwafikisha kwenye njia ya saada na iliyojaa neema na baraka tofauti za kimaanawi kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji tunahitimisha kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain kilichokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi juma lijalo tutakapokutana katika kipindi kingine panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warhmatullahi wa Barakatuh.