May 03, 2019 00:10 UTC
  • Ijumaa Mei 3 2019

Leo ni Ijumaa tarehe 27 Sha'aban 1440 Hijria mwafaka na tarehe Mei 3 2019.

Siku kama ya leo miaka 614 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Ibn Araqi fakihi na kadhi wa Kiislamu wa Misri aliaga dunia katika mji wa Makka. Alizaliwa mwaka 762 na alihudhuria darsa na masomo ya wanazuoni mashuhuri wa zama hizo katika elimu ya hadithi. Ibn Araqi baada ya kunufaika na elimu ya walimu wa zama hizo alifanikiwa kuingia katika faharasa ya maulama mashuhuri na kuanza kufundisha elimu za fikihi na hadithi.  Msomi huyo ameandika vitabu kadhaa kwa lugha ya Kiarabu.

 

Siku kama ya leo miaka 590 iliyopita, Jeanne d'Arc alianzisha harakati ya kihistoria ya kuzikomboa baadhi ya ardhi za Ufaransa zilizokuwa zikikaliwa kwa mabavu na Uingereza. Jeanne d'Arc alikuwa kamanda wa jeshi ambaye alipewa jukumu na Mfalme wa Ufaransa la kuongoza mapambano dhidi ya majeshi ya Uingereza yaliyolikalia kwa mabavu eneo la kaskazini mwa Ufaransa. Hatimaye Kamanda huyo alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kimaonyesho nchini Uingereza kwa tuhuma za kuritadi na kuacha dini na mwaka 1431, aliuawa kwa kuchomwa moto akiwa hai.

Jeanne d'Arc

 

Siku kama ya leo miaka 550 iliyopita alizaliwa Niccolò di Bernardo dei Machiavelli, mwanahistoria na mwanasiasa wa Italia katika mji wa Florence. Sambamba na shughuli zake za kisiasa, Machiavelli aliandika pia historia ya Florence. Katika mtazamo wa kisiasa, Machiavelli alikuwa akiamini kwamba yawezekana kutumia wenzo wowote ule kwa ajili ya kupata madaraka na kwa ajili ya kuyalinda, na kwamba hakuna udharura wowote wa kuheshimu misingi ya maadili katika masuala kama hayo. Miongoni mwa kazi za mwanahistoria na mwanasiasa huyo wa Italia ni "The Art of War" na "The Prince."

 

Siku kama ya leo miaka 504 iliyopita yaani tarehe 3 Mei 1515 Miladia, manowari za Ureno zilianza kushambulia kisiwa cha Hormoz cha Iran na hivyo kuanzisha wimbi la uingiliaji na ukoloni wa nchi za Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati. Kisiwa hicho kiko katika eneo la kiistratijia la lango la Hormoz lililoko katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman, kusini mwa Iran. Kutokana na kuwa Iran ilikuwa dhaifu katika upande wa jeshi la majini, wakoloni wa Kireno walivikalia kwa mabavu visiwa kadhaa vya Iran vilivyoko katika Ghuba ya Uajemi, kikiwemo cha Bahrain ambacho wakati huo kilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Hatua kwa hatua, Iran iliimarisha jeshi lake la majini, na ilipofika mwaka 1652, iliweza kuvikomboa visiwa vyote vilivyokuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno.

Na siku kama ya leo miaka 212 iliyopita ulitiwa saini Mkataba wa Finckenstein kati ya Iran na Ufaransa wakati mfalme Napoleon wa Ufaransa alipokuwa katika vita na nchi nyingine za Ulaya. Kwa mujibu wa mkataba huo uliokuwa na vipengee 16, ilipangwa kuwa Iran ingepata silaha za aina mbalimbali kutoka Ufaransa kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya Warusi. Ufaransa pia iliahidi kutuma wataalamu wa mizinga na wahandisi wa masuala ya kijeshi nchini Iran kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa jeshi la nchi hii. Kwa upande wake, Iran iliahidi kukata uhusiano wake na Uingereza na kuisaidia Ufaransa katika kupeleka majeshi yake huko India.