Maswali yetu na Majibu ya Thaqalain 121
Assalam Aleikum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 121 katika mfululizo wa vipindi hivi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalaini, ambapo kama mnavyojua kupitia vipindi kadhaa tumekuwa tukijadili sifa anazopaza kuwa nazo Imam wa haki anayewaongoza waja wa Mwenyezi Mungu kuelekea saada na mafanikio ya milele.
Kipindi cha juma hili kitajibu swali jingine linalohusiana na suala la Uimamu nalo linahusu haja ya kuwepo Imam maasumu anayeteuliwa na Mwenyezi Mungu moja kwa moja katika kila zama. Tulifahamu katika vipindi vilivyopita kwamba aya za kitabu kitakatifu cha Qur’ani zinasisitiza wazi kwamba kila kaumu ina mwongozaji na kwamba hakuna wakati ambapo dunia imewahi kubaki bila ya kuwa na hujja katika Maimamu maasumina (as). Kuna udharura gani wa hali kuwa hivyo? Karibuni wasikilizaji wapenzi tupate kujua jibu la swali hili muhimu katika maisha ya Waislamu.
*********
Ndugu wapendwa, katika kujibu swali hili kwanza tunachunguza hadithi muhimu ambayo imenukuliwa na Sheikh as-Swaduq katika kitabu cha Ilal as-Sharai’ kuhusiana na suala hili. Hadithi hiyo imepokelewa na mja mwema Jabir al-Ju’fi ambapo inasemekana kuwa alimuuliza Imam Baqir (as) kwa kusema: ‘Nabii na Imam wanahitajika kwa sababu gani?’ Imam alimjibu: ‘Kwa ajili ya kubakia ulimwengu katika hali bora inayofaa (kheri) na hilo ni kutokana na kuwa Mwenyezi Mungu huwaondolea walimwengu adhabu iwapo Nabii au Imam atakuwa miongoni mwao. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Na Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwaadhibu madamu wewe umo pamoja nao. Na Mtume (saw) amesema: ‘Nyota ni amani kwa watu wa mbinguni na Ahlul Beit wangu ni amani kwa watu wa ardhini (wanadamu). Hivyo nyota zikiondoka watu wa mbinguni hufikwa na wanachokichukia na Ahlul Beit wangu wakiondoka huwafika watu wa ardhini (wanadamu) wanachokichukia.’
Na kama mnavyoona wapenzi wasikilizaji, Imam Baqir (as) anatumia aya za Qur’ani na hadithi ya Mtume Mtukufu (saw) kubainisha kuwa haja ya kuwepo Nabii au Imam (as) ni jambo la dharura katika kuifanya dunia iendelee kuwepo kwa namna sahihi na inayohitajika na kutowafika wanadamu adhabu kali ya Mwenyezi Mungu kutokana na dhambi, ufisadi na umwagaji damu wao.
Kwa msingi huo inabainika wazi kwamba kuwepo Nabii au Imam katika kila zama ni katika rehema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Hii ni kwa sababu kuwepo maasumu miongoni mwa wanadamu huwaepusha na adhabu kali ya Mwenyezi Mungu kwa sababu huwaongoza walio na uwezo wa kuongoka na kuwashika mkono kuelekea kwenye mkondo wa kuomba maghfira na msamaha kutoka kwa Mungu muumba wa mbingu na ardhi kama inavyotuelezea hayo sehemu nyingine ya aya ya 33 ya Surat al-Anfaal iliyotumiwa na Imam Baqir kumjibu Jabir al-Ju’fi. Katika aya hiyo Mwenyezi Mungu anasema wazi kwamba waadamu kuepushwa na adhabu yake kunatokana na kuwepo Mtume Mtukufu (saw) miongoni mwao na wao kutubu dhambi zao.Tutabainisha zaidi suala hilo hivi punde.
*********
Hebu tuizingatie kwa pamoja aya hii ya 33 ya Surat al-Anfaal ambapo Mwenyezi Mungu anasema: Na Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwaadhibu maadamu wewe umo pamoja nao, wala hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaadhibu hali wanaomba msamaha.
Hapana shaka wapenzi wasikilizaji kwamba toba ya kweli ni kumrejea Mwenyezi Mungu na kumtii katika kila jambo na kuepuka maasi na dhambi. Kuthibiti kwa marejeo na utiifu huo bila shaka hutimia kwa kurejea na kuwatii watu ambao utiifu kwao ni sawa na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw). Kwa msingi huo mja mwema na maasumu anapasa kuwepo katika kila zama ili utiifu kwake uwe ni sawa na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na hili ndilo jambo analolibainisha Imam Baqir (as) katika kuendeleza hadithi tuliyotangulia kuinukuu ambapo anafafanua hadithi hiyo aliyoinukuu kutoka kwa babu yake Mtukufu Mtume (saw) kwa kusema: ‘Yaani kupitia Ahlul Beit wake Maimamu ambao Mwenyezi Mungu amefungamanisha itiifu kwao na utiifu kwake kwa kusema: Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi. Kisha akasema Imam (as): ‘Nao ni maasumu ambao hawafanyi dhambi wala kuasi, nao wanawezeshwa, kufanikishwa na kuongozwa. Kupitia kwao, Mwenyezi Mungu huwaruzuku waja wake, kuendelezwa ardhi yake, mvua kunyesha kutoka mbinguni na ardhi kutoa baraka. Kupitia kwao watenda dhambi hupewa muda na kutoharakishiwa ikabu na adhabu. Roho mtakatifu hatengani nao, nao hawatengani naye, hawatengani na Qur’ani wala Qur’ani kutengana nao (as).
***********
Kama manavyoshuhudia wapenzi wasikilizaji, Imam Baqir (as) anashiria katika hoja yake iliyotangulia kwamba kuwepo Imam masumu miongoni mwa watu katika kila zama huwaepusha na ikabu ya Mwenyezi Mungu hata kama Imam huyo hatakuwa anahudumia nafasi ya uimamu na madaraka ya kidhahiri. Hii ni kwa sababu kwa vyovyote vile yeye ndiye Imam na khalifa wa mwenyezi Mungu katika ardhi ambapo kupitia kwake hoja ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake hutimia. Kwa hivyo kuwepo kwake huwa ni sababu ya kuteremka na kushuka kwa baraka na riziki ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake na kila wanachokihitajia kwa ajili ya kudumisha maisha yao humu duniani. Kupitia kwao Mwenyezi Mungu huwapa waja wake na hata wanaomuasi, fursa ya kutubu na kurejea kwake ili hatimaye waweze kufanikiwa na kufuzu maishani kwa ajili ya saada yao ya mwisho huko Akhera. Na marejeo hayo baada ya kutubu hutimia kwa kumrejea khalifa wa Mwenyezi Mungu kwenye ardhi yake ambaye kamwe hatengani na mwongozo wa Mwenyezi Mungu kwa hali yoyote ile. Hivyo Imam aliye na sifa hizo huwa na uwezo wa kumfikisha mbele ya Mwenyezi Mungu kila mja aliyetubia na kumrejea Mola wake kwa dhati na nia safi.
*********
Kwa msingi wa mambo tuliyojifunza hadi sasa, jibu la swali la kipindi cha juma hili lililohusiana na haja ya kuwepo Imam maasumu katika kila zama linabainika wazi. Haja au sababu ya suala hilo ni kutokana na rehema kubwa aliyonayo Mwenyezi Mungu kwa waja wake, ambayo ilimpelekea kumteua khalifa wake katika ardhi ambaye kutokana na mwongozo wake na kutotenda kwake dhambi kunakomfanya awe na uhusiano wa moja kwa moja na Mungu Muumba, kila mtu aliye na hamu ya kumrejea Mwenyezi Mungu na kufanikiwa maishani humrejea Imam huyo kwa lengo la kumuondoa kwenye upotovu na kumuepusha na ikabu ya Mweyezi Mungu pamoja na kupata wongofu na ridhaa yake.
Na kwa maelezo hayo wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi cha juma hili cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kama kawaida kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena katika kipindi kingine juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyito wapenzi wasikilizaji kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.