Apr 22, 2019 01:33 UTC
  • Jumatatu, 22 Aprili, 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 16 Sha'aban 1440 Hijria mwafaka na tarehe 22 Aprili 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 295 iliyopita, alizaliwa mjini Königsberg, Ujerumani na katika familia ya kati Immanuel Kant, mwanafalsafa mkubwa wa nchi hiyo. Baada ya kuhitimu masomo yake katika fani ya hisabati, theolojia na falsafa Kant alijishughulisha na kazi ya ufundishaji vijijini. Baadaye na akiwa na umri wa miaka 46 msomi huyo alifanikiwa kuwa muhadhiri wa falsafa katika chuo kikuu cha mji alikozaliwa wa Königsberg. Katika miaka yote ya utafiti wake na kufundisha falsafa, alipata kuandika vitabu tofauti ambavyo baadhi vipo katika maktaba kubwa duniani. Kadhalika mwanafalsafa huyo mkubwa alifanikiwa kuasisi mfumo wa kifikra maalumu katika uga huo. Kwa imani ya Immanuel Kant, ndani ya mwanadamu kuna hisia maalumu ya kitabia ambayo huweza kutoa hukumu kwamba kitendo hiki ni chema na kile ni kiovu. Hii ikiwa na maana kwamba, mwanadamu binafasi anaweza kutenda mema na maovu, lakini ile hisia yake ya kitabia ndio huweza kumueleza kwamba kitendo fulani ni chema au kibaya na kwamba lau kama si kuwepo kwa hisia hiyo, basi mwanadamu asingeweza mwenyewe kujilaumu baada ya kutenda jambo fulani. Immanuel Kant alifariki dunia tarehe 12 Februari 1904 mjini Königsberg akiwa na umri wa miaka 80 huku akiwa ameishi maisha yake yote akiwa kapera (yaani bila kuoa.) ***

Immanuel Kant,

Miaka 124 iliyopita katika siku kama ya leo, wananchi wa Cuba kwa mara nyingine tena walianzisha mapambano ya kupigania uhuru wao kutoka kwa wakoloni wa Uhispania. Hayo yalikuwa mapambano yao ya tatu katika nusu ya pili ya karne ya 19 Miladia kwa ajili ya kutaka kujitawala. Uhispania ilituma wanajeshi laki tatu nchini humo kwa ajili ya kupambana na wanamapinduzi hao. Kufuatia vurugu hizo Marekani ilitumia fursa hiyo na kwa kisingizio cha kulipuliwa meli yake ya kivita karibu na pwani ya Cuba mwaka 1898 Miladia, kuingia katika vita hivyo dhidi ya Uhispania. Manowari za kivita za Uhispania ziliangamizwa katika maji ya Cuba na hatimaye nchi hiyo ya Amerika ya Latini ikakaliwa kwa mabavu na Marekani. ***

Bendera ya Cuba

Katika siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, alizaliwa mwanafizikia na mtengenezaji wa bomu la atomiki wa Marekani Robert Oppenheimer. Kabla ya Vita vya Pili vya Dunia mtaalamu huyo alifanya utafiti kuhusiana na jinsi ya kupasua atomu na kupata nishati ya nyuklia. Wakati wa vita hivyo alipewa wadhifa wa kusimamia kitengo cha utafiti katika Wizara ya Vita ya Marekani na chini ya usimamizi wake yakatengenezwa mabomu matatu ya kwanza ya nyuklia. Hata hivyo, wakati Marekani ilipoishambulia Japan kwa mabomu ya nyuklia mwaka 1945, makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia waliuawa katika kipindi kifupi, hali iliyomfanya Oppenheimer kujutia kitendo chake hicho na akatoa wito wa kutumiwa nishati ya atomiki katika masuala ya amani. ***

Robert Oppenheimer

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, yaani tarehe 22 Aprili 1948, Wazayuni waliushambulia mji wa bandari wa Haifa huko kaskazini magharibi mwa Palestina wakati wa kukaribia kuanzishwa utawala haramu wa Israel. Wazayuni waliwauwa shahidi Wapalestina 500 katika mashambulizi hayo makubwa na kuwajeruhi wengine 200 ambao walikuwa wanawake na watoto waliokimbilia huko Haifa wakisubiri kupelekwa katika maeneo mengine. ***

Bandari ya Haifa

Na miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo, Imam Ruhullah Khomeini (M.A) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuundwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH). Kwa mujibu wa amri hiyo, jukumu kuu la jeshi hilo ni kulinda Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya maadui wa ndani na nje. Baada ya kuundwa, jeshi la SEPAH lilikabiliana na makundi yaliyopinga Mapinduzi ya Kiislamu, yaliyoanzisha mapigano ya silaha katika pembe mbalimbali za Iran na kuweza kuzima njama za maadui. Aidha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi liliweza kudhihirisha uwezo wake mkubwa wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na utawala wa dikteta Saddam Hussein wa Iraq kwa lengo la kuyaangamiza Mapinduzi ya Kiislamu na kuigawa Iran. ***

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH)